The House of Favourite Newspapers

Jeshi zima Simba hili hapa

MABOSI wa Simba wameweka wazi jeshi lao ambalo watalitumia kwa msimu ujao ambapo kikosi hicho kitaundwa na nyota 26 pekee. Simba wametangaza kikosi hicho ambacho ndiyo watakitumia kwa msimu ujao kwenye michuano yote ambayo watashiriki ikiwemo ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Mapinduzi na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Mtendaji mkuu wa Simba, Crescentius Magori ameliambia Championi Jumatano, kuwa wameshamaliza usajili wao wote ambapo kikosi chao kitaundwa na wachezaji 26 ambao wamewasajili mpaka sasa huku wakibakisha nafasi moja pekee ya usajili ambayo watamsainisha mchezaji katika kambi ya timu hiyo nchini Afrika Kusini.

“Usajili wetu umeshakamilika kwa asilimia 90 ambapo imebakia nafasi moja pekee ya kusajili. Usajili huo utafanyika kule Afrika Kusini ambapo tumepanga kuwapa furaha mashabiki wetu.

 

“Kikosi kizima kitakuwa na nyota 26 huku kukiwa na wachezaji kadhaa ambao tayari tumeshawapa mkono wa kwa heri. Wachezaji ambao hawatakuwepo ni pamoja na Marcel Kaheza ambaye anaenda kwa mkopo Polisi Tanzania, Paul Bukaba anayetimkia Afrika Kusini, Mohammed Rashid tunampeleka kwa mkopo JKT Tanzania na Adam Salamba aliyetimkia Afrika Kusini.

 

“Wengine ni Abdul Mohammed aliyekuwa kikosi cha vijana, Nicholaus Gyan, Asante Kwasi na Zana Coulibaly ambao tumeshazungumza nao kukatisha mikataba yao. “Wachezaji Haruna Niyonzima, James Kotei, Emmanuel Okwi wao mikataba yao imemalizika na tumewaruhusu kwenda kwingine na Salim Mbonde ambaye kocha ametaka akacheze sehemu nyingine,” alisema Magori.

 

Katika hatua nyingine, Magori amesema wamepeleka suala la aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wadThamini wa Simba Mzee Hamis Kilomoni kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili wamhoji juu ya msimamo wake wa kudai kuwa bado ni mdhamini wa Simba hali ya kuwa alishaondolewa toka Oktoba 2017. Waandishi: Said Ally, Issa Liponda na Musa Mateja.

Comments are closed.