The House of Favourite Newspapers

Kahaba Kutoka China-09

0

Maandamano bado yalikuwa yakiendelea ndani ya nchi ya China katika mji mkuu wa Beijing. Watu zaidi ya laki saba walikuwa barabarani wakiyaendeleza maandamano hayo huku wakiwa wameshika mabango makubwa ambayo yalikuwa yakimtaka Waziri wa Afya wa China, Bwana Zhan Wei kujiuzulu kutokana na yale ambayo yalikuwa yakiendelea kutokea nchini hapo.

Maandamano yale hayakuishia Beijing tu, bado yalikuwa yakiendelea zaidi na zaidi mpaka katika miji mingine. Yalingia mpaka Lanfang na kuelekea mpaka Tianjin. Ndani ya masaa saba tu, miji mingi ya nchini China watu wake walikuwa wameingia katika maandamano hayo makubwa ambayo yalikuwa yakitaka waziri wa afya huyo ajiuzulu kutoka na ubadhilifu wa fedha ambazo alikuwa ameziiba.

Ufisadi ambao alikuwa ameufanya kuchukua zaidi ya dola bilioni mbili ukaonekana kuwakasirisha Wachina ambao hawakuwa wakipenda hata siku moja kiongozi yeyote wa Serikali kuiba kiasi chochote  kile cha fedha. Kila Mchina alikuwa akitaka waziri Zhan ajiuzulu yeye mwenyewe na kisha kufikishwa mahakamani kwa kile ambacho alikuwa amekifanya.

Maandamano hayakuisha, watu wengine hawakuwa wakienda kazini, kila siku saa mbili asubuhi walikuwa wakikutana na kisha kuanza maandamano. Nchi ya China ikaonekana kutokuwa nchi ya amani katika kipindi hicho hasa kwa wageni ambao walipokuwa wakiteremka na ndege katika viwanja vya ndege vya Kimataifa kama Beijing, Changchun, Anyang, Changzhou pamoja na viwanja vingine.

Waandishi wa habari wengi hasa wa Kimataifa walikuwa wameelekea nchini China kwa ajili ya kuandika kile ambacho kilikuwa kikiendelea wakati huo. Kila mtu alionekana kuwa na hasira kiasi ambacho wakati mwingine walikuwa wakimlaumu rais wao, Bwana Wou Peng kwa kumkingia kifua swahiba wake aliyeufanya ufisadi, Waziri Zhan Wei.

Watu hawakukoma hata mara moja, bado kila siku hali ilikuwa ikiendelea vile vile mpaka kufikia kipindi ambacho rais, Bwana Wou Peng alipoamua kumuita waziri wa Afya, Bwana Zhan na kumtaka kujiuzulu kwa ajili ya maendeleo na amani ya nchi hiyo.

“Nikijiuzulu, watu watataka nifikishwe mahakamani” Bwana Zhan alimwambia rais.

“Hilo usijali. Nitakukingia kifua tu. Hakuna kitu kibaya kitakachotokea” Bwana Wou alimwambia Bwana Zhan.

“Kama itakuwa hivyo, nitafanya hivyo”

Hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa waziri nchini China kujiuzulu kutoka na ubadhilifu wa fedha ambao ulikuwa umefanyika. Wachina wote wakaonekana kuwa na furaha, hawakuamini kama kweli fisadi mkubwa alikuwa amejiuzulu, fisadi ambaye alionekana kuwa kama adui kwa maendeleo ya nchi ya China.

Vyombo vingi vya habari vikaanza kutangaza kuhusiana na kujiuzulu kwake, kila mtu alimwangalia Bwana Zhan kwa jicho la tatu kwani kwa kitendo ambacho alikuwa amekifanya kilionekana kuwa kitendo cha kishujaa sana kwani viongozi wengi nchini China hawakuwa wakitaka kujiuzulu hata mara moja

Maandamano hayakuisha, kujiuzulu kwake hakukumaanisha kwamba maandamano yangemalizika. Kitu ambacho walikuwa wakikitaka ni yeye kujiuzulu lakini katika kipindi hiki walikuwa wamekuja na jambo jipya kabisa, jambo ambalo kila mmoja alitaka lifanyike kwa haraka sana. Katika kipindi hiki, watu wa nchini China walikuwa wakitaka kitu kimoja tu, Bwana Zhan afilisiwe mali zote alizokuwa nazo benki na kisha kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa hukumu kubwa na nzito.

“Anyongwe…Anyongwe…Anyongwe…” Wachina walikuwa wakipiga kelele katika kila maandamano ambayo walikuwa wakiyafanya.

Nyumbani kwake, Bwana Zhan hakuonekana kuwa na furaha, muda wote alikuwa akionekana kuwa na huzuni sana. Kitendo cha wananchi wa China kuandamana kwa kumtaka kujiuzulu kilionekana kumuumiza kupita kawaida. Kuhusu ubadhilifu wa fedha, ni kweli aliufanya kwa nia ya kuendeleza biashara zake mbalimbali ambazo alikuwa akizifanya.

Japokuwa alikuwa waziri nchini China, lakini Bwana Zhan alikuwa akimiliki kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilikuwa kikingia kila siku katika biashara zake mbalimbali. Yeye ndiye ambaye alikuwa akimiliki kiwanda kikubwa cha kutengeneza magari cha Chengdu Motor Industry ambacho kilikuwa kikitengeneza magari ya kifahari. Ukiachana na kiwanda hicho, pia alikuwa akimiliki kiwanda kingine ambacho kilikuwa kinatengeneza viatu vya aina mbalimbali na ndicho ambacho alikuwa amewekeana mkataba na chama cha mpira wa kikapu cha NBA cha nchini Marekani kwa ajili ya kuwauzia viatu.

Bwana Zhan alionekana kuwa msaada mkubwa watu, zaidi ya wafanyakazi milioni moja walikuwa wameajiliwa katika viwanda vyake hivyo. Kila siku Wachina walikuwa wakimpenda lakini kutokana na ubadhilifu ambao alikuwa ameufanya, kila mtu akaonekana kumchukia.

Bwana Zhan alikuwa na mke mmoja, Lucy Liu ambaye katika kipindi hicho alikuwa mjamzito ambaye alikuwa akitakiwa kuwekwa chini ya uangalizi mkubwa katika kipindi hicho kwani muda wowote ule angeweza kushikwa na uchungu na hatimae kujifungua. Kila wakati Bwana Zhan alikuwa akimwangalia mke wake, kila wakati kichwa cha mke wake kilikuwa mapajani mwake, alikuwa akimpenda sana mke wake kuliko mtu yeyote yule, kila alipokuwa akiliangalia tumbo kubwa alilokuwa nalo, alikuwa kitabasamu kila wakati.

“Nimejiuzulu” Bwana Zhan alimwambia mke wake ambaye wala hakuonekana kuwa na furaha kabisa. Lucy hakuongea kitu chochote kile, uso wake ulikuwa ukionekana kuwa na huzuni tu.

“Hii haimaanishi kila kitu kimefikia tamati, bado kuna mambo mengi ya kufanya. Natamani mtoto wetu aje kuwa tajiri mkubwa hapa nchini China kama nilivyokuwa” Bwana Zhan alimwambia mke wake kwa sauti ya unyonge.

“Hii haimaanishi kwamba kila kitu kimekufa kwetu, bado tuna nafasi kubwa mpenzi” Lucy alimwambia mume wake.

“Hiyo ndio ilikuwa maana yangu halisi. Bado tunampenda mtoto wetu atakayezaliwa, sitokuwa radhi ya kufilisiwa. Bado nahitaji kuwa na fedha zote hizo katika akaunti yangu” Bwana Zhan alimwambia mke wake.

“Kuna kitu nimeona”

“Kitu gani?”

“Kwa nini hizi fedha usiziamishe”

“Kwenda wapi?”

“Marekani au Japan”

“Mmmh! Hilo suala ni gumu sana kwani wataweza kugundua kwa haraka sana. Kama nitaamua kuzipeleka katika nchi masikini na ndogo, hapo hakuna tatizo kabisa” Bwana Zhan alimwambia mke wake.

“Kwa hiyo wewe umefikilia nchi gani?”

“Subiri kwanza” Bwana Zhan alisema na kisha kuinuka mahali hapo.

Moja kwa moja akaanza kuelekea chumbani kwake. Bado uso wake haukuwa na furaha hata mara moja, kichwa chake kilikuwa kimejaza mambo mengi kwa wakati huo. Katika kipindi hicho, alikuwa akitaka kufanya kitu kimoja tu, kuzisafirisha fedha zake mpaka katika nchi ambayo angeiona kufaa sana. Baada ya dakika kadhaa, akarudi mahali pale huku akiwa na kompyuta yake ya mapajani.

Akaiwasha na kisha kuunganisha na intaneti. Akaanza kuangalia kila kitu ambacho alikuwa akitaka kuangalia, uso wake ulionyesha umakini mkubwa kupita kawaida. Muda wote huo, mke wake, Lucy alikuwa kimya huku akimwangalia mume wake ambaye macho yake alikuwa ameyaweka katika kioo cha kompyuta yake tu.

“Nimeshapata” Bwana Zhan alimwambia  mke wake, Lucy.

“Wapi?”

“Tanzania. Nchi moja ambayo ipo Afrika” Bwana Zhan alisema.

“Basi hakuna tatizo” Lucy alisema.

Kila kitu mpaka katika kipindi hicho kilikuwa kikienda vizuri kabisa, hakukuwa na mtu ambaye aliona kwamba wangeweza kushindwa katika suala hilo. Baada ya kukubaliana kwa kila kitu, tayari kukawa na tatizo ambalo lilikuwa limetokea. Je fedha hizo zingeweza kusafirishwaje bila wafanyakazi wa benki kuu ya China kugundua? Alijua fika kwamba kama angeingia ndani ya bennki hiyo na kisha kusaini karatasi kadhaa na fedha zile kusafirishwa, watu wangejua kazipeleka nchi gani.

“Kwa hiyo utafanyaje ili asijue mtu?” Lucy alimuuliza mume wake ambaye alikuwa akifikiria mambo mengi.

“Nipe dakika kumi. Nitajua nini cha kufanya” Bwana Zhan alisema.

Kwa haraka haraka bila kupoteza muda akachukua kompyuta yake ya mapajani na kisha kuanza kuangalia baadhi ya vitu kadhaa. Akaandika ‘CRIMINALS IN USA’. Majina ya watu kadhaa ambao walikuwa wamefanya uhalifu mkubwa nchini Marekani yakatokea. Akaanza kumwangalia mmoja baada ya mwingine. Walikuwepo wahalifu ambao waliwahi kuvamia benki na kisha kuiba fedha, walikuwepo wale ambao waliwahi kuiba mamilioni ya fedha pamoja na kuua watu, ila ukiachana na hao, pia walikuwepo wale ambao walikuwa wameiba fedha nyingi kupitia kompyuta ambao walikuwa wamekamatwa.

Bwana Zhan hakuishia hapo, aliendelea zaidi na zaidi mpaka alipokutana na jina la Justin Terry, kijana mwingereza ambaye alikuwa akiishi nchini Marekani, kijana ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni kubwa ya GOOGLE. Huyo ndiye ambaye alikuwa akitaka kuwasiliana nae kwa kuamini kwamba kila kitu kingekuwa kama alivyotaka kiwe.

Hakutaka kuongea nae simuni, alichokuwa akikitaka ni kuongea nae ana kwa ana. Alichokifanya mara baada ya kuwasiliana nae ni kumtaka kuelekea nchini China ambapo huko angeonana nae na kisha kuongea nae juu ya kazi ambayo alikuwa akitaka kumfanyia.

****

Justin Terry. Huyu alikuwa kijana raia wa Uingereza ambaye alikuwa na akili za kuzaliwa. Uwezo wake mkubwa kiakili ndio ambao ulionekana kuwa tatizo kwa walimu wote ambao waliwahi kumfundisha kijana huyu darasani. Kila kitu ambacho alichokuwa akifundishwa alionekana kukijua jambo ambalo lilionekana kuwakasirisha walimu ambao kwake aliwaona kama wanafunzi wake.

Uwezo wake ulikuwa ni wa hali ya juu, walimu hawakutaka kuona wakiambiwa kwamba hapa ulitakiwa kufanya hivi, hivyo walikuwa wakimfukuza darasani. Kila mwalimu alikuwa akiogopa kufundisha mbele ya uwepo wa Terry ambaye kwake alionekana kuwakosoa kupita kawaida. Visa vikaanza mashuleni mpaka pale ambapo Terry akafukuzwa shule.

Hakukuwa na shule ambayo ilikuwa ikimkubali kutokana na kusikia juu ya uwezo wake. Akaanza kuishi nyumbani kwao tu katika jiji la Birmingham. Hakuelekea tena shule, alikuwa akijisomea nyumbani tu. Japokuwa alikuwa nyumbani lakini bado alionekana kufahamu mambo mengi. Katika umri wa miaka kumi na sita, hapo ndipo alipoanza kuwa rafiki mkubwa wa kompyuta, alikuwa akipenda kompyuta kuliko kitu kingine.

Ukaribu wake na kompyuta ndio ambao ulimfanya kufahamu mambo mengi mpaka kugundua njia ambazo mtu alitakiwa kuziibia benki nyingi duniani. Codes zote za benki akaanza kuzifahamu, kitu ambacho alikuwa amekifanya ni kuiba kiasi cha paundi elfu ishirini kutoka katika benki ya Barclays na kuziingiza katika akaunti yake.

Hakukuwa na mtu ambaye alifahamu kama fedha zilikuwa zimeibwa jambo ambalo lilimfanya kuona kwamba alikuwa ameiva katika wizi wa kutumia kompyuta. Alipofikisha miaka kumi na tisa, hakutaka kuishi nchini Uingereza, akaelekea nchini Marekani, huko ndipo alipoanzisha maisha yake. Kila wakati alikuwa na kompyuta yake ya mapajani begini mwake, hakutaka kuiacha, sehemu yoyote ambayo alikuwepo alikuwa akifanya uharifu wa fedha kwa kutumia kompyuta yake.

Alikuwa akiishi kwa ujanja ujanja lakini akafanikiwa kupata fedha nyingi za wizi za zaidi ya dola milioni mbili. Aliendelea na tabia yake hiyo mpaka pale ambapo wapelelezi wa FBI walipokuja kumgundua na kisha kumkamata. Kwao, tayari Terry alionekana kuwa mtu muhimu sana, usingeweza kumfunga jela mtu ambaye alikuwa na uwezo wa namna hiyo. Walichokifanya, wakamuweka katika kitengo hicho cha upelelezi akiwafanyia kazi zao kwa malipo makubwa mpaka pale ambapo kampuni kubwa ya GOOGLE ilipoamua kumchukua kwa malipo makubwa kwa kuwafanyia kazi kubwa zilizotakiwa kufanywa na yeye.

Kwa sasa alikuwa akifahamu mengi sana japokuwa hakutaka tena kuiba. Alikuwa akimiliki kiasi kikubwa cha fedha, alikuwa na uwezo mkubwa wa kumuibia mtu yeyote kiasi chochote cha fedha na kukipeleka kwenye akaunti yoyote duniani bila mtu yeyote kufahamu. Huyo ndiye alikuwa Terry, kijana ambaye alikuwa akihitajika na Bwana Zhen kwa ajili ya kuzisafirisha fedha zake katika benki kuu ya Tanzania bila serikali ya China kufahamu fedha zake zilikuwa zimesafirishiwa wapi. Katika kila kitu ambacho Bwana Zhan alikuwa akikifanya, alikuwa akifanya kwa ajili ya mtoto wake ambaye alitarajiwa kuzaliwa, mtoto ambaye alimuona kuwa kila kitu kwake.

“Nimekwishafika” Terry alimwambia Bwana Zhan simuni na kisha kumuelekeza kuelekea hotelini, huko ndipo ambapo wakakutana na kisha kuanza mazungumzo.

“Kazi rahisi sana hiyo. Tena kwa sababu una namba zako za siri, zoezi rahisi sana. Ila itakubidi uongee na hata rais wa nchi hiyo ili akaunti yako iwe salama”

“Hilo si tatizo. Kila kitu tayari, nimekwishaongea nae na ni wewe tu ndiye nilikuwa nakusubiria” Bwana Zhan alimwambia Terry.

“Hakuna tatizo. Kiasi changu cha dola milioni moja nitakiingiza kwenye akaunti yangu kama malipo”

“Hilo si tatizo”

“Basi sawa. Ndani ya dakika tano tu kazi yako itakuwa tayari”

“Dakika tano?” Bwana Zhan aliuliza huku akionekana kushtuka.

“Yeah! Tena hapo nimechelewa. Huwa ninafanya kwa dakika moja tu. Zimekuwa tano kwa sababu nataka kuziiba codes za benki ya huko na hii benki ya hapa China” Terry alimwambia.

“Hakuna tatizo”

“Poa” Terry alisema na kisha kuchukua kompyuta yake ya mapajani na kisha kuanza kazi yake.

****

Joshua alikuwa akitetemeka kupita kawaida, hakuamini kwamba mtu ambaye alikuwa akimhofia ndiye ambaye alikuwa mbele yake kwa wakati huo. Alibaki akiwa amesimama huku simu yake ikiwa sikioni mwake, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati huo, akabaki kimya kwa muda.

“Wewe kijana” Bwana Shedrack alimuita Joshua, katika kipindi ambacho akataka kuitikia, simu ambayo alikuwa amepiga ikapokelewa. Alichokifanya ni kumuomba radhi Bwana Shedrack kwa ajili ya kuongea na simu mara moja.

“Ebwana nimefika mpaka hapa ila nimekuta mlango umefungwa na Joshua hayupo. Nadhani bado hajarudi kutoka Mbezi, sasa tufanye nini manake bila huyu jamaa hata spika zetu za rusha roho hatutoweza kuzipata muda muafaka” Joshua alisema na kuendelea huku Bwana Shedrack akiwa mbele yake.

“Ok! Basi cha msingi tufanye hivi nirudi baadae kwa sababu mtu mwenyewe kashaonekana kuzingua. Yeah! Ndio hivyo bosi, cha msingi sisi tupate spika zetu tu” Joshua alisema huku kadri alivyokuwa akiongea, mwili wake ulikuwa ukipoa. Alipomaliza, akakata simu na kuizima kwa kuona mtu ambaye alikuwa amempigia na kumwambia habari zisizoeleweka angeweza kumpigia.

“Samahani mzee. Nikusaidie nini?” Joshua alimuuliza Bwana Shedrack.

“Wewe unaishi humu?”

“Hapana. Nimekuja kumuulizia Dj Joshua kwa ajili ya kuchukua spika zetu ila bahati mbaya nimemkosa” Joshua alidanganya.

“Ila unamjua?”

“Ndio”

“Sawa. Ukimuona mwambie namtafuta. Nataka nimuue tu” Bwana Shedrack alisema huku akionekana kuwa na hasira.

“Nimwambie anatafutwa na nani?”

