JEURI SAKATA LA NYUMBA… MOBETO AMUONESHA MONDI

DAR ES SALAAM: Fedha inaongea! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Hamisa Mobeto kujilipua kwa kujilipia kodi ya nyumba ya mwaka mzima, Ijumaa limedokezwa.

 

Mobeto alimwaga ‘mpunga’ huo hivi karibuni baada ya kudaiwa kuwa, Diamond au Mondi alichomoa kumlipia kodi ya nyumba hiyo iliyopo Kunduchi-Beach jijini Dar. Diamond alipaswa kulipa kodi hiyo kwa sababu amezaa na Mobeto mtoto wa kiume aitwaye Dyllan kama sehemu ya masharti aliyopewa mahakamani.

 

VIJEMBE VILITAWALA

Kitendo cha Diamond kuchomoa kumlipia kodi Mobeto kilizua gumzo la aina yake mitandaoni huku wengi wakionekana kumnanga Mobeto kwa kuhisi ataaibika baada ya mzazi mwenzake huyo kukataa kulipa kodi.

 

TUJIUNGE NA CHANZO

Kwa mujibu wa mtu wa karibu na Mobeto, awali ilikuwa ahame katika nyumba hiyo kutokana na kushindwa kulipia kodi ya shilingi milioni moja kwa mwezi iliyokuwa inaishia Desemba, mwaka jana. “Ilikuwa ahame hapa mwezi wa 12 (mwaka jana) kwa sababu asingeweza kulipia kodi, si unakumbuka hapa alikuwa analipiwa na Diamond?,” kilinyetisha chanzo chetu cha kuaminika.

MONDI ALILIPIA MIEZI 6

Gazeti la Ijumaa linafahamu, Diamond alilipia kodi ya miezi sita katika nyumba hiyo ambapo ilipaswa kuisha Desemba, mwaka jana.

TAARIFA MPYA SASA

Wakati Gazeti la Ijumaa likianza kudodosa kama mrembo huyo ataweza kulipia kodi hiyo au la ndipo lilipobaini kwamba, ametunisha msuli na kulipia kodi ya mwaka mzima yaani shilingi milioni 12. “Huyu dada ana madili mengi sana hapa mjini, hiyo mlioni moja isingemshinda kulipa, amemuonesha Diamond jeuri kwamba anaweza kuishi bila msaada wake, si unakumbuka Diamond alishaanza vijembe kipindi kile kuhusu hii ishu ya kodi!’’ kilieleza chanzo hicho kilichoomba hifadhi ya jina.

 

HUYU HAPA MOBETO

Baada ya kunyetishiwa ubuyu huo ulioshiba, Gazeti la Ijumaa lilimvutia waya Mobeto ambapo alipopatikana na kuulizwa kuhusu suala hilo, aliishia kushukuru kisha akakata simu.

Ijumaa: Mambo vipi Misa (Mobeto)?

Mobeto: Poa.

 

Ijumaa: Hongera kwa kukamilisha malipo ya nyumba yako, maana watu walikuwa wanasema kwamba hutaweza kulipia kwa sababu kodi ni kubwa sana.

Mobeto: (Anaguna) kwani wewe nani?

Ijumaa: Mimi ni mwandishi wa habari kutoka Gazeti la Ijumaa.

Mobeto: (Anacheka) Asante. (akakata simu.)

 

MAMA’KE ANASEMAJE?

Hata hivyo, Ijumaa halikuishia hapo likampigia simu mama mzazi wa Mobeto, Shufaa Rutigunga ili alizungumzie hilo ambapo baada ya kupokea, mambo yalikuwa hivi;

Ijumaa: Habari yako mama Mobeto.

Mama Mobeto: Nzuri tu.

Ijumaa: Mama hongereni sana naona yametimia yale maneno uliyowahi kunukuliwa na Magazeti ya Global kwamba ile shilingi milioni 1 ya kodi ya nyumba haiwezi kumshinda mwanao.

Mama Mobeto: Wewe nani kwanza?

Ijumaa: Mimi ni mwandishi wa Gazeti la Ijumaa hapa Global Publishers.

Mama Mobeto: (Kwa sauti ya ukali kidogo lakini haikumtisha mwanahabari wetu) Hivi kwa nini mnapenda sana kumfuatilia mwanangu? Ina maana ninyi hamuwezi kufanya vitu vingine mpaka Hamisa tu? Ni hivi, nilishakwambia kwamba Misa (Mobeto) hawezi akashindwa kulipa hiyo shilingi Mil. 1 ya kodi, kwanza wewe unamuonaje? Siyo hiyo tu, mengi mazuri yanakuja. Mmeona? Tena amelipa kodi ya mwaka mzima sasa na bado mengi yanakuja, naomba mumpumzishe mwanangu ili naye afanye mambo yake.

 

Gazeti laIjumaa lilishindwa kuendelea kumhoji maswali mengi mama huyo kwa sababu baada ya kumaliza kuongea alikata simu na hata mwanahabari wetu alipojaribu kupiga tena, haikupatikana hewani. Alipotafutwa Mondi, simu yake iliita bila kupokelewa.

TUJIKUMBUSHE

Agosti 8, 2017, Diamond na Mobeto walifanikiwa kupata mtoto wa kiume aliyepewa jina la Dyllan ambapo baadaye wawili hao walimwagana.

Baada ya kumwagana na Diamond kuonekana hatoi matunzo kwa mwanaye, mwanzoni mwa mwaka jana, Mobeto alimburuza staa huyo wa Bongo Fleva katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar kudai matunzo. Hata hivyo, wawili hao walimalizana nje ya mahakama ambapo Diamond aliahidi kumpa matunzo mtoto huyo ikiwemo suala zima la kumlipia kodi ya nyumba.

 

Stori: MEMORISE RICHARD, IJUMAA

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO


Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment