The House of Favourite Newspapers

Jux, Huddah penzi ni kikohozi!

0

 

AMA kweli penzi ni kikohozi! Huu ni msemo wa siku nyingi wa wahenga, lakini sasa unafanya kazi kwa mastaa wengine wawili Afrika Mashariki.  Hawa ni staa wa Bongo Fleva kutoka Tanzania, Juma Musa ‘Jux’ na video vixen (modo kwenye video za muziki) matata wa Kenya, Huddah Monroe ‘The Boss Chick’.

Kama tujuavyo penzi halielezeki au halina tafsiri maalum. Kila mtu ana maelezo yake kuhusu penzi na maelezo hayo hutegemea zaidi na uzoefu wake. Lakini wanasaikolojia wengi wanakubaliana kwamba, penzi ni hisia zenye nguvu ya ajabu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hisia hizo hazijalishi muonekano, utajiri, umri, elimu, aina ya maisha au tabia.

Hisia hizo humfanya mtu ashindwe kabisa kufanya mambo ya kawaida ambayo huyafanya kila siku kwa vile kichwani anakuwa anamfikiria yule ampendaye. Hisia hizo zinaweza kumsababishia mtu kubadilisha wasifu na tabia zake hasa pale anapofanikiwa kuwa na huyo ampendaye.

Anapofanikiwa kumpata yule ampendaye, huwa anapata raha ya ajabu kila anapomuona, inakuwa ngumu mno kuwa mbali naye. Hisia hizo zikikomaa, humfanya mtu kuhisi maumivu ikiwa huyo anayempenda anaumwa, amemuudhi au ameudhiwa na mtu mwingine. Anapokuwa na huzuni, hakika naye huhisi huzuni!

TUJIUNGE VISIWANI ZANZIBAR

Hicho ndicho kinachotokea kwa Jux na Huddah! Mapema Januari mwaka huu, Jux na Huddah ambaye anatajwa kuwa na utajiri mnono, walionekana wakioneshana mahaba mazito wakiwa katika hoteli moja ya kifahari kwenye visiwa vya marashi ya karafuu, Zanzibar. Tukio hilo lilikuja siku chache tu baada ya Jux kudaiwa kumwagana na yule mchumba’ke, Nayika Thongom, raia wa nchini Thailand.

Kabla ya tukio hilo la Zanzibar, Jux na Huddah hawakuwahi kuhusishwa kutoka kimapenzi. Lakini mara kadhaa Huddah aliwahi kunukuliwa akisema anamzimia mno Jux, lakini alikuwa akimheshimu mwanamuziki Vanessa Mdee ‘V-Money’ ambaye alikuwa mchumba wa jamaa huyo kabla ya Nayika.

Katika moja ya intavyu zake, Huddah alisikika akisema kuwa Jux ni mwanaume ambaye yeye anaweza kuwa naye kwenye uhusiano wa kimapenzi huku akimmwagia sifa kuwa ana muonekano mzuri kwenye mavazi.

“Aaah…Nafikiri ni mwanaume ambaye ninaweza kuwa naye kwenye uhusiano…Si yupo single? Hata mimi ninapatikana…” Alisema Huddah. Huddah alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa, yeye ndiye aliyeanza kumcheki Jux kupitia mtandaoni na kumwambia jinsi gani anapenda muonekano wa mavazi yake; jinsi anavyovaa tofauti na wengine.

HUDDAH ATUMIA FURSA

Sasa basi, wananzengo wanasema, baada ya kuwa na uhakika kwamba Jux hayupo tena na V-Money, mrembo huyo maarufu mitandaoni (sosholaiti), aliona Nayika ni mwepesi na ni fimbo ya mbali (anaishi Bangkok, nchini Thailand barani Asia, yapata kilometa 7,135 kutoka Dar nchini Tanzania), hivyo akatumia fursa vizuri.

Kwa mujibu wa kurasa za udaku za Instagram, kwa sasa Jux na Huddah wanainjoi penzi lao baada ya kuviziana kwa muda mrefu.

WASHINDWA KUJIZUIA

Baada ya kuwepo kwa tetesi za penzi hilo huku kila mmoja akiumauma maneno kila anapoulizwa, ukaribu unaripotiwa kuzidi kukolea na kidogokidogo wenyewe wanaanza kushindwa kujizuia kujianika.

Hilo linazidi kuthibitika kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo juzikati f’lani, Jux aliposti picha kisha Huddah akaja kuweka maoni kwa kuandika; “Yaani sasa hivi Zanzibar ni sehemu bora ya kukaa rafiki yangu, nitakuona huko!”

Baada ya Huddah kuweka maoni hayo, Jux naye akamjibu kwa kuandika; “Kabisa rafiki yangu, asante kwa kuniongezea mwanga rafiki yangu!”

JUX AFUNGUKA

Ili kuweka mambo sawa juu ya penzi hilo lingine matata linalounganisha Tanzania na Kenya, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Jux ambapo alifunguka;

“Mashabiki wetu wajue tu kwamba, tuna project inakuja. Si kweli kwamba tuna uhusiano wa kimapenzi na pia wajue Huddah anapapenda sana Zanzibar, ndiyo maana huwa tunakutania huko. Mbali na hilo, wote ni wafanyabiashara. Huddah ana bidhaa zake za urembo kama lipstick, na mimi nina bidhaa zangu za mavazi ya African Boy.”

UTAJIRI WAO

Kwa mujibu wa ripoti za mwaka jana za Mtandao wa CelebrityNetWorth wa Afrika Mashariki, Jux alitajwa kuwa na utajiri uliokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 2 za Kitanzania.

Kwa upande wake, Huddah ambaye alipata umaarufu zaidi aliposhiriki Shindano la Big Brother Africa (BBA), alikadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya shilingi bilioni 6 za Kitanzania akishindana na mwanamama mjasiriamali wa Uganda; Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ mwenye zaidi ya shilingi bilioni 10 za Kitanzania.

Jux anaungana na mastaa wengine walioingia kwenye mapenzi na wanawake wa Kenya wakiwemo; Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ aliyemuoa Amina Khaleef, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyezaa na Tanasha Donna na Benard Paul ‘Ben Pol’ aliyemchumbia Anerlisa Muigai.

MAKALA: NEEMA ADRIAN

 

Leave A Reply