The House of Favourite Newspapers

JAY-Z JAY-Z ANALITEKA SOKO LA SOKA

Rapa Jay-Z.

WIKI iliyopita kulikuwa na taarifa kuwa beki raia wa Cote d’Ivoire au Ivory Coast na Manchester United, Eric Bailly amesaini mkataba na Kampuni ya Roc Nation Sports, hiyo ni kampuni ambayo inamilikiwa na rapa Jay-Z.

 

Bailly, 24, ameungana na mastaa wengine wa soka katika kampuni hiyo ambao ni Romelu Lukaku anayecheza naye Man United pamoja na beki wa Bayern Munich, Jerome Boateng.

 

Mara baada ya kujiunga Roc Nation, Lukaku alitumia ukurasa wake wa Twitter kumkaribisha kwa kuandika: “Nakukaribisha kwa furaha kwenye familia yetu ya Roc Nation Sports, ndugu yangu na mchezaji mwenzangu Eric Bailly.”

Awali ilionekana kama maajabu wakati Jay-Z alipokuwa akianzisha kampuni hiyo ambayo ipo chini ya kampuni mama ya Roc Nation.

Kampuni nyingine ambazo nazo zipo chini ya Roc Nation ni Roc Nation Records na StarRoc. Katika moja ya mashairi yake kwenye nyimbo zake, Jay-Z ambaye jina lake halisi ni Shawn Corey Carter, aliwahi kusema yeye siyo mfanyabiashara bali yeye ni ‘biashara’, kwa wanaomfuatilia kwa ukaribu wanaweza kuelewa kwa nini anajiita kuwa yeye ni biashara.

 

Jay-Z amepata mafanikio makubwa katika muziki wa Hip Hop na ndiyo maana popote jina lake linapotajwa na yeye kuhusika, tambua kuwa kuna fedha inaingia kwake, alipoanzisha Roc Nation mwaka 2008, lengo lake kubwa lilikuwa kwenye upande wa burudani.

 

Kampuni hiyo iliyoanzishwa New York nchini Marekani na ndipo makao makuu yake yalipo, hadi sasa ina ofisi katika majiji mengine makubwa kwenye nchi tofauti ambayo ni London (England), Nashville, Austin na Los Angeles yote yapo Marekani.

Ilipoanzishwa Roc Nation kazi yake kubwa ilikuwa ni burudani hasa muziki, na ndiyo maana kuna wasanii wengi wakubwa wamewahi kuwa chini ya lebo ya Roc Nation na wengine bado wapo, baadhi yao ni J. Cole, Big Sean, Shakira, DJ Khaled, Omarion, T.I na Kanye West. Jay-Z aibuka kwenye michezo Katika mahojiano yake ya nyuma, Jay-Z aliwahi kunukuliwa akisema: “Kuna siku niliamka asubuhi na kujiuliza, nimefanya muziki kwa miaka mingi na ninaendelea kufanya, lakini nafikiri inatakiwa ifike hatua niwe nafanya kazi ya kila siku, kutoka nyumbani kwenda ofisini ndipo wazo la Roc Nation likaja.

“Ilipoanzishwa Roc Nation kulikuwa na ndoto nyingi na mipango mingi pia, lakini yote huwezi kuifanya kwa wakati mmoja, napenda michezo na ndiyo maana nilikuwa na mpango wa kuwekeza kwenye michezo.”

 

Roc Nation Sports yaanza Baada ya mafanikio ya kampuni mama, mwaka 2013, Jay-Z akaanzisha kampuni hii ambayo kazi yake itakuwa ni kushirikiana na wanamichezo katika kuwapa mikataba ya matangazo ya biashara na jinsi ya kukuza ustaa wa mchezaji. Baada ya kuanza mdogomdogo kampuni hiyo hadi sasa imeshaingia mikataba yenye thamani ya dola 900m (Sh trilioni 2).

 

Kasi ya Jay-Z imeanza kuwatisha mawakala wa wachezaji maarufu wakiwemo Mino Raiola na Jorge Mendes, ambao wao kazi yao kubwa ni kusimamia mikataba ya wachezaji na timu, lakini kampuni ya Jay-Z yenyewe inajihusisha na masuala ya biashara ya wachezaji.

