The House of Favourite Newspapers

Kaburi la Banza Latelekezwa

kaburi-la-banza-stone-2STORI: ISSA MNALY NA MAYASA MALIWATA | GAZETI LA UWAZI, Toleo la Desemba 20, 2016

DAR ES SALAAM: Kaburi la aliyekuwa mwanamuziki nyota, Ramadhani Masanja maarufu kama Banza Stone, lililoko katika makaburi ya Sinza jijini hapa, limetelekezwa, Uwazi linaweza kuthibitisha.

Gazeti la Uwazi lilifanya ziara ya kushtukiza katika kaburi hilo, miezi 17 tangu kufariki kwake na kukuta udongo wa katikati ukiwa umebonyea, huku kingo za ukuta uliojengwa kwa matofali zikiwa zimeweka nyufa, zinazoweza kulifanya likabomoka wakati wowote.

Baadhi ya watu wanaoshinda katika makaburi hayo, waliliambia Uwazi kuwa kwa kipindi kirefu hawajawahi kuona ndugu au jamaa wa marehemu wakilitembelea kaburi hilo, ambalo kibao kimoja kati ya viwili vilivyoandikwa jina lake kimedondoka.

1banza1Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ enzi za uhai wake.

Gazeti hilo liliwasiliana na kaka wa marehemu, Hamis Masanja, ambaye baada ya kuelezwa kuhusu kukutwa kwa kaburi hilo likiwa hovyo, alikiri na kusema;

“Itakuwa tumepishana tu, hata sisi jana (Jumamosi) tulikwenda pale na mafundi ili waangalie namna ya kufanya. Kuna mtu mmoja rafiki yake marehemu anaitwa Manyolii anaimba Singeli ameahidi kutusaidia, sisi kama familia hali yetu siyo nzuri kidogo.

“Wasanii kama Ally Choki na Asha Baraka tunashirikiana nao vizuri, lakini siyo kila kitu uwategemee wao, hata hivyo nadhani tutafanikisha kuliweka sawa kaburi la marehemu,” alisema.

kaburi-la-banza-stone-1Kaburi la Banza Stone

Ally Choki, aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Banza Stone kikazi, ambaye pia alikuwa bosi wake wakati akiwa Extra Bongo, alisema kimsingi suala la kaburi hilo ni la kifamilia, ila yeye kama rafiki na mwajiri wake wa zamani, anaweza kufanya ubinadamu kwa kushirikiana na ndugu zake.

“Ni lazima familia ishiriki, maana nikisema mimi kama mimi niende kaburini kwake ndugu yangu unafikiri watu watasemaje? Lakini kama familia itatushirikisha, nadhani tunaweza kutoa msaada unaohitajika,” alisema.

Mwajiri mwingine wa zamani wa Banza, Asha Baraka, alisema yupo tayari kushirikiana na familia kuhakikisha kaburi la mwanamuziki huyo linawekwa katika hali inayolingana na hadhi yake.

“Mimi silijua kaburi lake lilipo kwa sababu unajua sisi watoto wa kike wa Kiislamu haturuhusiwi kwenda makaburini siku ya mazishi, na kaburi linatakiwa kuangaliwa. Mimi nimetoka mbali sana na Banza, ninashukuru kwa kunipa taarifa hizo, nitawasiliana na Hamis ili waniambie jinsi ninavyoweza kusaidia jambo hili.

“Tunatembelea makaburi ya wanamuziki wetu kila mara, nimeshaenda kwa Hamis Amigolas na Tanga kwa Abuu Semhando ambako tuliweka mambo vizuri, hata hili litashughulikiwa, tuombe Mungu,” alisema Asha Baraka.

 

Sanchoka: ‘Nilimuokota’ Idris Sultan Kwenye Apartment Sauzi, Amfungukia Gigy Money

 

Comments are closed.