The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi 58

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa. Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Baada ya kuwa DCP, Dickson anakutana na msichana aitwaye Pamela, anatokea kuvutiwa naye, anafanya naye mapenzi kwa kumnunua Kinondoni. Kupitia changudoa huyo aliyetoka Arusha, anajikuta akianza kuwaua wanawake wengi jijini Dar es Salaam.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Biashara ilikuwa mbaya kwa Shamila, alishinda katika kijiwe chake lakini wanaume siku hiyo waliadimika, hakukuwa na mwanaume yeyote aliyemfuata mpaka mishale ya saa kumi alfajiri alipoamua kurudi nyumbani kupumzika kwa kuhesabu kwamba siku hiyo aliambulia patupu.

Wakati akiwa amefika karibu na mahali alipokuwa akiishi, bahati nzuri kwake akakutana na mwanaume, aliyeonekana kuwa na hela nyingi ambaye alihitaji huduma yake kwa muda huo uliobakia.

Shamila hakutaka kulaza damu, hiyo ilionekana kuwa bahati yake, yaani kama kutembea kilometa hamsini pasipo kuuona mwembe halafu mbele unakutana na embe dodo, alichokifanya ni kuondoka na mteja huyo na kwenda naye katika gesti iliyokuwa karibu na eneo hilo.

“Unaonekana mzuri sana, ila unaweza au ndiyo utaleta usista duu?” aliuliza Kamanda Dickson kwa sauti ya kilevi kwa mbali, hakutaka kugundulika kirahisi, yaani msichana huyo ajue kwamba alikutana na mlevi.
“Usije ukakimbia wewe tu.”
“Kweli?”
“Ndiyo!”

“Basi kama ndiyo hivyo, nitakuongeza fedha, ilimradi unifikishe ninapokwenda,” alisema Dickson huku wawili hao wakipiga hatua kuelekea kwenye gesti moja iliyokuwa karibu, kwa namna walivyokuwa wakitembea ilikuwa ni rahisi sana kusema kwamba walikuwa wapenzi wa muda mrefu, kwani walishikana kimahaba.

Walipofika katika gesti hiyo, moja kwa moja wakaelekea mapokezi ambapo dada wa hapo alionekana kufahamiana sana na Shamila, wakasalimiana kwa furaha na kuomba chumba, wakapewa chumba namba ishirini na mbili.

“Si ndiyo kile chenye wavu uliochanika na kitanda chenye kelele?”
“Ndiyo! Ila wavu tulibadilisha na hata kitanda kipo poa, tulikibadilisha, tumeweka cha chuma,” alisema mhudumu.

“Kama ni hivyo sawa, leo nipo na mpenzi mpya, sitaki presha ya kitanda cha kelele,” alisema Shamila pasipo Dickson kuzungumza chochote kile.

Kwa sababu Shamila ndiye alikuwa mwenyeji, alichokifanya ni kuchukua ufunguo wa chumba hicho na kuanza kuelekea huko. Bado walikuwa wakishikana kimahaba mpaka walipofika chumbani ambapo yeye kama mteja, Dickson akahitaji kufanya mapenzi kwenye giza kwa lengo la kutokuonekana.

“Nyie wateja wa siku hizi mna masharti kama waganga…mnapenda sana kufanya mapenzi gizani kama paka,” alisema Shamila kwa sauti iliyoashiria kutania, alipomaliza kusema hayo, akampiga Dickson kibao cha mahaba kisha kuanza kuvua nguo zake.

Uso wa Dickson ulionesha tabasamu pana lakini moyo wake ulikuwa na hasira kali, hakumpenda Shamila, alimchukia kwa kudhani kwamba huyo Hadija alimwambia kuhusu yeye hivyo kupania kumuua humohumo ndani.

Shamila alijichekesha huku akizungumza maneno ya mahaba ambayo alidhani kwamba yangeingia ndani ya moyo wa Dickson na kuubadilisha hatimaye kuwa mteja wake wa kila siku hasa baada ya kubadilishana namba za simu.
“Nataka nikupe mapenzi ya kisasa baby…” alisema Shamila.
“Yapoje hayo?”

“Wewe subiri, nitakuonesha kwa nini wananiita Shamila mkia wa taa,” alijigamba msichana huyo.

Dickson alitulia tu, alibaki akimwangalia msichana huyo ambaye alionekana kupania sana usiku wa siku hiyo pasipo kujua kwamba usiku huo ndiyo ungekuwa kwisho wa kuvuta pumzi ya hii dunia.

Baada ya kumaliza manjonjo yake yote, akamsogelea Dickson pale kitandani na kulala juu yake. Dickson akamgeuza Shamila na kumuweka chini huku akileta unafiki wa kumbusu hapa na pale hali iliyomfanya msichana huyo kufumba macho kimahaba.
“Bila shaka unaitwa Shamila…” alisema Dickson, Shamila akashtuka.
“Kumbe unanifahamu?” aliuliza Shamila huku kwa mbali akionekana kushtuka.
“Ndiyo! Hadija yupo wapi?”

“Nani? Hadija? Ndiye nani?” aliuliza Shamila huku akijidai kutokumjua Hadija kwa kuhofia kuchukuliwa mteja wake.
“Haumfahamu?”
“Wala simjui kabisa.”

“Una uhakika?”
“Ndiyo! Kwanza ndiyo nini kumtajataja mtu kwenye muda kama huu jamani baby? Mbona unataka kuniumiza?” aliuliza Shamila huku akijifanya kama kutaka kulia eti kwa kuumizwa na wivu mkali.

“Na wewe si ndiye uliyetumia naye fedha zangu alizoniibia gesti? Bila shaka mlifurahi na kula bata sana kwa hela za mwanaume msiyemjua ni nani,” alisema Dickson, maneno hayo yakaanza kumtia shaka Shamila, akataka kujitoa pale kitandani, akashindwa, mikono yake ilizuiliwa vilivyo, Dickson alikuwa juu yake.

“Wewe ni nani?” aliuliza Shamila huku akiwa na hofu tele.
“Mwenye simu na fedha! Nimekuja kwa ajili ya kuwaonesha ni jinsi gani mali za mwanaume haziendi bure,” alisema Dickson, hapohapo pasipo kuchelewa akaanza kumkaba Shamila kooni.

Msichana huyo alikukuruka huku na kule, alijitahidi kuitoa mikono ya Dickson shingoni mwake lakini hakufanikiwa, alikabwa vilivyo, macho yakaanza kubadilika na mishipa ya shingo kumsimama, Dickson hakumwacha, aliendelea kumkaba kwa lengo la kumuua.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Comments are closed.