The House of Favourite Newspapers

Kabendera Akwama Kortini, Arudishwa Rumande Siku 12 – Video

KESI ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera, imeahirishwa kutokana na hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile, kupata udhuru.

 

Mbali na hakimu huyo kupata udhuru, wakili wa serikali mwandamizi, Wankyo Simon, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Simon ameeleza hayo leo Jumatatu Agosti 19, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mmbando kwamba hakimu anayesikiliza shauri hilo ambaye ni hakimu mkazi mwandamizi, Augustine Rwizile, amepata udhuru.

 

Wakati Simon akieleza hayo, wakili wa Kabendera, Jebra Kambole, ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi wa shauri hilo unakamilika kwa wakati kutokana na mteja wake kutokuwa na dhamana.

“Hatuna pingamizi kuhusu kupata udhuru kwa hakimu, ila tunaomba upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hii iweze kuendelea kwa sababu mteja wangu anaendelea kusota rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana,” amesema Kambole.

 

Kabendera amerudishwa rumande kwa siku 12 baada ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Agosti 30, 2019.

Comments are closed.