The House of Favourite Newspapers

Joto la Mapenzi – 48

0

ILIPOISHIA…

    “Itakuwa vizuri mpigie yeye.”Ambe alimpigia simu Ester, baada ya kuita ilipokelewa upande wa pili.

    “Haloo.”

    “Haloo.”

    “Nani?”

    “Nazungumza na Ester?”

    “Ndiyo, nani mwenzangu?”

    “Ambe.”

    “Ha! Shemu?” Ester alishtuka.“Ester taratibu.”

    “Upo salama shemu?”

    “Ester nani?” Koleta alijikuta amenyanyuka kutaka kujua simu ya nani.

    ENDELEA NAYO…

“Shemu.”Koleta aliikwapua simu na kuzungumza:

“Haloo.”

“Koleta?”

“Ndiyo mimi, ooh mpenzi upo salama?”

“Ndiyo, upo wapi?”

“Nipo sebuleni.”

“Nenda chumbani kwako tuzungumze.”

“Haya mpenzi.”

Koleta alikimbilia chumbani kwake na kujifungia kwa ndani na kuanza kuzungumza na mpenzi wake.

“Haloo mpenzi nimo chumbani nimejifungia kabisa.”

“Za toka jana?”

“Mbaya.”

“Ubaya wake?”

“Hata sijui hukumu yangu kwako.”

“Hukumu ya nini tena mpenzi?”

“Kwa kitendo nilichokufanyia.”

“Hujafanya lolote, nina uelewa zaidi ya baba yako hivyo najua kila kitu.”

“Sasa kama unajua kwa nini hamkumuua?”

“Hajafa?”

“Ndiyo, risasi imempiga chini ya bega.”

“Kwa sasa yupo wapi?”

“Hospitali.”

“Ipi?”

“Huruma.”

“Sawa,” baada ya kusema vile simu ilikatwa.

“Haloo..halooo.”

Koleta aligundua simu imekatwa. Alijaribu kuipiga lakini ilikuwa imezimwa upande wa pili, alijiuliza Ambe atakuwa wapi na kwa nini hakutaka kujua hata hali ya mwanaye.

Wakati akiwaza yale Ambe baada ya kukata simu alimgeukia Mabina aliyekuwa akimsikiliza kwa umakini.

“Yule mzee hajafa.”

“Nilijua alikuwa amekaa kwenye tageti mbaya hata hivyo nilijitahidi sana, hiyo hospitali unaijua?”

“Ndiyo.”

“Twende tukafanye savei usiku tumalize kazi.”

“Hakuna tatizo.”

Ambe na Mabina walielekea ilipo hospitali ya Huruma kuangalia mazingira yake. Walipofika waliingia mpaka ndani na kufanya uchunguzi wao na kugundua hakuna ulinzi wa maana.

Hali ile iliwapa matumaini ya kutekeleza mpango wao kwa urahisi.

Waliamua kurudi kijijini kwao kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa usiku. Koleta baada ya kuwa na uhakika wa usalama wa mpenzi wake, aliamini kazi iliyokuwa imebaki kwake ni yeye kucheza upande wake ili kuonesha yupo pamoja na mpenzi wake.

Aliamini kama atampokea mama yake usiku ili alale na baba yake basi ile ingekuwa nafasi nzuri ya kutekeleza mpango wa kumuua baba yake.

Alimpigia simu mama yake kuwa  usiku atalala yeye na baba yake.

“Mama leo nitakupumzisha nitalala mimi na baba.”

“Hakuna tatizo mwanangu, tena umejua maana kulala nimekaa mgongo wote unaniuma.”

“Hakuna tatizo mzazi wangu, nipo kwa ajili yenu.”

“Umenifurahisha kwa  moyo wa upendo mwanangu.”

“Nisipowapenda ninyi wazazi wangu nimpende nani?”

“Haya basi baadaye.”

Koleta baada ya kukata simu alijikuta akilia kwa kitendo alichotaka kukifanya usiku ule cha kumuua baba yake lakini hakuwa na jinsi kwani aliamini kifo cha baba yake ni faraja ya moyo wake.

                                                                  ****

Koleta alijiandaa kwenda kumpokea mama yake akiwa na lengo la kummaliza baba yake.

Majira ya saa mbili usiku alikwenda mpaka hospitali kumpokea mama yake. Mama yake alimshukuru sana Koleta kwa moyo wa upendo aliouonesha kwa baba yake pamoja na kumfanyia mambo mabaya.

“Asante mwanangu kwa kuonesha unamjali baba yako.”

“Mama unafikiri nikifuata mambo ya baba tutakuwa pamoja, nimeamua kumsamehe ili tujipange upya.”

“Asante mwanangu kwa maneno matamu ngoja nirudi nyumbani.”

“Haya mama mumeo anakusubiri.”

“Mmh! Mume wangu hata kuja kumuona babu yake hataki?”

“Analia wivu, lakini atakuja tu.”

Koleta aliagana na mama yake aliyerudi nyumbani na yeye kwenda kukaa na baba yake.

Alikaa kwenye kiti kwa muda kisha alinyanyuka na kumuangalia baba yake aliyekuwa amepitiwa na usingizi kutokana na kumeza dawa za maumivu.

Alimuangalia baba yake kwa hasira huku roho ya huruma ikimjia, alijiuliza amuue baba yake kwa ajili ya mwanaume tu.

Pamoja na matatizo ya baba yake bado alitakiwa kumheshimu kwa kuamini yote aliyofanya ni kwa ajili yake japo alimgeuka na kumfanyia kitu kibaya.

Uamuzi wa kumuua ulikuwa mgumu sana moyoni mwake japo alikuwa na mtihani mzito kwa Ambe aliyeapa kumuua baba yake. Alijiuliza atafanya nini kuweza kumshawishi tena mpenzi wake amsamehe baba yake kitu ambacho alijua hakitawezekana hata siku moja.

Alimuomba Mungu amuepushe na moyo wa ukatili uliopanga kumuua baba yake kwa ajili ya mapenzi.

Aliyakumbuka maneno ya Ester kuwa baba ni kila kitu vilevile mzazi hakosei kwa mtoto.

Aliamua kuachana na mawazo ya kumuua baba yake na kuwa upande wa baba yake huku akitafuta suluhu ya kumaliza tatizo la baba yake na mpenzi wake.

Baada ya kumgeuza vizuri baba yake aliyekuwa amelala vibaya alitengeneza kiti chake na kujilaza kwa nyuma huku akinyoosha  miguu kwenye stuli ndogo iliyokuwa mbele yake.

 Masikioni aliweka hedifoni pana na kuweka muziki toka katika iPod uliombembeleza na kujikuta akipitiwa na usingizi bila kujijua.

Wakati akipitiwa na usingizi Ambe na Mabina walikuwa ndiyo wanawasili nje ya hospitali ya Huruma.

Kwa vile muda ulikuwa bado na pilikapilika za ingia toka katika hospitali ile kubwa ilikuwa bado, lakini haukuwa msongamano mkubwa kama wa mchana.

Walitafuta baa ya karibu ili kuvuta muda kabla ya kuingia hospitalini na kukifanya kilichowapeleka pale.

Majira ya saa sita na nusu baa ilianza kupungua watu huku wahudumu wakianza kupanga viti, waliona ule ni muda mzuri wa kuingia hospitali kufanya kazi yao ambayo waliamini muda mfupi ulitosha kumaliza kazi.

Waliingia taratibu hadi mapokezi ambako muuguzi alikuwa amepitiwa na usingizi, hawakutaka kumshtua walielekea kwenye chumba alicholazwa mzee Mtoe kufuatana na maelekezo waliyopewa na Koleta.

Mabina aliyetangulia mbele alizungusha kitasa taratibu bila kupiga kelele lakini kwa haraka huku Ambe akiangalia usalama.

Lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyepita muda ule kuonesha wagonjwa,  madaktari wa zamu na wauguzi walikuwa wamepitiwa na usingizi.

Baada ya mlango kufunguka alichungulia ndani kabla ya kuingia na kumuona mzee Mtoe amelala kitandani akiwa amepitiwa usingizi.

Pembeni yake alikuwepo Koleta ambaye naye alikuwa amepitiwa na usingizi huku akiwa na hedifoni masikioni.

Alimfanyia Ambe ishara ya mkono kuwa amfuate ndani,  kwa haraka aliingia ndani wakati huo kila mmoja alikuwa ameshikilia bastola mkononi.

Ambe alirudisha mlango alipogeuza kichwa alishtuka kumkuta mpenzi wake Koleta yumo mule ndani.

Alimuuliza Mabina kwa ishara wamuamshe Koleta au? Mabina alimkataza na kusogea kitandani na kumkuta mzee Mtoe akiwa katika usingizi mzito.

“Tummalizeje?” Mabina alimuuliza kwa sauti ya kunong’ona.

 Je, nini kitaendelea? Tukutane wiki ijayo.

Leave A Reply