The House of Favourite Newspapers

Jeshi la Polisi Lamsaka Mwanaume Aliyemtoboa Jicho Mkewe na Kumng’oa Jino

0

Jeshi la Polisi mkoani Arusha, linamsaka Isaack Mnyagi kwa tuhuma za kumtoboa jicho na kumng’oa meno mkewe, Jackline Mkonyi kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justin Msejo amenukuliwa akisema:

“Taarifa hizo zipo tunazifanyia kazi, tunaendelea kumtafuta mtuhumiwa kwa kushirikiana na wananchi, tunaamini mtuhumiwa anasoma mitandao na anaona kinachoendelea.”

Taarifa zilizosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Mei 23, 2023, Sombetini jijini Arusha, nyumbani kwa Jackline na mumewe.

Kwa mujibu wa Jackline, siku ya tukio alitembelewa na mjomba wake, Vincent Nicodemus ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu.

Mwanamke huyo ameeleza kuwa usiku wa siku hiyo, mumewe alirudi nyumbani akiwa na hasira na kumtaka amueleze alikuwa na nani siku hiyo, ambapo Jackline alimueleza kwamba alikuwa na mjomba wake.

Maelezo hayo hayakumridhisha mwanaume huyo ambapo alianza kumpiga kisha akamng’oa meno kwa kutumia ‘plaiz’ kabla ya kumtoboa jicho moja.

Baada ya kumtendea ukatili huo, alienda kumtupa getini, nyumbani kwa wazazi wake, Sinoni Daraja Mbili jijini Arusha ambapo baadaye alikimbizwa hospitali akiwa kwenye maumivu makali.

Baba wa Jackline, ameeleza kwamba alipigiwa simu na mume wa mwanaye kwamba ‘akachukue mzoga’ wa mwanaye getini, ambapo walipotoka walimkuta mtoto wao akiwa katika hali mbaya ambapo walimkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru ili kuokoa maisha yake.

Tukio hilo limeripotiwa polisi kwa jalada namba ARS/RB/5416/2023.

Leave A Reply