The House of Favourite Newspapers

JPM Aanika Majina ya Matajiri Vinara wa Kukwepa Kodi – Video

RAIS Dkt. John Magufuli amesema wapo wafanyabiashara wakubwa nchini ambao wamekuwa wakikwepa kodi kwa kupitia makontena wanayoingiza na wengine kupitia njia za mipakani kupeleka biashara zao nje ya nchi.

 

Magufuli amesema hayo leo wakati akizungumza na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakuu wa Mikoa nchi nzima katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam na kusema majina yao anayo lakini anashangazwa na TRA kutochukua hatua sitahiki.

 

“Nawataka TPA, TRA, polisi na Idara ya uhamiaji mjirekebishe, vipo vitendo vingi vya kukwamisha wawekezaji naomba mlifanyie kazi. TRA toeni adhabu kwa wakwepa kodi ilimradi msiwaonee na hili litakuwa rahisi tu endapo mtapunguza viwango vya kodi watakuja wenyewe kulipa.

 

“Wapo watu wamekuwa wakikwepa kodi, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tarafa wote mpo. Wakati mwingine naonaga kidogo kwenye TV mmekamata watu, ila najua ile mnafanyajaga kujitangaza kuwa mpo, baada ya muda hali inarudi ile ile.

 

“Mimi nina majina ya wafanyabiashara wa Kariakoo ambao wanaingiza bidhaa zao bila kulipa kodi kwenye mipaka yetu na wanashirkiana na vyombo vya dola nashangaa wakuu wa wilaya na mikoa hamuwajui. yupo mmoja jina linaishia na ‘AGENCY’, mwingine ‘O’.

 

“Yupo mfanyabiashara kule Mwanza, halipi kodi na anapitisha magari hata 10 kwa siku moja. Wapo wafanyabiashara wengine wawili wao huleta makontena hadi 700 Kariakoo kwa mwak kisha wanawauzia wengine. Nashangaa TRA, RC Dar hamuwajui.

 

“Gavana wa BoT (Prof. Florens Luoga) ameeleza hapa alipovamia maduka ya kubadilishia fedha Arusha, alikuta maduka 37 hayana leseni, huku mengine yakifanya biashara bila hata TRA wenyewe kujua na serikali haipati hata shilingi 10.

 

“Najua kuna kitengo pale TRA mtu akiwa na makosa anafunguliwa kesi baada ya muda kesi inafutwa kwa maelewano maalumu bila huyo mtu kulipa kodi. Wapo wafanyabiashara hutetewa na wanasiasa eti wanasaidia chama, mimi ndiyo mwenyekiti wa chama nasema wote walipe,” amesema Magufuli.

VIDEO: FUATILIA TUKIO HILO HAPA

Comments are closed.