The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-17

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Watu wanaposogea kule kulipokuwa na jeneza, kila mmoja alikuwa akimwagiwa unga usoni ili wale waliokuwa na nguvu ya kugundua kwamba yule aliyezikwa hakuwa mtu bali gogo au nyoka mkubwa, waweze kuuona mwili wa marehemu. Endelea…

Ndivyo ilivyokuwa, wakati tunasimama na kuanza kuelekea kwenye jeneza kuaga, tayari wachawi wakakimbia na kuelekea kule, wakajipanga mstari, walikuwa uchi wa mnyama, kila aliyekuwa akilisogelea jeneza lile, alipuliziwa unga fulani usoni mwake, unga wenye nguvu uitwao Yakumonzi wenye rangi ya njano.

Waliponiona nasogea kule lilipokuwa jeneza, hawakunimwagia unga ule, nilikuwa mtu wao, wakaniacha na hivyo kuangalia ndani ya jeneza. Nilichokifikiria ndicho kilichokuwa, kulikuwa na mgomba mkubwa ndani ya jeneza, sikushtuka, nikazidi kulia niliamini kwamba Thomas alikuwa nyuma ya mlango.

Nilipotoka hapo, sikutaka kubaki nje, nilichokifanya ni kwenda ndani kwao huku nikilia, nilipofika sebuleni, nikakaa kwenye kochi na kuangalia nyuma ya mlango. Nilimuona Thomas akiwa amesimama na mchawi mmoja.

“Thomas wangu! Thomas wangu kwa nini hili limetokea?” nililia huku nikiuliza, macho yangu yalikuwa yakiwaangalia wawili hao waliokuwa nyuma ya mlango.
“Nyamaza Davina, kazi ya Mungu haina makosa,” aliniambia Anita, tayari alikuwa ameingia ndani ya sebule ile.
***
Nilitakiwa kusahau kila kitu, nilitakiwa kusahau kuhusu Thomas, kitendo kile cha kufariki dunia huku akiwa mbele ya macho yangu kiliniumiza sana. Mlinzi na dada wa kazi walichukuliwa na kupelekwa polisi, walitakiwa kuelezea kilichokuwa kimetokea.

Hawakujua kitu, walipoulizwa kama Thomas alimchukua mtu na kwenda naye chumbani, hakukuwa na aliyekumbuka chochote kile. Nguvu kubwa ya kichawi ikawasahaulisha kila kitu, hawakutakiwa kukumbuka kitu chochote kile kuhusu mimi.
Walichokikumbuka ni kwamba Thomas alitembelewa na mtu mmoja ambaye aliingia naye ndani, walipotakiwa kusema alikuwa nani, walisahau kabisa. Hiyo ilikuwa ni kazi ya bibi, alitaka kuwasahaulisha kila kitu na kweli alifanikiwa.

Sikuwahi kuhisi kama hapo baadaye ningekuwa na furaha kabisa, kila siku nilikuwa mtu wa huzuni kwani kuchukuliwa kwa Thomas na kufanywa msukule, hakika kuliniumiza sana moyoni mwangu.

Baada ya miezi mitatu, kidogo nikaanza kusahau kuhusu Thomas, nikaendelea na maisha yangu na niliendelea kuroga kama kawaida. Ndugu yangu, kiukweli kwa kipindi hicho nilipenda sana kuroga, niliufurahia uchawi kuliko kitu chochote kile.

Maisha yaliendelea kusogea mbele, baada ya kipindi fulani, Mudi akanifuata na kunisisitizia kwamba bado alikuwa akinipenda mno. Sikutaka kukubaliana naye hata mara moja, nilimwambia ukweli kwamba kwa kipindi hicho sikutaka kuwa na mwanaume yeyote yule.

Mudi alikuwa king’ang’anizi, aliendelea kunisumbua lakini na mimi nikaweka msisitizo wangu kwamba haiwezekani kuwa naye. Mpaka tunafunga shule na kuingia kidato cha tatu, bado Mudi aliendelea kuniambia kwamba alikuwa akinipenda sana.

Niliendelea kumwambia kwamba sikutaka kuwa naye hata mara moja. Alilia sana lakini sikutaka kuwa na huruma hata mara moja, nilimwambia ukweli kwamba sikutaka kuwa na mwanaume yeyote yule.

“Mchawi huyo hapo,” nilimsikia mwanafunzi mmoja.
“Nani? Davina? Kumbe ndiye mchawi mwenyewe?” aliuliza mwanafunzi mwingine.
Kwanza nilishtuka, sikutegemea kusikia maneno kama hayo.

Nikageuka na kuwaangalia wasichana hao, walikuwa wamekaa chini na msichana ambaye alisema kwamba mimi nilikuwa mchawi alikuwa Agape, yule msichana aliyekuwa akimtaka Thomas.

Nilikasirika mno, sikuweza kuvumilia, kweli nilikuwa mchawi lakini sikutaka mtu aniambie kwamba mimi ni mchawi hivyo nikaanza kumfuata. Alijua kwamba namfuata yeye, alichokifanya ni kusimama kibabe na kuanza kuniangalia.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply