The House of Favourite Newspapers

MWANAMKE ANAVYOWEZA KUPOTEZA UWEZO WA KUSHIKA MIMBA -2

INAENDELEA toka wiki iliyopita Vyanzo vingine vya matatizo yote haya ni kuharibika kwa mimba, iwe kwa bahati mbaya au kwa kuitoa kwa makusudi. Mirija kama imethibitika imeziba, basi ni vyema umuone daktari bingwa wa kina mama ili aangalie jinsi ya kukusaidia.  

 

Vifuko vya mayai pia ni sehemu nyingine muhimu sana katika mfumo wa viungo vya uzazi vya mwanamke. Vifuko vya mayai au ovaries, zipo mbili kulia na kushoto. Kazi ya ovari ni kupevusha mayai na kuzalisha vichocheo au homoni za progesterone na estrogen.

 

Homoni hizi ni muhimu katika mfumo wa uzazi wa mwanamke. Matatizo katika vifuko vya mayai ni kushindwa kuzalisha vichocheo hivyo kwa kiwango chake, uvimbe au ovarian cyst, kutokwa na vivimbe vidogovidogo sehemu hiyo ya ovari viitwavyo polycystic.

 

Dalili za matatizo katika vifuko vya mayai ni kuvurugika mzunguko wa hedhi, kutokupata hedhi pasipokuwa na ujauzito, maumivu upande mmoja chini ya tumbo. Tiba yake inaweza kuwa dawa au upasuaji endapo uvimbe huu ni mkubwa sana au umejinyonga.

MATATIZO YA MFUMO WA HOMONI

Hii ni sehemu nyingine kubwa ya pili inayosababisha mwanamke asifanikiwe kupata ujauzito. Mwanamke anaweza kuishi muda mrefu na mumewe bila mafanikio, mumewe akawa vizuri tu na yeye akajihisi hana tatizo lolote, lakini mimba haipatikani.

 

Matatizo ya mfumo wa homoni huambatana na baadhi ya dalili zifuatazo. Kupata siku za hedhi bila mpangilio, kufunga kupata hedhi kwa muda mrefu, kutopata ute wa uzazi, kutohisi hamu au raha wakati wa tendo la ndoa, maziwa kutoka wakati huna mimba au hunyonyeshi na kujihisi mjamzito wakati huna mimba.

 

Chanzo cha matatizo haya yote ni mengi na zaidi huwa ya muda mrefu. Ni vizuri umuone daktari bingwa wa matatizo ya uzazi au magonjwa ya kina mama katika hospitali ya mkoa.

Comments are closed.