JINSI YA KUWAEPUKA MATAPELI WA MAPENZI

JUMATATU nyingine mpenzi msomaji wangu tunakutana kwenye eneo letu zuri la kupeana darasa la masuala ya uhusiano. Natumai umzima wa afya kama nilivyo mimi, kama afya imeleta mushkeli kidogo basi nikupe pole na Mungu akupe nguvu, urudi katika hali yako ya kawaida.  Moja kwa moja nikienda kwenye somo la leo kama linavyo­jieleza hapo juu, lahusu matapeli wa mapenzi. Dunia ya sasa kila mmoja wetu ni sha­hidi wa hili, matapeli au walaghai wa mapenzi wamekuwa ni wengi kuliko wale wenye mapenzi ya dhati.

Ni nadra sana kumpa­ta mtu sahihi kwenye ulimwengu huu uliojaa matapeli wa kila namna. Kuna ambao ni hodari wa kuwa­tumia wanawake, kuna wengine pia ni hodari wa kuwa­tumia wanaume. Bahati mbaya sana matapeli hawa wana mbinu za hatari.

Ukihisi umempatia na kumtambua katika mbinu hii, mwenzako kumbe ana mbinu nyingine. Mtu anakuja utadhani kweli ni muoaji kumbe wapi, tapeli tu. Anakuhadaa kwa maneno matamu, anakuambia anahitaji kuwa na wewe kwa mai­sha yake lakini baada ya muda anakuchenga. Anageuka kama kinyonga baada tu ya kupata kile anachoki­taka. Wakati mwingine anakuwa anaongozwa na tamaa tu. Akishap­ata anachokitaka basi hakuna tena mapenzi. Anahamia kwa mtu mwingine na kukuacha solemba.

Hivyo basi marafiki zangu, tunapaswa kuwa makini sana katika suala zima la uhusiano. Unapaswa kuwa makini kabla ya kuanzisha uhusiano na mtu. Unapaswa kumjua kiundani mhusika kabla ya kuzama penzini.

Sio unakutana leo tu na mtu anakulaghai, unamkubalia kesho tayari ameshakuwa mpenzi wako. Hujui anatokea wapi, ndugu zake ni kina nani au ana tabia gani wewe unabeba tu. Hii ni hatari sana, uhusiano mzuri ndugu zangu ni ule wa watu wawili ambao wamesomana kwa muda kidogo kama si muda mrefu.

Unapomjua mtu kwa undani angalau inakupa picha ya kule uendako. Unaweza kumfanyia tathimini na kujua kama anafaa kuwa mwenzi wako au la. Acha papara za kuwa mp­weke, wakati mwingine ni bora kuishi peke yako kuliko kuishi na mtu ambaye atakuwa ni pasua kichwa.

Mimi na wewe ni mashahidi juu ya matukio mabaya ya wapendanao yanayo­tokea katika dunia ya sasa. Watu wanaua­na, ukichunguza kwa makini wanaofanya matukio haya huwa na historia ya ukorofi au hata ujambazi.

Unaolewa au kuoa jambazi unategemea nini kwenye maisha yako? Jambo dogo tu ukimkosea mtu wa aina hiyo ni rahisi kuk­uua kwa risasi kama si kukukata mapanga. Mtu anakuwa hana ubinadamu, kukuua ni dakika tu. Wa nini mtu wa aina hiyo? Jifunze kukaa kwenye mazin­gira salama ya kuwa na watu wazuri.

Mathalan waweza kuwa karibu na watu ambao wana imani na hofu katika Mungu. Watu wa namna hiyo wapo katika maeneo fulanifulani, yatafute. Nako ukiwa pia si kwa kukurupuka. Ni vizuri pia ukamsoma mtu aliye karibu nawe kabla ya kuanzisha uhusiano.

Angalau umjue kidogo tabia, historia yake na hata watu wanaomzunguka. Mfanye awe rafiki kwa muda fulani kabla ya kuwa mpenzi wako, mchumba na hata mumeo. Tukutane wiki ijayo, unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. In­stagram na Facebook natumia Erick Evar­ist, Twitter natumia ENangale.

 


Loading...

Toa comment