The House of Favourite Newspapers

JPM Amtaja Aliyeingiza Magari 194 Akagoma Kulipa Kodi, Ataja Siri Nzito! – Video

RAIS John Magufuli ameanika madudu yanayofanywa na baadhi ya viongozi kwa kushindwa kutimiza wajibu wao vizuri huku wakiwakumbatia wala rushwa na wakwepa kodi,  jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

 

Magufuli amesema hayo baada ya kumwapisha Valentino Mlowola kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na kupokea taarifa ya mwaka ya utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wake, CP Diwani Athuman, leo Alhamisi, Machi 28, 2019, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

 

“Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru hivi karibuni ulinieleza kuwa kuna mtu ameagiza magari 194 bila kuyalipia kodi, maana yake amekwepa kodi zaidi ya shilingi bilioni 8. Lakini ametetewa kweli na watu, unaweza kuona mlivyo na kazi ngumu kwenye kazi zenu,” alisema rais.

 

“Kwa renki ya upolisi aliyofikia Kamishna wa Takukuru (Diwani Athuman) ni mtumishi wa TISS (Taaisi ya Usalama wa Taifa), leo nimetaja siri ya kazi yako nyingine kwa sababu ya kazi kubwa unayofanya, nataka watu wajue, wasikuone wa kawaida, najua IGP Sirro atashangaa, lakini ndiyo ukweli.

 

“Nilikuteua ili hata kama ni mtu wa usalama amekula rushwa umkamate umshughulikie, msaidizi wako ambaye ni Brigedia, hata hata akimkamata mwanajeshi akipokea rushwa atamsondeka ndani huku wakipigiana saluti. Ukishindwa kutumia sheria za Takukuru, tumia hata za polisi.

 

Aidha, amesema wapo baadhi ya wafanyabiashara wana mashine za EFD walizopewa na Serikali na nyingine zao wenyewe, wana Tax Refund nyingi ambazo ni za kughushi na kufanya serikali kupoteza mapato. Amesema nchi hii ina watu wengi hatari na wanaiibia serikali katika ukusanyaji mapato na kwamba wezi wana tabia ya kuteteana.

 

Kuhusu maduka ya kubadilishia fedha,  amesema; “Hizi Bureau de change zinafunguliwa kama uyoga, mimi niliwahi kwenda Ujerumani, nikataka kubadili Dola 2,000, nilikaguliwa hadi passport zangu, hapa mtu anabadili mamilioni ya Dola kawaida tu.

 

“Takukuru ni chombo kilichobaki kinachotisha, sasa mkakitumie vizuri katika kutenda haki, katika uchunguzi mfanye vizuri, msionee mtu ili msije baadaye mkajibebea dhambi za bure, katendeni haki,” amesema Rais Magufuli.

VIDEO: MSIKIE MAGUFULI AKIFUNGUKA

Comments are closed.