The House of Favourite Newspapers

Jokate Azungumza, Wenyeviti, Watendaji Kata Na Wilaya Ya Korogwe Wakizawadiwa Mitungi Na Majiko Yake 500 Na Oryx

0
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo akizungumza kwenye hafla hiyo.

Kampuni ya  Oryx Gas Tanzania Limited imegawa mitungi na majiko yake 500 kwa Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji na Kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga huku ikieleza lengo la kugawa mitungi hiyo ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa mitungi hiyo mbele ya viongozi hao wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo,  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Araman Benoite amesema wamekuwa wakiendelea kufanya uwekezaji mkubwa nchini Tanzania kwa makundi mbalimbali ya wananchi ili kuunga mkono juhudi za serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Araman Bonoite (wa pili kulia) wakimkabishi mtungi wa gesi ya Oryx pamoja na jiko lake Mjumbe wa kikundi cha Lutind Tea Herbs and Spices Mariam Angeline Isidor .Wengine katika picha hiyo ni viongozi wa ngazi mbalimbali katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.(Picha na mpiga picha wetu).

“Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya gesi safi ya LPG ambayo ni suluhisho la kuondoa matumizi ya kuni na mkaa, hivyo basi kuboresha afya ya jamii na kulinda mazingira,sambamba na ahadi ya Rais kutoa nafasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.”

Aidha amesema  katika muendelezo uleule wa juhudi za kuhamasisha matumizi ya nshati safi ya kupikia kwa wananchi wote,kampuni ya Oryx  Gas imeamua kusimama na wananchi wa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga  kupitia kwa viongozi wao kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wote.

Meneja Mauzo Ukanda wa Dar es Salaam na Pwani Shaban Mohamed kutoka Kampuni ya Oryx Gas Tanzania akielezea namna ya kutumia mtungi wa gesi ya Oryx.

“Juhudi hizi ni pamoja na kusaidia kuwabadilisha viongozi wa wananchi kuachana na kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati ya gesi za kupikia (LPG).Hivyo tumekabidhi mitunge ya gesi na majiko 500, ” amesema na kuongeza ugawaji huo umekwenda sambamba na kutoa mafunzo ya usalama wa matumizi ya mitungi hiyo.

Benoite amesema wanaamini viongozi wanawakilisha wananchi na kiongozi anapaswa kuongoza kwa mifano na wanaushawishi mkubwa kwa wananchi wanaowaongoza hivyo Oryx imeona itoe mitungi ili wao wenyewe wakianza kutumia watape mamlaka ya kuwaambia wananchi umuhimu wa mabadiliko.

Pia amesema Oryx Gas Tanzania Ltd  inaendelea kuwekeza katika uagizaji, uhifadhi, ujazaji wa gesi kwenye mitungi na usambazaji wa LPG  Tanzania nzima, pamoja na Visiwa vyake. Oryx Gas Tanzania  huwekeza kila mwaka mamilioni kadhaa ya dola kwenye mitungi mipya inayoingizwa sokoni kila siku.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amesema ugawaji wa mitungi hiyo ya gesi inakwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye alishazindua kampeni ya kutumia nishati mbadala kwa lengo la kulinda mazingira.

Amesema katika wilaya hiyo wameamua kugawa mitungi hiyo ya gesi kwa viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya wilaya mpaka ngazi ya msingi wakiwemo wenyeviti wa vijiji na watendaji katika kata zote huku akifafanua lengo kubwa ni kutoa ujumbe kwamba miti mingi inayokatwa iko vijijini na huko ndiko ambako viongozi hao wapo.

”Wenyeviti na watendaji wa vijiji tumewaona na tumetambua uwepo wenu, kama viongozi kwenye maeneo yeenu kuna watu wanawaakangalia. Leo hii mwenyekiti wa kijiji na mtendaji wake wakiamua kutumia nishati mbadala na wanakijiji watahamasika.

“Kwasababu wanaangalia viongozi wao wanawajua, wamewachagua wenyewe na wana uwezo wa kuwashawishi kuacha kutumia miti vibaya wakaanza sasa kuunga mkono jitihada hizi za kutumia nishati mbadala ili tuokoe kizazi hiki na kinachokuja.”

Aidha ameeleza kutokana na uharibifu wa mazingira Serkali ilitoa maelekezo mahususi wananchi kupandeni miti na kutunza mazingira , vyanzo vya maji ili kupata maji lakini kilimo kibaki salama kuwe na chakula cha kutosha.

“Sasa maamuzi ni ya kwetu sisi, na ndio kwenye haya  nikasema lazima sisi viongozi katika ngazi zote ndani ya wilaya ya Korogwe tukubaliane tuachane na matumizi ya mkaa na kuni.Tukiamua kubadilika tutachochea wenzetu kubadilika.

“Nikasema sipendi kushurutisha watu bila kuwezesha , majiko ya gesi ndio haya kazi kwenu , lakini hii ni awamu ya awali tumeshauriana na viongozi wenzangu hivyo tutaenda awamu kwa awamu.Nia yangu ni kuwa na Korogwe inayosomeka kama wilaya kinara kwenye matumizi ya nishati safi,”amesema Jocate.

Ameongeza suala la nishati safi ya kupikia ni la wote hivyo watalibeba kwa mikono miwili ili kunusu misitu na mazingira sambamba na kwenda na kauli ya Rais Dk.Samia ya kuigeuza Tanzania salama na yenye kusifika katika utunzaji mazingira na kutumia nishati safi ya kupikia.

“Huo ndio mtazamo wetu na katika kufanikisha tumeungwa mkono na wenzetu wa Oryx ambao wanasifika kwa kugawa mitungi lakini mimi ningependa wasifike kwa watu unaowagawia mitungi waendelee kutumia hii mitungi.Watu lazima waendelee kutumia gesi na hii  iwe endelevu,”amefafanua.

Leave A Reply