The House of Favourite Newspapers

 Jux: Amethubutu, ameweza

WEKA pembeni uhusiano wake na yule ‘Mchina’ mwenye asili ya Thailand, Nayika Thongom, kwa sasa Juma Musa ‘Jux’ ndiye habari ya mjini kwa upande wa wasanii wanaokimbiza katika Muziki wa R&B Bongo.

TULIPOTOKA

Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, ni wasanii wachache tu waliokuwa wakifanya Muziki wa R&B Bongo, wenyewe na walikuwa wa kuwahesabu kama vile Mr. Paul, Mad Ice na wengineo.

Baada ya kuondoka kizazi hicho ambapo wengi wao kwa sasa wapo nje ya nchi wakiendeleza maisha yao mengine, walikuja wengine ambao ni Nemo pamoja na Steve R&B nao hawakuweza kukaa kwenye gemu kwa muda mrefu, wakajikita kwenye bendi za Muziki wa Dansi.

BEN POL

Kizazi kipya kilichokuja kuibuka katikati ya miaka ya 2000 kikawa kwa Ben Pol na Jux ukipenda waweza kumuita African Boy.

Kwa upande wa Ben Pol, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuachia albamu tatu ambazo hazikuingia sana masikioni mwa watu kama vile Maboma aliyoiachia mwaka 2012 ikiwa na ngoma tisa, mwaka 2014 akaachia albamu nyingine ya Ben Pol iliyokuwa nayo na ngoma tisa na mwaka 2017 akaachia albamu yake ya Best Of Ben Pol.

Ukizisikia albamu zake zote, hazikuwa katika levo ya kuitwa albamu kutokana na kuchanganywa ngoma. Mfano ukisikiliza albamu ya mwaka 2012, 2014 na 2017 ngoma karibia sita zote zinajirudia katika albamu hizo.

JUX

Jux anayeshikilia rekodi ya kuwa msanii pekee wa R&B Bongo kufanya video nyingi nje ya nchi kuliko msanii mwingine yoyote wa muziki huo Bongo, tangu katikati ya miaka ya 2000 hakuwahi kuibuka na albamu yoyote zaidi ya kuachia singo ambazo zote zilipokelewa vema na mashabiki.

Miongoni mwa singo hizo ni Uzuri Wako, Utaniua, Sisikii, Nitasubiri, Nimedata, Juu na Napata Raha. Licha ya singo hizo kubamba vilivyo, hakuwahi kuziweka kwenye albamu ya pamoja.

Kwa sasa Jux amethubutu kuachia albamu yake ya kwanza ya The Love ikiwa na ngoma 18. Katika mahojiano niliyowahi kufanya naye, Jux anasema albamu hiyo ni kitu kikubwa sana kwake na kwamba kama ingekuwa ni chuo, basi kwake ni cheti.

“Hii ni albamu yangu ya kwanza toka nimeanza muziki, Ilikuwa ni ndoto yangu kwa muda mrefu kutimiza hili na leo Mwenyezi Mungu amenisaidia nimekamilisha.

“Ndani ya albamu hii nimeweka asilimia nyingi sana maisha yangu na maisha ya watu tofauti. Nikiamini kwa namna moja au nyingine itahusiana au kuwagusa mashabiki wangu kwa njia tofauti tofauti,” anasema Jux.

Jux anasema kilichomsukuma kuachia albamu hiyo ni kwa sababu amepitia vitu vingi sana katika uhusiano wake wa kimapenzi kwani amewahi kuacha, kuachwa, kulizwa, kuliza, kuumizwa, kuumiza kupenda na kupendwa.

“Katika mambo yote haya yamenifanya niwe imara na bora zaidi. Asante Vanessa Mdee ‘Vee Money’ nimekuwa kwenye muziki ni miaka 10 sasa. Miaka saba yote nimekuwa nao kwenye maisha yangu, 75% ya maisha yangu kwenye mapenzi (uhusiano) ni wao.”

Albamu hiyo ya The Love imepikwa na maprodyuza wakali Bongo akiwemo Manecky, Bob Manecky,S2kizzy, Chiz Brain, Abbah Process, Elipiano Msimbe, Mr T Touch, Mocco Genius, Mr VS, Luffa na Paul Maker.

Walioshirikishwa ni Ruby, Nyashiski (Kenya), G Nako,Tommy Flavour, Vanessa Mdee, Diamond Platnumz, Singah (Nigeria),Q Chief na Joh Makini, huku waliohusika kuandika mashairi ni Walter Chilambo na Marioo.

Hata kama ukiwa huna jicho la kuona lakini unapotazama kazi kubwa aliyoifanya Jux hongera lazima zimuendee na nishani ya kuutendea haki muziki wa R&B inapaswa kuwa mabegani kwake.

Bila shaka Jux anasimama kama jasiri muongoza njia anayestahili kufuatwa na vizazi vijavyo wa wanaR&B katika nchi yetu.

Hii ina maana kwamba kuweza kwake kuushika muziki huo laini kwa miaka zaidi ya kumi bila kumponyoka ni mafanikio kwake binafsi na sanaa kwa ujumla; hongera Jux umethutu na bila shaka umeweza!

Comments are closed.