The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-9

0

ILIPOISHIA
“Kama hautaki kuwa mchawi, binti yako atachukua hii mikoba,” alisema bibi huku akionekana kumaanisha alichomwambia mama.
“Hawezi kuwa mchawi, Davina hawezi kuwa mchawi.”
“Tutaona.”ENDELEA…

Baada ya miaka saba, hatimaye nikaanza kujitambua, nikaanza kutambua mimi ni nani na nilitakiwa kufanya nini, yaani, kwa kifupi ni kwamba nilitambua baya lipi na jema lipi.

Nilianza masomo ya darasa la kwanza katika shule moja iitwayo Makurumla iliyokuwa Mwembechai jijini Dar. Hapo, nilipata marafiki wengi waliokuwa na uwezo wa kawaida darasani.

Mama alinipenda sana, alinipa mapenzi ya dhati, kila nilipohitaji kitu fulani, alinipa pasipo tatizo lolote lile. Kwa kipindi hicho bado mzee Abdallah aliendelea kuwa na mama, alinichukulia kama mtoto wake wa kumzaa na nilimheshimu mno kwani nilijua kwamba alikuwa baba yangu.

Nakumbuka kuna siku nilitoka shuleni, nilikuwa nimechoka mno na nilihisi kichwa kikianza kuniuma, nilipofika nyumbani, nikaelekea chumbani na kuamua kulala. Siku hiyo niliogopa sana na mwili ulinisisimka, ndoto niliyoota ilinitisha sana.

Nilimuona mwanamke mmoja mzee, alikuwa amesimama mbele yangu, mikono yake ilijaa damu, alikuwa akiniangalia huku akinionyeshea tabasamu pana, sikuona upendo wowote ule ndani yake, mikono yake ilijaa damu, kwa nini anionyeshee tabasamu lile, kwangu nililichukulia kuwa tabasamu la kinafiki.

Nililia sana, kila nilipomwangalia, alinitisha, alisimama juu ya kaburi moja kubwa, kaburi ambalo hata maiti iliyozikwa ndani ilionekana vilivyo. Pembeni ya mwanamke yule kulikuwa na tunguri kubwa huku akiwa na mkoba mmoja mkubwa mkononi mwake, akaanza kuniita na kuniambia nichukue mkoba ule.
“Mimi?” nilimuuliza.

“Ndiyo! Njoo mjukuu wangu,” aliniambia mwanamke yule mzee, sikuwa nimejua kama alikuwa bibi.Sikutaka kumsogelea, alinitisha sana, nilibaki nikitetemeka pale niliposimama, nilijiuliza juu ya mwanamke yule alikuwa nani na ule mkoba ulikuwa na nini mpaka kunitaka nimfuate na kunigawia, sikutaka kufanya hivyo.

Aliniita tena na tena, sikutaka kumsogelea, niliendelea kusimama pale niliposimama. Baada ya kunibembeleza sana kwa kuniita, tena kwa kuniambia maneno ambayo kwangu yalikuwa matamu, nikaanza kumsogelea, nikainyoosha mikono tayari kwa kuupokea mkoba ule.

“Davina….Davina…Davina….” nilisikia sauti, niliifahamu, ilikuwa sauti ya mama yangu, hapohapo nikajikuta nikirudi nyuma katika ndoto ile na ghafla nikashtuka kutoka usingizini huku nikiwa ninatweta kwa jasho jingi.
“Davina…nini binti yangu?” aliniuliza mama huku akinipima joto la mwili wangu kwa kutumia mkono wake.

“Mama! Mama…” nilimuita, jasho lilinitiririka kwa wingi.
“Kuna nini?”
“Mkoba! Kuna mwanamke alitaka kunipa mkoba,” nilimwambia mama ambaye alionekana kushtuka mno.

Mama aliniangalia, alionekana kunihurumia, hapohapo akakunja uso wake, alionekana kufahamu kila kitu, hakuzungumza kitu, alichokifanya ni kuniambia kwamba alileta chakula na hivyo nilitakiwa kula, nioge ili nilale kwani usiku ulikuwa umeingia.

Nilipomaliza kula, nikaenda chumbani kwangu na kulala. Sikumbuki ilikuwa muda gani, ghafla nikaanza kusikia sauti za paka wengi nje. Ni kweli kwa uswahilini kama tulipokuwa tukiishi kulikuwa na paka wengi lakini siku hiyo, milio yao ilinishtua sana.

Kulikuwa na paka waliokuwa wakilia kama watoto lakini pia kulikuwa na paka waliokuwa wakilia kwa kuliita jina langu. Nilishtuka sana, sikujua nini kilikuwa kinaendelea mpaka paka wale kulia kwa kuliita jina langu.

Nikashtuka, mapigo yangu ya moyo yakaanza kudunda na hivyo kumwamsha mama kwani nisingeweza kulala tena.
“Mama…mama…” nilimwamsha.
“Abee binti yangu.”

“Paka…nasikia paka,” nilimwambia mama, bado sauti za paka zilisikika lakini kitu cha ajabu mama hakusikia hata mara moja.
“Unasemaje?”
“Nasikia paka wananiita.”
“Paka?”
“Ndiyo mama.”

“Wapo wapi?”
“Huwasikii hao wanalia?”
“Hapana!”
“Mama! Nawasikia paka wakilia,” nilimwambia mama.

Leave A Reply