The House of Favourite Newspapers

Jinsi ya kukabiliana na maambukizi katika mirija ya uzazi (salpingitis)

Salpingitis ni maambukizi yanayoathiri mirija ya uzazi ya mwanamke. Mirija ya uzazi au fallopian tubes ipo miwili upande wa chini wa tumbo la mwanamke, kulia na kushoto. Kazi ya mirija hii ni kupitisha mayai na kutungisha mimba.

 

Maambukizi haya hutokana na maambukizi ya jumla katika viungo vya uzazi vya mwanamke ‘PID’. Tatizo hili la PID hujumuisha maambukizi katika tabaka la ndani la kizazi yaani endometritis, maambukizi katika vifuko vya mayai yaani oophoritis na mengineyo kama myometritis na parametritis. Maambukizi haya yanaweza kuwa makali ‘acute’ au sugu ‘chronic’.

 

DALILI ZA UGONJWA

Dalili hujitokeza zaidi baada ya mwanamke kumaliza damu ya hedhi ambayo ni kama vile kutokwa na uchafu ukeni wenye rangi isiyo ya kawaida na harufu mbaya, maumivu makali wakati wa upevushaji mayai ‘ovulation pains’, maumivu makali wakati wa tendo la ndoa, maumivu kabla ya kuingia kwenye hedhi na huisha baada ya kupata damu ya hedhi, maumivu ya mara kwa mara ya tumbo chini ya kitovu, maumivu ya kiuno, kujihisi homa na uchovu mara kwa mara, kichefuchefu, kutapika na kuhisi tumbo kujaa gesi.

 

JINSI TATI ZO LINAVYOTOKEA

Kawaida maambukizi huanzia ukeni na husambaa kupitia mlango wa kizazi hadi ndani ya kizazi na mirija, maambukizi hupitia katika mirija ya ‘lymph’ na kuathiri mirija yote miwili. Kwa hiyo mwanamke mwenye tatizo la kutokwa na uchafu mara kwa mara ukeni awe makini na tiba kwani asipotibiwa

vizuri na tatizo kujirudiarudia hupatwa na tatizo hili ambalo athari zake ni ugumba.

 

Aina ya bacteria wanaosababisha maambukizi haya ni ‘neisseria gonorrhoea’ ambao husababisha ugonjwa wa kisonono, aina nyingine ni chlamydia trachomatis, mycoplasma, staphylococcus na streptococcus.

 

Hata hivyo, tatizo hili la maambukizi ya mirija husababishwa na aina nyingi moja. Bakteria hawa pia wapo wanaotegemea hewa ya oksijeni pamoja na wale wanaotegemea hewa ya kabondayoksaidi.

 

WANAWAKE WALIO HATA RINI

Wanawake wote wanaweza kupatwa na ugonjwa huu hasa ikitegemewa kwamba wakati wa hedhi mlango wa kizazi hufunguka hivyo bacteria husafiri na kufikia mbali, lakini pia mwanamke anaweza kuathirika na ugonjwa huu wakati wa kusafisha kizazi, kutoa mimba na hata wakati wa vipimo kama uangalizi makini hautakuwepo.

 

Vyanzo vingine vya maambukizi ni wakati wa hedhi kama tulivyoona, wakati wa ovulation au upevushaji mayai na uwepo wa magonjwa ya zinaa. Hivyo inashauriwa mwanamke awe msafi daima ukeni na kutibu kila tatizo linalojitokeza huko. Wakati wa tendo la kujamiiana pia kunaweza kusababisha bakteria waliopo ukeni kufika ndani ya kizazi.

 

UCHUNGUZI

Vipimo mbalimbali hufanyika kuangalia chanzo cha tatizo na ukubwa wake. Vipimo vya mkojo, speculum examination, high vaginal swab, ultra-sound na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa vifanyike. Uchunguzi hufanyika katika kliniki za magonjwa ya kina mama kwenye Hospitali za Mikoa na Rufaa.

 

MADHARA YA UGONJWA

Umri ambao mwanamke hupatwa na ugonjwa huu ni miaka 15 hadi 44. Madhara ya ugonjwa huu ni makubwa pamoja na ugonjwa kusambaa katika viungo vingine kama vifuko vya mayai na kizazi kwa jumla. Mwanamke anaweza kupata mimba nje ya kizazi yaani ectopic pregnancy, kuziba mirija yote na ugumba. Anaweza kumuambukiza mwanaume wake, akawa analalamika maumivu ya kukojoa, vifuko vya mayai vinaweza kutungisha usaha.

 

TIBA NA USHAURI

Matibabu Mazuri hutegemea na uchunguzi mzuri na utaalam sahihi. Ili kuepuka kupata madhara, wahi hospitalini mara uhisipo dalili ambazo tumekwishazielezea.

 

Waone madaktari bingwa wa kina mama katika Hospitali za Mikoa na katika kliniki za madaktari bingwa wa magonjwa ya kina mama ukafanyiwe baadhi ya vipimo kama tulivyokwishaelezea.

Comments are closed.