The House of Favourite Newspapers

Jokate Afunga Mwaka 2019 Kibabe

0

 

AMEFUNGA mwaka kibabe! Ndivyo unavyoweza kumtafsiri Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe (DC), Jokate Urban Mwegelo ambaye licha ya kuiongoza wilaya hiyo kwa miezi 17, ameifanyia mambo makubwa yaliyoirudisha hadhi ya Kisarawe ambayo ni moja ya wilaya kongwe nchini.

 

Jokate ambaye aliteuliwa Julai 28, mwaka jana, amekuwa mmoja wa wakuu wa wilaya waliofanikiwa kubuni miradi na kutatua changamoto za wananchi wa eneo wanaloongoza hadi kulazimu mbunge wa eneo hilo, Suleiman Jafo kumsifia hadharani.

 

Licha ya kwamba ni nadra kwa mbunge wa eneo husika kumsifia mkuu wake wa wilaya kwa kuwa wabunge wengi huhofia kupoteza majimbo yao, hali ni tofauti kwani Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jafo ambaye ni Mbunge wa Kisarawe.

 

“Leo Jokate ni mpya zaidi, haya yote ni matunda ya kufanya wema uliopitiliza, ukifanya wema Mungu anakupa nuru usoni mwako, hata ukipaka mafuta ya nazi, watu wanaona unang’aa tu,” alisema Jafo na kumuomba Rais Dk John Pombe Magufuli amuone zaidi Jokate.

 

MIRADI ALIYOIBUNI YATIKISA

Mojawapo ya miradi aliyoibuni na kufanikiwa kuleta mabadiliko Kisarawe, ni pamoja na Tokomeza Zero, Tokomeza Jembe la Mkono, Ukatili wa Kijinsia Kisarawe Sasa Basi na miradi mingine ambayo imesaidia kurudisha furaha kwa wananchi wa eneo hilo.

 

Tokomeza Zero Kisarawe, ni miongoni mwa miradi aliyobuni mkuu huyo wa wilaya na kufanikiwa kuleta mabadiliko ikiwemo katika shule ya sekondari kidato cha tano na sita ya Maneromango, iliyoanzishwa mwaka 2017. Katika matokeo ya shule hiyo mwaka huu ilitoa zero moja na daraja la kwanza 38 katika wahitimu wa kidato cha sita kwa mara ya kwanza shuleni hapo.

 

‘Ukatili wa Kijinsia Kisarawe Sasa Basi’ ni kampeni nyingine aliyoianzisha mwaka huu wilayani humo na kufanikiwa kupunguza matukio ya ukatili ikiwa ubakaji.

 

“Mwaka huu kupitia mahakama yetu ya Wilaya ya Kisarawe, tumehukumu miaka 30 jela kila mmoja, watu nane waliobaka pia miaka 30 jela kwa watu wawili waliowapa mimba mabinti. Nipongeze mahakama kitengo cha ustawi wa jamii, jeshi la polisi, ofisa elimu wa msingi na sekondari,” aliandika Jokate kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Twitter.

 

Jokate alisema kwa kupitia dawati la jinsia na watoto Kisarawe kwa uratibu wa OCD wamezindua Mpango Mkakati wa Kudhibiti Ukatili Wa Kijinsia Wilaya ya Kisarawe 2020.

 

“Itajumuisha kutoa elimu, kushirikisha jamii katika kusimamia hili na kuhamamisha utoaji wa taarifa kwa wakati . Ukatili wa Kijinsia Kisarawe Basi!!!! #KisaraweMpya #TanzaniaMpya,” aliandika Jokate.

‘Tokomeza Jembe la Mkono’ ni kampeni nyingine aliyoianzisha mwaka huu, mkuu huyo wa wilaya ambayo imeanza kuonesha matunda kutokana na juhudi zake.

 

Itakumbukwa kuwa, Novemba, mwaka huu, Serikali ya Wilaya ilitenga ekari 533 kwa vijana kwa ajili ya kufanya ufugaji, kilimo cha kisasa na teknolojia, kilimo kipana na endelevu cha mpunga, ufuta, korosho na mihogo.

 

“Na kwa kushirikiana na wadau wa kilimo na uwekezaji, tunakusudia ndani ya miaka miwili kutengeneza ajira kati ya 500 mpaka 1000 na kuzalisha kampuni za kilimo za vijana kati ya 50 mpaka 100 zenye thamani ya chini ya shilingi bilioni mbili katika Wilaya ya Kisarawe,” alisema Jokate.

 

Pamoja na miradi hiyo, pia mkuu huyo wa wilaya amefanikiwa kutatua kero ya maji kwa wakazi wa Kisarawe, kuboresha uwanja wa mpira wa miguu na kuiwezesha timu ya Ruvu Shooting inayoshiriki Ligi Kuu Bara kupata hamasa ya kushinda mechi zake.

 

“Kupitia hili naendelea kujifunza nguvu ya kinywa-maneno tunayonena na uthubutu-kujiamini. Wanasema penye nia pana njia.

Hongera JKT Ruvu Shooting na kila la kheri,” aliandika Jokate baada ya kukamilisha ukarabati wa uwanja huo.

 

…ABEBA TUZO

Kutokana na juhudi hizo, baadhi ya taasisi zimempatia tuzo mlimbwende huyo ambaye aliwahi kushiriki mashindano ya Miss Tanzania 2006.

Moja ya taasisi hizo ni Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Women in Management Tanzania ambayo imempatia tuzo hivi karibuni kama mmoja wa wanawake 50 waliofanya vizuri mwaka huu.

“Asante @tgnp_mtandao kwa tuzo hii ya heshima na hongera kwa halmashauri yetu ya Wilaya ya Kisarawe na kwa wadau wote tunaoshirikiana nao,” aliandika Jokate.

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply