The House of Favourite Newspapers

Jinsi Ya Kumfanya Mwenza Wako Afurahie Penzi Lenu

NI IJUMAA nyingine ambayo Mwenyezi Mungu ametukirimia na mimi ninawakaribisha hapa jamvini, mahali ambapo tunajadili mapenzi na maisha kwa jumla. Watu wengi wamekuwa wakiniuliza ni nini siri na kuwa na penzi la kudumu lenye furaha hasa kwa watu ambao wapo bize na shughuli za kimaisha kama kazi za kuajiriwa au ujasiriamali?

Mara nyingi huwa ninawajibu kwamba ni kuwa kwenye penzi ambalo hutegemei kupokea tu, bali na kutoa pia. Yaani uwe chanzo cha furaha ya mwenza wako na siyo akuone kikwazo cha kutokuwa na furaha maishani mwako.

Kumbuka kila mtu, awe mwanamke au mwanaume ana mahitaji fulanifulani ambayo akiyapata, basi anakuwa na furaha na roho safi. Kwa hiyo cha muhimu ni kujifunza mahitaji ya mwenza wako. Kama ukiyakidhi kwa usahihi, furaha kwake na kwako kamwe haiwezi kukosekana. Yafuatayo ni mambo ambayo ukiyatimiza yatamfanya mwenza wako kuwa na furaha au kufurahia penzi lenu;

MFANYE NAMBA MOJA

Jua kwamba mpenzi wako, hasa wa kike hufurahi sana kuona yeye ndiye kipaumbele kwa mwanaume wake. Anataka awe wa muhimu kuliko mwingine na hata kazi au biashara zako. Hataki kulinganishwa na mtu mwingine humu duniani.

ANAHITAJI UKARIBU

Ni lazima ujue kwamba mpenzi wako anapokuwa amechoka na mihangaiko ya kimaisha hasa kipindi hiki ambacho usawa umekaba, anahitaji ukaribu na kufarijiwa. Mtu pekee anayeamini ni faraja kwake ni mwenza wake. Kunapokuwa na hali kama hiyo, wewe ndiye unakuwa baba na mama wa kumtia moyo na kumfanyia mambo ambayo yatamsahaulisha changamoto za kimaisha alizokutana nazo.

ANAHITAJI KUSIFIWA

Inapaswa kuwa tabia yako siku zote kwa mwenza wako. Msifie na kumpongeza pale anapofanya jambo au kazi fulani. Ukishamaliza kumsifia ndipo umkosoe kwa lugha ambayo haitamuondolea furaha. Kwa kufanya hivyo mwenza wako atajiona wa thamani na sehemu ya maisha yako.

ANAHITAJI ULINZI

Ulinzi siyo wa kumlinda na silaha za kawaida au za moto wakati amelala badala yake ni kuwa mtetezi wake pale anapohisi kuonewa. Anachotakiwa kuhakikishiwa ni kwamba upo kwa ajili yake na hapo atakuwa na furaha.

SHIRIKI NAYE

Shirikiana maisha na mwenza wako. Anahitaji umuunganishe kwenye maisha yako kwa njia maalum hivyo mtengenezee mazingira ya kukushirikisha kwanza jambo lake kabla ya mtu mwingine. ‘Usimfungie vioo’ kwani utamuumiza mwenza wako.

USIMKWAZE

Epuka sana kumkwanza mwenza wako kwa kumfanyia matendo ambayo atahisi anadhalilishwa. Badala ya kumdhalilisha, wewe mtie moyo. Ukosoaji wako kwake usilenge kumuondolea utu au ubinadamu. Usiwe mkali kwake kwani utamjengea kutojiamini mbele yako. Kwa kufanya hivyo utamfanya afurahie penzi lenu.

MJENGEE HESHIMA

Mtu ambaye amekuchagua wewe kati ya mamilioni ya wengine, mjengee heshima mbele ya jamii. Unapomzungumzia kwa watu, mzungumzie chanya au vizuri na siyo kumponda kuwa hana lolote kwa sababu utamjengea picha mbaya kwa watu.

MUUNGE MKONO

Mwenza wako anapokuja na wazo la kimaendeleo, usiwe mwepesi wa kumpinga au kumkatisha tamaa, badala yake muunge mkono. Mwanamke aliyeko kwenye presha ya kutaka kuchangia pato la familia na kuwalea wanaye vizuri hapaswi kukatishwa tamaa.

Tukumbuke furaha ya mwenza hainunuliwi dukani hivyo mfanye mwenza wako awe na furaha wakati unaofaa kuwa na furaha.Kwa maoni au ushauri, nicheki kwenye namba hapo juu.

Comments are closed.