The House of Favourite Newspapers

JPM Apiga STOP Wanunuzi Korosho, Serikali Itainunua kwa 3,300/= – VIDEO

RAIS John Magufuli amemtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuachana na wafanyabiashara wa korosho waliopewa siku nne na serikali hadi leo Jumatatu, saa 10:00 jioni kuwasilisha majina yao na idadi ya tani za korosho watakazonunua na lini watazinunua kwa bei elekezi ya Tsh. 3,000, ambapo amesema serikali itazinunua korosho hizo kutoka kwa wakulima kwa bei ya Sh. 3,300 kwa kilo.

Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu, Novemba 12, 2018 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akihutubia mara baada ya kuwaapisha mwaziri wawili na manaibu waziri wanne aliowateua juzi Jumamosi. 

Awali, akitoa maelezo kuhusu mchakato huo, Majaliwa alitaja kampuni moja ya China iliyotaka kununua tani  200,000 na makampuni mengine ya nchi za nje yaliyotaka kufanya hivyo pia.

Rais alisema alisikitishwa na uamuzi wa Bodi ya Korosho nchini kutoa bei elekezi ya sh. 1,500 kwa kilo moja ya korosho ambapo bei ya kawaida bodi hiyo ilisema ni 1,000.

“Nikaona Bodi ya Korosho haipo kwa ajili ya manufaa ya Watanzania. Nikawapa bei elekezi ya shilingi  3,000 lakini siku ya mnada bodi hiyo iliongeza shilingi moja na aliyeongeza zaidi miongoni mwa wanunuzi kiwango kilifikia 3,016,” alisema Magufuli na kuongeza kwamba huo ulikuwa ni mchezo uliopangwa ili mvua ikianza wanunuzi hao wakainunue korosho kwa bei ya chini kwa sababu wakulima wangeogopa kuharibikiwa zao hilo.

“Korosho tunainunua wenyewe kwa shilingi  3,300 kwa kilo moja badala ya 3,000. Benki ya Wakulima nchini watatoa fedha na Jeshi litaichukua korosho  likabangue kwa namna watayoona inafaa,” alifafanua.

Alisema maghala yote ya korosho yatalindwa na Jeshi la Wananchi na kwamba kiwanda cha kubangua korosho kilichopo Lindi amekikabidhi kwa jeshi mara moja ili kiendelee na kazi hiyo.

“Korosho yetu ni daraja la kwanza duniani lakini wananchi wanaishi maisha ya chini,” alisema na kuongeza kwamba mamlaka za kuwalinda wakulima hazifanyi kazi inayotakiwa, na pia alitoa wito kwa jeshi kuianya kazi hiyo kwa uadilifu kwa ajili ya taifa kwa jumla.

VIDEO: MSIKIE HAPA AKIFUNGUKA

Comments are closed.