The House of Favourite Newspapers

Jokha Kassim; Mtoto wa ‘Prezdenti’ Kaamua Kamtuliza

0

MAKALA: ISSA MNALLY | GAZETI LA AMANI

KAMA wewe ni mdau wa Muziki wa Taarab utakubaliana na mimi kwamba, mwanamama ambaye kwa muda mrefu amekuwa tisho apandapo stejini, Jokha Kassim, sasa hivi hayuko kama zamani!

Nikisema hayuko kama zamani namaanisha kuwa mbwembwe zimepungua, matashititi siyo kama enzi zileee na hata ile kuonekana sana kwenye majukwaa akitumbuiza, sasa hivi kapunguza.

Yawezekana wapo mashabiki wake wanaojiuliza kulikoni? Kama wewe ni kati yao, basi leo utapata jibu kwani nimebahatika kumpata na akazungumzia maisha yake ya sasa na sababu za kukauka kwenye kumbi za burudani.

Jokha ni nani?

Kwa wasiomjua, Jokha ni mwimbaji wa Muziki wa Taarab aliyeibuliwa na Bendi ya Zanzibar Stars baadaye akahamia Five Star kisha akajiunga na bendi ya mumewe ya T. Moto. Ukiachana na Jokha kuimba pia wadogo zake, Asina na Fatma Kassim nao ni waimbaji wa Taarab kwenye Kundi la Jahazi.

Kwa nini kapotea?

Akizungumzia sababu zinazomfanya asionekane majukwaani akiimba, Jokha anasema: “Mimi ni mke wa mtu, majukumu ya familia yananihitaji zaidi. Hivyo nasikiliza anachokipenda mume wangu na ndiyo maana mashabiki wangu hawanioni sana kama ilivyokuwa zamani, ila niko nao na wajue tu kwamba nawapenda na pale ninapokuwa free kuzirusha roho zao, nitafanya hivyo.”

Mumewe ni nani?

Aliyemchukua jumlajumla mwanamama huyu ni mmiliki wa iliyokuwa Bendi ya T.Moto ambaye pia ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Amin Salmin.

Mume ampiga stop Taarab

Kwa wale wafuatiliaji wa Muziki wa Taarab watakuwa wamesikia zile tetesi kuwa, mume wa Jokha alimzuia kufanya muziki huo, tetesi hizo zina ukweli kama anavyoeleza mwenyewe:

“Namheshimu sana mume wangu ndiyo maana aliponiambia niache kuimba ili niwe bize na masuala ya familia nikamtii ingawa ana mpango wa kuifufua bendi yake ya Tanzania Moto ‘T. Moto’ sasa sijajua kama nitaendelea kuimba huko au lah.”

Bendi kibao zinamhitaji

Jokha anasema kutokana na umahiri wake katika tasnia ya muziki huo wa mwambao, bendi kibao zinamhitaji lakini hawezi kwenda kinyume na matakwa ya mumewe. Anasema ndoa inastahili kuheshimiwa hasa katika ulimwengu wa sasa ambao kuolewa ni bahati.

Vipi kuhusu kuhudhuria matamasha?

Akilifungukia hilo, Jokha anasema: “Nimekuwa nikipata mialiko mbalimbali ya kushiriki kwenye matamasha ya Taarab Tanzania Bara na Visiwani, lakini huwa nakwenda kwa ruhusa ya mume wangu.”

Nyimbo alizotamba nazo!

Baadhi ya nyimbo alizotamba nazo Jokha ni Utakufa Nacho Kijiba cha Roho, Mtenda Akitendewa, Nia Njema ni Tabibu, Unalo Lililokukaa na Roho, Domo la Udaku, Yote ya Nini na nyinginezo.

Tujikumbushe

Baadhi ya makundi ya Taarab yaliyowahi kutamba siku za nyuma ni East Africa Melod, Babloom, Muungano, Mwichacho Zanzibar Star, Five Star na mengineyo ingawa kwa sasa mengi hayasikiki kivile huku nafasi kubwa kwenye ulimwengu wa burudani ikichukuliwa na Muziki wa Bongo Fleva.

Leave A Reply