The House of Favourite Newspapers

JOKATE KAFUNGUA MLANGO, KING MAJUTO KAACHA SOMO

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo

MIONGONI mwa wadau wanaoifahamu sanaa ya Bongo nje ndani ni mwanamama Asha Baraka ‘Iron Lady’, ambaye ni Mkurugenzi wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’. Asha amekuwa kwenye sanaa kwa zaidi ya miaka ishirini na wanamuziki wengi wamepitia mikononi mwake hasa wa Muziki wa Dansi.

 

Roho zilizota-ngulia mbele za haki za wana-muziki wa Dansi maarufu nchini na wane-nguaji wakiwemo Abuu Semhando, Ismail Kizunga, MCD, Banza Stone, Joseph Watuguru, Halima White, Happy Choki, Diana Aston Villa, Pendo Bouda, Mwantumu MCD na Amigo Rasi, zimepitia mikononi mwake.

 

Hata hivyo pamoja na kuwa na mchango mkubwa kwenye Dansi, ana mchango pia kwenye Bongo Fleva kwani amewasaidia wanamuziki wengi wakubwa wakiwemo kina Diamond Platnumz, MwanaFA na wengine wengi kupata shoo za nje, ndani ya Bongo na kufika mbali kwenye muziki.

 

Hatuwezi kuacha kuzungumzia mchango wake kwenye filamu. Kamsaidia sana marehemu Steven Kanumba, kina Vincent Kigosi ‘Ray’, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper katika lokesheni za muvi zao pamoja na mambo mengine kwenye tasnia yao.

 

Asha ni mwanasiasa pia. Itikadi zake amezielekezea kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) na ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho. Hivi karibuni, Risasi Vibes, imekutana na mwanamama huyu kwenye harakati za kiburudani na alikuwa na mengi ya kuzungumza kuhusu Muziki wa Dansi na mengine mengi. Huyu hapa;

 

Risasi: Wamiliki wengi wa bendi wanaachana na bendi na kufanya mambo mengine kutokana na muziki huo kuyumba, nini siri ya wewe kuendelea kuwa kwenye gemu hilo?

Asha: Kwanza niseme kwamba dansi kwa sasa imerudi kama zamani. Ni kweli ilikuwa imeyumba lakini hali imebadilika, kwa sasa shoo zimeanza kujaza tena kama ilivyokuwa zamani. Kuhusu mimi kuendelea kukomaa na bendi ni kwamba ni kitu ninachokipenda. Kwa hiyo nipo tayari kupitia hali tofauti pamoja na bendi yangu lakini si kuachana nayo.

Risasi: Unafikiri tatizo lilikuwa ni nini hadi muziki huo kuyumba hapo nyuma?

Asha: Hali ya uchumi ilikuwa imeyumba. Kwa kuyumba kwake ilipelekea mpaka watu wengi kufunga kumbi zao. Sasa bendi nyingi ziliamua kuacha kupiga katikati ya mji zikawa zinatoka nje ya mji kwenda kufuata kumbi, ndiyo maana zilionekana hazipo. Lakini bendi zipo na sasa shoo zinarudi kama zamani.

Risasi: Sawa, tuzungumzie msiba wa King Majuto (Amri Athuman), kwa upande wako umekugusa kwa namna gani?

Asha: Kiukweli umenigusa sana natamani siku zirudi nyuma na aendelee kuishi lakini hivyo inakuwa ni sawa na kumkufuru Mungu.

Ninachoweza kusema ni kwamba tujifunze kupitia mapito yake. Ameishi na watu vizuri. Kawasaidia vijana wengi kuwa juu kisanii. Alikuwa anazungumza na mtu yeyote na wala si mtu wa kuringa kama vijana wa siku hizi ambao wakipata majina tu kidogo wanajisahau na kuwadharau wengine. Kikubwa pia tumuombee huko anakokwenda apumzike kwa amani.

Risasi: Kuhusu Jokate Mwegelo naye, kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe una lolote la kuzungumza?

Asha: Ndiyo. Jokate amefungua njia kwa wasanii kuanza kupata vyeo. Unajua wakati Rais Dk. John Magufuli alipokuwa anaingia madarakani alituambia hatatusahau wasanii. Kwa kuanza na Jokate ametimiza ahadi aliyoitoa. Kwa hiyo tutegemee wasanii wengi kuwa viongozi.

Risasi: Alipoteuliwa tu kuna watu wakaanza kuonesha picha zake za zamani mitandaoni kwa lengo la kukosoa, unazungumziaje hilo?

Asha: Kikubwa watu ndio wanatakiwa kujifunza kwamba kuna hatua kila mtu anapitia akiwa kijana. Zile picha Jokate alizipiga akiwa mdogo, lakini pia alikuwa mwanamitindo na kijana ambaye alikuwa huru kufanya kila kitu.

Hazina uhusiano wowote na uwezo wake wa akili au uchapaji kazi wake. Nina uhakika pia Jokate atafanya makubwa kwenye nafasi hiyo aliyopewa.

Risasi: Huko nyuma unafikiri kwa nini wasanii walikuwa hawateuliwi kwenye nafasi za uongozi serikalini?

Asha: Tulikuwa hatuaminiki. Lakini ukweli tunaweza. Unaona kama kina Hadija Kopa wapo kwenye siasa kwa muda mrefu, mimi, kina Irene Uwoya au Wema Sepetu tumejaribu kugombea baadhi ya nafasi lakini hatukupata.

Si kwa sababu hatuwezi kuongoza, lakini pengine tulikuwa hatuaminiki, kwa Jokate kuanza na akionyesha makubwa wasanii tutaanza kuaminika na huko mbele wengi tutakuwepo serikalini.

Risasi: Una kipi cha kumalizia?

Asha: Twanga Pepeta tunajiandaa kufanya tamasha la miaka 20 ya bendi yetu. Tutazialika bendi nyingi na mpaka sasa ambayo imekwisha kubali kuwepo ni B Band ya Banana Zorro.

Kwenye tamasha hili tutawaenzi pia wote ambao wametangulia mbele za haki. Lakini pia kwa mashabiki wa Twanga Pepeta wasikose kila siku za Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili The Club Legend, kwani ndiko burudani ilipo kwa sasa.

BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.