The House of Favourite Newspapers

Jeraha Lililojeruhiwa Nchini Ethiopia

0

MACHO ya Mr Johnson, mtafiti wa miamba madini na mafuta yalitulia katika darubini kwa muda na kusahau alichokikusudia kwa wakati ule. Umbile changa la binti wa Kihabeshi liliushtua moyo wake na kujikuta akimvuta zaidi na kugundua ni binti mdogo sana lakini mwenye umbile zuri.

Akilini mwake kuna kitu kiliingia na kuona kuna kitu cha ziada kutoka kwa binti yule maskini, kilichojificha ambacho mtu wa kawaida asingeweza kukiona kutokana na mavazi na hali yake duni.

Alimuomba rubani ateremshe helikopta eneo lile la pembezoni mwa Ziwa Chamo lililokuwa karibu na mji wa Arba Mich nchini Ethiopia, eneo lilikuwa likisemekana linaweza kuwa na mafuta ambalo lilikuwa katika utafiti wa Kampuni ya Caltex ya Kimarekani.

“Mikias hebu teremsha helikopta kwenye kundi lile la ng’ombe.”
“Mr Johnson mbona si eneo husika?” rubani alihoji baada ya kuona helikopta inateremshwa eneo lisilo husika.

“Kuna kitu nimekiona.”
Rubani Mikias aliiteremsha ndege hiyo pembeni kidogo ya kundi la ng’ombe, mbuzi na kondoo lililokuwa likichungwa na binti mdogo aliyekuwa amesimama pembeni akiangalia mifugo hiyo iliyokuwa ikila majani. Hata ilipotua chini binti yule hakushtuka zaidi ya kushangaa.

Baada ya kutua, Mr Johnson alifungua mlango na kuteremka huku rubani wake akitaka kujua anataka kufanya nini. Alijiuliza ameona nini sehemu ile iliyokuwa na kundi la ng’ombe, mbuzi na kondoo. Naye aliteremka ili kujua mgeni wake alitaka kufanya nini.
“Mikias kuna kitu nataka kujua kwa binti huyu mchunga ng’ombe.”

“Aah, Johnson huyu binti maskini asiye na elimu atakusaidia nini?”
“Kuna kitu nimekiona kwake ambacho kwa macho ya kawaida huwezi kukiona.”
“Kitu gani? Au umempenda mbona bado binti mdogo tena hana hadhi?”
“Hata nikikueleza hutanielewa, naomba msaada wa kuzungumza naye nina imani Kiingereza haelewi.”

“Sawa.”
Waliwapita ng’ombe na kumsogelea binti yule aliyekuwa ameshikilia bakora na kibuyu kidogo cha maji alichokuwa amekining’iniza begani. Kwa vile Mikias alikuwa akijua lugha ya Kiwolayta alimsalimia yule msichana.
“Hujambo.”

“Sijambo.”
Mikias alimgeukia Johnson aliyekuwa bado akiutathmini mwili wa yule binti aliyekuwa amevalia mavazi ya ngozi ya ng’ombe iliyokuwa imenakshiwa na shanga iliyokuwa imesitiri sehemu chache za mwili na kuliacha eneo kubwa la mwili kuwa wazi.

“Mr Johnson ulikuwa una shida gani?” Mikias alimgeukia Johnson kumuuliza.
“Naomba nitakachomuuliza umuulize bila kuongeza wala kupunguza neno.”
“Hakuna tatizo.”

“Unaitwa nani?”
“Zinash.”
“Una umri gani?”
“Miaka kumi na tano.”

“Unasoma?”
“Hapana.”
“Kwa nini husomi?”
“Familia yangu imeshindwa kuniendeleza na masomo.”
“Kwa sababu gani?”

“Haina pesa ya kunisomesha.”
“Umeishia darasa la ngapi?”
“Elimu ya msingi.”
“Unajua kuzungumza Kiingereza?”
“Kidogo sana.”

“Nikikuendeleza kimasomo utakubali?”
“Mpaka baba akubali.”
“Lakini wewe upo tayari?”
“Ndiyo.”
“Unakaa wapi?”
“Migie.”

“Eti Migie ndiyo wapi?”
“Mbele kidogo,” Mikias alisema huku akimuonesha sehemu ulipo mji wa Migie.
“Ooh!”

“Basi nataka kuonana na wazazi wako, unamaliza kuchunga saa ngapi?”
“Mchana kaka anakuja kunipokea mi narudi nyumbani kuendelea na kazi zingine.”
“Pale unakaa kwa mzee nani?”
“Natnael Behailu.”

Waliagana na yule binti kwa kumuachia kiasi kidogo cha pesa, wakiwa ndani ya helikopta bado Mikias alikuwa hajamuelewa Johnson.
“Bado sijakuelewa naona umemuuliza maswali ambayo nimeona hayana tija kisha tumeondoka.”

“Mikias yule binti ni mgodi unaotembea, kama nilivyo mtaalamu wa kugundua madini ardhini nimeona kitu kingine chenye utajiri wa muda mfupi.”
“Madini? Ina maana gani?”
“Mikias mimi si mtaalamu wa kurusha ndege hivyo nauheshimu uwezo wako wa kujua ndege iruke usawa gani au hali ya hewa ikiwa mbaya ufanyeje, lakini mimi siwezi kujua kitu.”

“Ni kweli, lakini bado siamini kama mwanadamu ana madini mwilini yanayoweza kuchimbwa kama almasi au dhahabu.”
“Ndani ya miaka minne ijayo Zinash ataishika dunia mkononi mwake.”
“Mr Johnson unataka kunichekesha, aishike dunia kivipi?”

“Kwa muonekano wake nimevutiwa naye nataka nisimamie maisha yake na kuipandisha Ethiopia kwa mlango mwingine baada ya riadha ambayo imefanya vizuri katika mbio ndefu sasa itakuwa katika utalii.”

“Unataka kuibadili vipi?”
“Kwanza kabisa nataka kumuongezea elimu ili akirudi nyumbani aweze kuchangia katika kunyanyua uchumi wa Ethiopia.”
“Mmh, ngoja tuone, kama ungetaka mtu wa kumsomesha si ungesema nikutafutie mjini wenye mwanga kidogo kuliko huku kijijini kusiko na hadhi?”

“Jicho langu hutazama kilichojificha ambacho wewe huwezi kukiona hata ukipewa kiona mbali, Zinash ni zaidi ya almasi ni mgodi wa thamani unaotembea.”
Waliendelea na utafiti wa mafuta eneo lenye milima Gel’eme Kusini Mashariki ya Ziwa Abaya katika mji wa Arba Minch’.

Baada ya kukamilisha utafiti wa awali kwa kuweka alama sehemu zote zenye dalili za mafuta, walirudi ofisini kwa ajili ya kuandika ripoti.
Je, kiliendelea nini? Usikose Jumamosi ijayo hapahapa.
na kuiwasilisha makao makuu Caltex nchini Marekani.

Usikose wiki ijayo, gazeti hilihili.

Leave A Reply