The House of Favourite Newspapers

Wamevipiga Vita na Mwendo Wameumaliza 2019

0

KIFO ni haki yetu licha ya kwamba hakizoeleki, kisikie tu kwa mwenzako, siku kikifika kwako hupati picha kutokana na kwamba maumivu ya kufiwa na mtu wako wa karibu au ndugu yako hayapimiki kwa mizani wala kipimo chochote.

 

Ukiona wewe bado ni mzima, unapumua, mshukuru Mungu kwa kuwa ni kwa neema yake tu na siyo kwamba sisi tumetenda mema na wale waliotangulia mbele ya haki walitenda mabaya, bali ni kwa neema ya Mungu tunaishi.

 

Wakati mwaka 2019 ukielekea ukingoni, kuna mastaa ambao tulikuwa nao wakati tunauanza na walipigana kwa ajili ya maisha yao kwa kufanya kazi zao za sanaa na nyinginezo, lakini leo hawapo. Wamevipiga vita vilivyo vizuri na mwendo wameumaliza;

 

GODZILLA

Jina lake halisi ni Golden Mbunda. Alikuwa mwanamuziki wa Hip Hop Bongo ambaye enzi za uhai wake alikuwa akifanya vizuri kwenye sanaa ya muziki hasa kwenye eneo la kuchana.

 

Msanii huyu alifariki dunia ghafla akiwa nyumbani kwao Salasala jijini Dar, Februari, mwaka huu na kuacha simanzi na pengo kwa sanaa ya muziki.

 

Marehemu Godzilla aliwahi kutamba na Ngoma kama X, Salasala, King Zilla na nyingine nyingi ambazo bado hazifi. Licha ya kutangulia mbele ya haki, muziki wako bado unaishi.

 

ANTI FIFI

Tumaini Bigilimana ‘Anti Fifi’ alikuwa msanii mkongwe wa filamu za Kibongo ambaye pia alikuwa ni diwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma kupitia Chama cha ACT-Wazalendo. Alifariki dunia Juni, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mfupi.

 

Kifo cha mama huyu ambaye ameigiza filamu mbalimbali kama Fake Smile, Daddy, Cross My Sin, Sinior Bachelor na nyingine nyingi kilishtua wengi kwani hakuna aliyekuwa ana taarifa za kwamba anaumwa, bali walisikia tu habari ya msiba ambapo baada ya hapo taarifa zilieleza kuwa aliugua kwa siku chache na kufariki dunia.

 

Mwigizaji huyu alikuwa ni mpambanaji kwani mbali na kuwa diwani na kuigiza filamu, pia alikuwa mtunzi au mwandishi mzuri wa filamu. Hivyo wasanii mbalimbali wa tasnia hiyo walikuwa wakimtumia.

 

MAMA ABDUL

Mtaani ukilitaja jina hili ni maarufu mno. Marehemu Mama Abdul jina alilopewa na wazazi wake ni Salome Nonge ambaye alifariki dunia Januari, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu.

 

Mama Abdul alikuwa ni mwigizaji na Mtangazaji wa Radio Times FM ambapo ameshiriki katika filamu kama vile Kan’tangaze na michezo mbalimbali tangu enzi za Kaole Sanaa Group.

 

SETH BOSCO

Ni mdogo wa aliyekuwa msanii maarufu wa filamu, marehemu Steven Kanumba ambaye alifariki dunia hivi karibuni, Desemba, mwaka huu baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kupooza kwa muda mrefu.

Seth alikuwa mpiganaji tangu enzi za uhai wa kaka yake, lakini kifo kilikatisha ndoto zake alizokuwa nazo kuhusiana na sanaa hiyo.

Makala: Gladness Mallya

Leave A Reply