The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi -54

0

Kofia yake haikutoka kichwani mwake, bado hakuhitaji kujulikana, kila kitu kilikuwa siri kubwa kwake, walipofika mapokezi, akalipia chumba na kwenda chumbani tayari kwa kufanya kile kilichowapeleka pale.

“Naruhusiwa kuweka masharti kama mteja?” aliuliza Dickson.
“Kama lipi?”
“Napenda kufanya gizani, sipendi taa.”
“Kweli?”

“Ndiyo!”
“Hata mimi napenda giza, hakuna tatizo,” alisema msichana huyo kwa furaha, tena huku akionekana kuchangamka sana, kwa muonekano wake tu, alionekana kuwa na kitu nyuma ya pazia, Dickson hakuelewa hilo.

Pamela hakuamini kile alichokisikia kwamba rafiki yake kipenzi alikutwa akiwa amekufa porini huku mwili wake ukiwa umezikwa. Mara ya kwanza hakuamini kile alichokisikia lakini baada ya yeye na mashoga zake kwenda hospitali kuutambua mwili huo, hapo ndipo alipoamini kwamba rafiki yake huyo kweli alifariki dunia.

Moyo wake ukawa kwenye majonzi mazito, alibaki akilia tu, alimzoea sana Magreth, japokuwa hawakuwa marafiki kwa zaidi ya mwaka lakini walizoeana vya kutosha. Harakati za mazishi zikaanza kufanyika, hakukosa kwenye msiba huo, alikwenda kila hatua mpaka pale mwili wa Magreth ulipozikwa katika Makaburi ya Mburahati jijini Dar es Salaam.
Kwa kuwa alikuwa kwenye kipindi cha majonzi, hakutaka kwenda sehemu yoyote ile, alisimamisha kazi yake ya kuuza mwili kwa kuwa alikuwa kwenye majonzi makubwa. Hata Kamanda Dickson alipompigia simu na kumwambia kwamba alitaka kulala naye, alikataa, hakujisikia kabisa kulala na mwanaume yeyote.

Siku zikaendelea kukatika, baada ya wiki kupita hapo ndipo alipoamua kurudi katika kazi yake kama kawaida. Wakati huo ambao alirudi kazini ndipo alipopata tetesi kwamba kulikuwa na wanawake wengi waliokuwa wakipotea, tena machangudoa ambao walinunuliwa na mwanaume mmoja kisha alipoondoka nao, hawakuweza kurudi.
“Huwa anawaua,” alisema changudoa mmoja, alionekana kuwa na hofu.
“Ni nani?” aliuliza Pamela.

“Sijui! Ila hata Magreth aliuawa na huyohuyo mwanaume hata Khadija naye aliuawa na huyohuyo mwanaume,” alisema changudoa huyo maneno yaliyomtisha sana Pamela.Hakuwa na amani, moyo wake ulikuwa na hofu tele, kuanzia siku hiyo hakutaka kuchukuliwa na mwanaume yeyote yule kwenda naye kufanya mapenzi, kila mteja aliyekuja mahali hapo, ilikuwa ni lazima kufanya mapenzi makaburini au garini lakini si sehemu nyingine, hasa hotelini au nyumbani.
“Wateja wengi wanakuwa wagumu kufanya makaburini, wanaogopa,” alisema Pamela.
“Kweli?”

“Ndiyo! Jana kaja jamaa wa Kiarabu, aliniahidi hela nzuri tu ila mwisho wa siku nilipomwambia kwamba makaburini, akakata kamba, huyo akaondoka zake,” alisema Pamela.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Kwani nyie si mmesema mtu anayeua anatembelea gari nyeusi?”
“Ndiyo!”

“Sasa kama mtu akija na gari nyeupe, tunatakiwa kumuogopa kwa lipi? Sidhani kama ni sahihi,” alisema Pamela, kipindi cha wiki nzima alichokaa bila kuingiza chochote, ilimuumiza. Hakutaka kujali, alichokipanga ni kufanya popote pale, hata kama huyo mwanaume muuaji akija na kumchukua kwa lengo la kumuua, alikuwa tayari, alichokiangalia ni hela tu.
* * * *
Wanaume wengi walilizwa na machangudoa, wengi walipoteza mamilioni ya fedha na vitu vyao vya thamani kutokana na kuibiwa na machangudoa hao. Michezo michafu iliyokuwa ikichezwa na machangudoa iliwaogopesha wengi.
Machangudoa wengi walitumia dawa za usingizi kwa ajili ya kuwawekea wanaume na mwisho wa siku wanapolewa na kulala, wanawaibia kila kitu kisha kuondoka zao. Huo ndiyo mchezo uliokuwa ukiendelea kwa machangudoa wengi, hasa wale waliokuwa jijini Dar es Salaam.

Kitendo cha Dickson kumchukua changudoa yule, hakujua kama huyo alikuwa miongoni mwa machangudoa waliokuwa wakiwaliza wateja wao. Mara baada ya kuingia humo chumbani, kabla ya kuanza kufanya mapenzi, msichana yule akamwambia Dickson kwamba alitaka kwenda bafuni kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo huo.
Alipofika bafuni, akachukua kikopo kidogo kilichokuwa kwenye mfuko wake wa jinsi ambacho kilikuwa na unga fulani uliochanganywa na dawa za usingizi, akaupaka kifuani na kurudi chumbani.

Alipofika, akachojoa nguo zake, akajilaza kitandani na kumvuta Dickson. Dickson akaingia katika mikono ya changudoa huyo aliyebaki mtupu kitandani pale, kilichoendelea baada ya kupokelewa ni kushughulika na kifua cha msichana huyo.

Wala hazikupita dakika nyingi, macho yake yakaanza kuwa mazito, mbele akaanza kuona giza nene na baada ya dakika moja tu, usingizi mzito ukampata akiwa palepale kifuani.

Changudoa yule akamtoa Dickson kifuani, hakutaka kuwasha taa, alichokifanya ni kuzichukua nguo za Dickson na kuanza kuzipekua mifukoni. Humo, akakuta kiasi cha shilingi laki tano, hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuzichukua na simu yake ya gharama kubwa kisha kuondoka chumbani hapo.

Alipofika nje, alitaka kuingia ndani ya gari lakini akasita kwa kuhofia kwamba angeweza kugundulika kwa wanaume waliokuwa nje ya nyumba hiyo ya wageni. Akaelekea upande wa Kaskazini kulipokuwa na barabara ya lami, alipofika huko, akakodi bodaboda na kutokomea kurudi nyumbani kwake huku akiona kwamba amefanikiwa kufanya wizi kama ambao alizoea kuufanya kwa wateja wengine.
“Vipi Khadija?”

“Kama kawaida. Nishamliza mtu huko, pedeshee fulani alijitokeza, nimemuacha akiwa hoi,” alisema Khadija huku meno yote yakiwa nje.
“Mmmh! Hongera zako aisee…”
“Asante. Kwa hiyo bata wapi?”
“Wewe ndiye tajiri, unataka twende wapi?”
“Twende Savannah…tukale bata tu.”

“Ngoja nijiandae, usiku huuhuu tunaelekea huko, tumpitie Shamila, Ashura na Mariamu, akijipendekeza mwingine huko, kama kawaida tunamliza,” alisema Khadija huku akijiona mshindi pasipo kujua ni mtu gani aliyekuwa amemfanyia mchezo huo mchafu.
Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply