JINSI YA KUJIEPUSHA NA MIGOGORO

KWENYE ndoa hizi ambazo wengi hutamani kuziingia kuna changamoto nyingi. Hii inatokana na jinsi ambavyo wanandoa wenyewe wanashindwa kubaini matatizo mbalimbali yanayosababisha migogoro ya mara kwa mara ambayo kimsingi ndiyo inayoharibu afya ya mapenzi.  Ndio maana kizazi cha sasa kinaangamia na ndoa nyingi hazidumu. Hii inatokana na wanandoa kukiuka misingi ya ndoa na matokeo yake wanajikuta wakiishi kwa mazoea tu lakini ndoa ilishawashinda zamani. Unakuta wanandoa kila uchwao ni ugomvi tu, hawafurahii kabisa ndoa yao.

Wanaosikia au kushuhudia hayo ambao bado hawajaingia kwenye ndoa, inawakatisha tamaa. Wanaona hakuna sababu ya kuingia kwenye ndoa kama waliopo kila siku wanagombana. Wanatukanana na wakati mwingine hawasemeshani kwa muda mrefu. Mtu na mkewe wanaishi nyumba moja lakini inapita hata miezi hawasalimiani. Lile tabasamu walilokuwa wanapeana zamani, kupokeana kwa mahaba na mabusu motomoto vyote vinayeyuka. Wanaishi kwa amri kama vile wanajeshi ndani ya ndoa.

Ndugu zangu tunapaswa kujiuliza, haya yote yanatokana na nini? Mbona mlipoishi kwenye uchumba hadi kufikia hatua ya kuamua kufunga ndoa mlikuwa hamgombani hivyo? Mlikuwa hampendani kwa dhati wakati mnaingia kwenye uhusiano? Kama mlikuwa mnapendana tatizo ni nini? Lazima ipo sababu.

Hiyo sababu ndio ambayo mnapaswa kuifahamu na kuifanyia kazi. Mjue nini kiini haswa cha ugomvi wenu na mchukue hatua za haraka. Kama kweli mlikuwa mnapendana kwa dhati tangu zamani iweje sasa muishi kama maadui? Jamani haya mambo siku zote yanatokana na mabadiliko ya tabia. Yawezekana kuna mmoja wenu amebadilika tabia hivyo ni vyema kumkumbusha kwa busara. Kwa mtu mzima ambaye anaelewa msingi wa hatua za maisha yake, unapomkumbusha kwa busara, hakika atakuelewa.

Hata kama atashindwa kukiri hapohapo lakini atakapokaa peke yake na kutafakari kwa makini, atalikiri moyoni kosa lake na kulifanyia kazi. Na wewe uliyemkosoa, usichukulie kwako kama ni ushindi bali lichukulie limepita na hakuna sababu ya kujiona mshindi. Mabadiliko ya tabia wakati mwingine yanaletwa na mafanikio. Yawezekana mlipokuwa mnaanza uhusiano mlikuwa hohehahe, mmefika mahali sasa Mungu amewafungulia milango mmeanza kupata utajiri, mambo yanabadilika.

Japo ni mtihani mkubwa kubakia na tabia zilezile za awali angali umepata mafanikio lakini kwa kusemezana, kuelimishana nyinyi kwa nyinyi mtafanikiwa kubaki kwenye mstari. Mwanaume na asiwe mzinifu kwa sababu tu amepata mafanikio, mwanamke naye asiwe na kiburi kwa sababu tu na yeye anajimudu. Hakuna kitu kizuri sana kama wanandoa kuishi kwa kuelewana. Mke amjue mumewe vizuri na mume vivyo hivyo. Mke anajua ratiba ya mumewe ya siku, anajua wajibu pia wa kukaa na mumewe kwa wakati. Mnaishi kwa upendo wa dhati.

Kama mume ametoka kazini, amekuambia kabisa kwamba amekwenda mahali kama mtoko kidogo na marafiki, mke unapaswa kumuelewa. Unapaswa kumuamini na anayeaminiwa kweli ajiheshimu. Ajue kabisa kwamba anatembea na roho ya mtu. Asifanye michezo isiyofaa. Mume naye ajue wajibu wake kwa mkewe. Sio kila siku kurudi saa tisa usiku, ukiulizwa upo na marafiki.

Tenga muda wa kukutana na mkeo kadiri uwezavyo. Onesha unampenda na unamthamini. Mke naye amtii mumewe. Aoneshe thamani ya kupendwa na mumewe, amjali kuliko kitu kingine chochote. Kila mmoja wenu aguswe na thamani ya ndoa yenu. Kila mmoja athamini furaha ya penzi lenu maana inapokuwepo, mnajenga familia bora. Mtapata maendeleo pale mnapokuwa mnaelewana hivyo kila mmoja wenu ahakikishe kadiri awezavyo anatengeneza furaha ya mwenzake pale inapoonekana kuterereka.

Mwenzako anapokuwa kwenye majonzi, usikubali kumuacha peke yake. Huzunika naye, mfariji na umuondoe kwenye lindi la mawazo. Hilo kila mmoja alifanye, mkiishi hivyo miaka yote ndoa mtaiona tamu. Tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifuata Facebook na Instagram natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment