The House of Favourite Newspapers

JK Ahutubia Viongozi Wa Chama Cha Vyuo Vya Elimu Ya Juu Uganda

0
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea zawadi ya picha yake ya kuchora baada ya kuhutubia chama cha viongozi wa zamani na wa sasa wa Serikali za Vyuo vya Elimu ya juu nchini Uganda katika mkutano wao ulioandaliwa katika Chuo Kikuu cha Makerere jijini Kampala jana Jumatatu.

Mkutano huo, uliojulikana kama ‘Guild Leaders Summit’ uliwaleta pamoja marais wa zamani na wa sasa wa chama hicho, wazungumzaji maalmu na viongozi wengine wa wanafunzi kutoka vyuo vikuu na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kote nchini humo.

Tukio hili lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Makerere linalenga kukuza ujuzi wa uongozi na kuhimiza mazungumzo kati ya viongozi wore wa wanafunzi nchini humo.


Dkt. Kikwete, anayesifika kwa utetezi wake wa maendeleo ya elimu na uongozi wakati wa uongozi wake, katika hotuba yake kama mgeni rasmi ameangazia changamoto na fursa zilizopo katika uongozi kwa wanafunzi wa vyuo katika zama za leo.

Alisisimua viongozi hao na wanafunzi waliofurika ukumbini hapo kwa kuwasimulia historia yake yeye akiwa kiongozi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es salaam, hadi kuonekana na uongozi wa juu wa nchi na kuaminika kupewa dhamana mbalimbali za uongozi.

 Dkt. Kikwete akiwa na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda alipomtembelea Ikulu ya Entebbe baada ya kumalizika kwa mkutano wa Makerere hiyo jana Jumatatu

Dkt Kikwete aliusifia mkutano huo na kuwataka viongozi hao kujumisha viongozi wenzao wa vyuo vikuu vya Afrka Mashariki katika mazungimzo kama hayo ili kuwa na umoja na kushirikiana katika mijadala inayojenga hoja za kimaendeleo kimasomo na katika mustakabali wa ustawi wa mataifa yao.

Alizungumzia pia umuhimu wa kutenganisha masomo na mambo ya siasa vyuoni, akisisitiza kwamba mbali na kukwaza ushiriki wa wanafunzi wa kutoka nje ya nchi, pia hilo linaweza kusababisha sintofahamu katika mustakabali wa masomo.

Mkutano huo ulitumika kama jukwaa la viongozi wa wanafunzi kubadilishana uzoefu, kujadili masuala ya sera, na kuchochea mikakati madhubuti ya uongozi. Uwepo wa Dkt Kikwete katika mkutanoni hapo kumehamasisha pakubwa wahudhuriaji na kuibua mijadala ya kusisimua ya jinsi viongozi wa wanafunzi wanaweza kuchangia vyema kwa jamii zao na sekta pana ya elimu.

Baada ya mkutano huo Dkt Kikwete alikwenda kumsalimia Rais Yoweri Kaguta Museveni katika Ikulu ya Entebbe.

Rais Museveni akimkaribisha kiongozi huyo mstaafu wa Tanzania nchini humo, alimueleza Dkt. Kikwete kuwa kama viongozi hawana budi kutatua tatizo la soko ili kuhakikisha ustawi wa watu wa Afrika Mashariki.

Rais Museveni alisisitiza pia usalama wa kimkakati kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akisema hii itasaidia mataifa kulinda maslahi yao.

Kwa upande wake, Dkt. Kikwete amewasilisha salamu za Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa Rais Museveni, na kumshukuru kwa mapokezi mazuri.

Leave A Reply