The House of Favourite Newspapers

JECHA ANG’ATUKA ZEC

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha amestaafu baada ya kumaliza muda wake wa majukumu ya tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Aprili 30, 2013 hadi Aprili 29, 2018 ambapo yeye na wajumbe wa tume hiyo wamekabidhi ripoti yao ya kazi kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.

 

Akitoa taarifa yake, Jecha amesema ZEC inaamini kuwa, mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa majukumu yake hasa ya uchaguzi yalitokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali na wananchi kwa jumla.

 

“Katika miaka mitano, ZEC imeweza kuendesha jumla ya chaguzi ndogo nne, zikiwemo tatu za udiwani na moja ya uwakilishi pamoja na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na ule wa marudio yake Machi 20, 2016. Tume imefanya mapitio ya majimbo ya uchaguzi na kubadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi, majina ya majimbo na kuongeza idadi ya majimbo kutoka 50 hadi 54″, ameeleza Jecha.

 

“Tume imeweza kufanya uandikishaji wa wapiga kura kwa awamu mbili na kuendeleza daftari la kudumu la wapiga kura. Pia imeendesha programu mbalimbali za elimu ya wapiga kura kupitia vyombo vya habari, mikutano ya wadau, uchapishaji wa vipeperushi, majarida na makala mbalimbali”.

 

Pia Jecha alisema ZEC imechaguliwa kuwa kiongozi wa Uchaguzi Mkuu wa nchini Congo utakaofanyika mwezi Disemba mwaka huu.

 

Aidha, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ameipongeza Tume hiyo kwa kutekeleza vyema majukumu yake ndani ya miaka mitano kwa kuendesha chaguzi zote .

 

“Tume hii inastahili pongezi kwa kufanikisha vyema kazi waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuendesha chaguzi zote ukiwemo uchaguzi Mkuu, chaguzi ndogo na ule uchaguzi wa marudio ambazo zote hizo zilifanywa kwa ufanisi mkubwa”, amesema Dkt. Shein.

 

Wajumbe wa tume hiyo ambao wamemaliza muda wao ni Mwenyekiti mwenyewe Jecha Salim Jecha, Jaji Abdul-hakim Ameir Issa, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Nassor Khamis Mohammed, Ayoub Bakari Hamad, Haji Ramadhan Haji na Salmin Senga Salmin ambao wote hao waliapishwa rasmi  Mei, 4, 2013.

Comments are closed.