 

Tishio hilo ni kwa kuwa inaonekana rapa huyo ambaye ana umri wa miaka 49, anaweza kuendelea kutumia nguvu kubwa ya jina lake kuwashawishi wanamichezo mbalimbali kumkubalia maombi yake pindi anapotaka kuwekeza kwao, pia nia yake ya kuwekeza fedha nyingi imeonyesha jinsi ambavyo alivyo makini na mchakato huo.

 

Akiwa na tuzo 21 za Grammy na ngoma kibao zilizowahi kutamba ikiwemo Hard Knock Life, Jay-Z ambaye ni mume wa Beyonce, anaonekana kuwa na nia ya kuendelea kuwatafuta wanasoka ili kuingia katika kampuni yake.

 

Awali, alianza na wachezaji wa kikapu kwa kuwa ndiyo mchezo unaopendwa zaidi Marekani, baadaye akahamia kwenye michezo mingine ikiwemo ndondi, baseball na American Football ambao nao unapendwa sana nchini mwake, kisha ndiyo akageukia soka.

 

Jay-Z anajua kuwa akiushika mchezo wa soka ataweza kutanua soko lake kwa haraka kwa kuwa ndiyo mchezo wenye wafuasi wengi duniani kuliko mingine yote. Mwaka 2017, kampuni yake iliwahi kutajwa kuwa inashika nafasi ya 33 katika kampuni za michezo zenye nguvu duniani, lakini idadi ya wachezaji inavyoongezeka na thamani ya mikataba yao inavyokuwa kubwa ndivyo thamani ya kampuni inavyopanda pia.

 

Rais wa Roc Nation Sports, Juan Perez alipoulizwa vigezo wanavyotumia kumpa mkataba mchezaji, alisema: “Tunatazama uwezo wake uwanjani, kuna levo fulani ambayo mchezaji anatakiwa kuwa nayo, baada ya hapo tunaangalia historia yake ya nyuma, tabia, thamani ya soka lake na mambo mengine kadhaa.”

 

Staa wa kwanza kusainiwa Staa wa baseball, Robinson Cano alikuwa mwanamichezo wa kwanza kusainiwa na kampuni hiyo Aprili 2013, alipokuwa akiichezea New York Yankees. Baadaye alihamia Seattle Mariners alipo hadi sasa.

 

Kevin Durant yumo Mkali wa kikapu katika timu ya Golden State Warriors, Kevin Durant ambaye ameshashinda tuzo kadhaa katika Ligi ya NBA, alijiunga na kampuni hiyo Juni 2013 na bado ni mwanachama. Ilibidi Jay-Z auze hisa Katika kile ambacho kilionyesha kuwa aliamua kweli kuwekeza kwenye kampuni yake ya michezo, Jay-Z alilazimika kuuza hisa zake za umiliki wa timu ya kikapu ya Brooklyn Nets ili kuondoa maslahi binafsi ya kuwa mmiliki wa timu na wakati huohuo ni wakala.

 

Soko la soka analiteka taratibu Kwenye soka, mtu wa kwanza kusainiwa alikuwa Boateng, ambaye alijiunga Julai 2015. Baada ya kusaini mkataba, Boateng alikaribishwa kutembelea ukumbi wa burudani na michezo wa 40/40 Club uliopo Brooklyn ambao unamilikiwa na Jay-Z.

 

Wakiwa hapo walizungumza na rapa huyo huku Boateng akiwa na familia yake. Hivyo, tayari ameanza kupata wawakilishi katika ligi mbili kubwa za soka, Premier League na Bundesliga, inavyoonekana anajua nguvu yake katika kufanya muziki inaweza kupungua kwa kuwa vizazi vinabadilika, ndiyo maana sasa anapambana kupata wachezaji wakubwa mastaa ili kampuni yake ikue zaidi.

 

Roc Nation ambayo ina miaka 11 sasa, ipo chini ya utendaji wa watu makini ambao ni Jay Brown huyu ni Mtendaji Mkuu (CEO) na Michael Yormark ambaye ni rais wa kampuni. Huyu ndiye Jay-Z Kuzaliwa: Desemba 4, 1969 Majina mengine: Hova, Jigga Kuanza muziki: 1994 Biashara nyingine: Mbali ya kumiliki 40/40, pia anamiliki kampuni ya nguo ya Rocawear na mtandao wa muziki wa Tidal. Utajiri wake: Dola 900m (Sh trilioni 2) Alichoingiza mwaka 2018: Mwaka 2018 aliingiza dola 76.5m (Sh bilioni 176) kutokana na dili zake mbalimbali za muziki na uwekezaji.

Comments are closed.