Jux + Vee Money = Project?

Haya mapenzi basi ya kisela,

Leo raha kesho wanisema,

Haya mapenzi basi ya kisela,

Leo raha kesho wanikera,

Haya mapenzi basi ya kisela,

Si ulisema kamwe hutonitenda,

Moyo wangu hauna uwezo tena,

Kwani mapenzi haya ya kisela…

 

NI mistari inayopatikana katika Ngoma ya Kisela ya Vanessa Mdee ‘Vee Money’ akiwa amemshirikisha staa wa muziki kutoka Nigeria anayeunda Kundi la P Square, Peter Okoye.

Ni bonge moja la ngoma, kideo chake Vee Money amejiweka kama mmoja kati ya mabondia akibishana na bondia Peter kuhusiana na mapenzi.

 

Achilia mbali kideo hicho na kilichozungumzwa, wakati huo penzi la Vee Money na staa wa R&B Bongo, Juma Khalid ‘Jux’ lilikuwa moto wa kuotea mbali Bongo.

Penzi lao lilikuja kukolezwa zaidi na ziara ya pamoja ya In Love & Money ambayo ilitokana kwa kuunganisha majina ya albamu zao Money Mondays ya Vee Money na The Love ya Jux.

 

TETESI ZASAMBAA

Baada ya kumaliza ziara hiyo, kila mmoja alikuwa kivyake na hata katika kurasa zao katika mitandao ya kijamii hawakuwa wakipostiana kama ilivyokuwa nyuma. Hawakuwa wakiongozana tena au kuonekana pamoja, madai yakazidi kusambaa kama moto wa kifuu kuwa wawili hao hawapo pamoja tena.

 

VEE MONEY ATHIBITISHA

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Story ‘Insta Story’, Vee Money aliulizwa na shabiki kuhusiana na tetesi za kuachana na kuweka wazi kuwa hawapo pamoja tena;

“Ndio tumeachana, lakini ni marafiki wazuri sana na tutabaki kuwa familia daima.”

 

JUX AIBUKA

Juzikati wawili hao wameibuka tena baada ya Jux kuachia Ngoma ya Sumaku akiwa amemshirikisha Vee Money ukiwa ni wimbo wake wa kwanza kutoka katika albamu yake ya The Love.

Muda mfupi baada ya Vee Money kuweka kava la ngoma hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram, mashabiki wengi walifurahi kurudiana kwao ambapo Jux naye aliibukia katika posti hiyo na kukomenti; ‘Mtu wa Mungu, mtoto wa Kipare.’ kitu ambacho hakuwahi kukifanya tangu tetesi za kuachana zisambae.

 

MREMBO WA JUX GUMZO

Wakati kukiwa bado na sintofahamu juu ya wawili hao, limeibuka jambo jipya ambapo mwanamitindo mwenye asili ya Thailand, Nayika amegeuka gumzo baada ya picha zake za mitego kusambaa zikimuonesha akiwa kwenye bwawa la kuogelea na Jux.

Katika picha hizo, nyingine zinamuonesha akiwa amevaa nguo za kuogelea zinazoonesha wazi eneo kubwa la mwili wake na nyingine akiwa na Jux juu ya gari katika hifadhi ya wanyama ya Serengeti.

 

NI PROJEKTI?

Kwa asilimia kubwa inaonekana Jux na Vee Money hawajaachana bali waliamua kuliweka wazi ili kuwaweka mashabiki katika sintofahamu kabla ya kuachia wimbo wao.

Vipo viashiria vinavyoonesha wawili hao wapo pamoja kikiwepo cha kuanza kupostiana katika mitandao kupitia kazi zao ambapo Vee Money amekuwa akiupaisha Wimbo wa Sumaku kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii huku Jux naye akiposti Wimbo wa Moyo wa Vee Money kupitia kurasa zake.

 

Mwanamitindo Nayika ambaye anaonekana kuwahi kusoma nchini China kama ilivyokuwa kwa Jux, wapo Serengeti siyo kama mtu na mchumba wake bali maalum kwa projekti ya Sumaku.

Tayari mwanamitindo huyo kupitia ukurasa wake wa Instagram amekuwa akiposti picha akiwemo Serengeti na kuweka ishara kuwa anafanya maandalizi ya video ya Sumaku.

ANDREW CARLOS


Loading...

Toa comment