“Bwana Shedrack”

“Sawa” joshua alijibu na kisha Bwana Shedrack kuondoka mahali hapo huku tayari suruali ya Joshua ikiwa imeloa kwenye zipu.

****

Njia nzima Rose alikuwa na mawazo, hakuamini kama ule ndio ulikuwa mwisho wa kukaa nyumbani kwao. Hakutaka kurudi tena, hakutaka kuwasiliana na ndugu yeyote yule kutoka nyumbani kwao, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuondoka na kwenda kuishi mbali. Bado alikuwa akifikiria mengi, hasa kutokana na ujauzito ambao alikuwa nao katika kipindi hicho, haukuonekana kuwa sababu ya yeye kuendelea kuishi ndani ya nyumba ile.

Leo baba yake alikuwa ameamua kwenda kumuua Irene, ile ilimaanisha kwamba ingewezekana siku nyingine kuamua kumuua hata yeye mwenyewe. Alitaka kuwa makini kwa kila hatua ambayo ilikuwa inatokea, alitakiwa kuwa makini kwa kila kitu ambacho alitakiwa kukifanya.

Ndani ya jiji la Dar es Salaam alikuwa na ndugu wengi lakini katika kipindi hicho aliona asingeweza kwenda kwa ndugu yeyote yule zaidi ya Irene ambaye nae alionekana kuwa adui wa familia yake. Safari bado ilikuwa ikiendelea kuelekea Sinza Makaburini, katika kipindi hicho alikuwa akitaka kuonana na msichana Irene na kumwambia kwamba alikuwa ameamua kuondoka nyumbani kwao.

Safari wala haikuwa ndefu sana, wakafika Sinza Makaburini ambapo akamlipa dereva bajaji kiasi cha fedha alichokuwa akikihitaji na kisha kuanza kuifuata jengo la hosteli ile, alipolifikia akafungua geti na kuingia ndani. Wasichana wengi walikuwepo ndani ya eneo lile wakifua wengine wakiwa na mataulo wakielekea bafuni kuoga.

“Samahani. Irene nimemkuta?” Rose alimuuliza dada mmoja ambaye alikuwa akifua.

“Irene yupi?” Msichana yule aliuliza.

”Irene Godfrey”

“Mmmh! Sijui. Nenda katika chumba chake ukamuulizie” msichana yule alimwambia Rose

“Chumba chake kipo wapi?” Rose aliuliza.

Hapo ndipo ambapo yule msichana alipoanza kumuelekeza Rose chumba cha Irene kilipokuwa na kisha Rose kuanza kupiga hatua kuelekea alipoelekezwa. Alipoufikia mlango, akaanza kupiga hodi na kisha kufunguliwa. Wasichana kadhaa walikuwa ndani ya chumba hicho wakijiandaa kuelekea vyuoni.

“Samahani” Rose alisema mara baada ya salamu.

“Karibu” Msichana mmoja alimwambia Rose.

“Irene nimemkuta?”

“Hayupo”

“Kaelekea wapi?”

“Aliondoka toka jana. Hakutuaga. Ila si umpigie simu” Msichana yule alimwambia Rose.

Hapo hapo Rose akachukua simu yake na kisha kuanza kumpigia Irene, simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya kichovu ya Irene kuanza kusikika. Waliongea kwa dakika kadhaa, Rose akatakiwa kuelekea Mwananyamala A alipokuwa Irene. Rose hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuaga na kisha kuondoka mahali hapo. Alipofika nje, akakodi bajaji na kuondoka.

Safari ya kuelekea Mwananyamala A ikaanza , mpaka pale ambapo alipofika Mwananjamala A na kumuona Irene ambaye alikuwa akimsubiri. Wakakumbatiana kwa furaha na kisha kuanza kuondoka mahali hapo. Safari hiyo ikaishia katika chumba cha Asha, chumba ambacho kilionekana kukaliwa na mtu msela kutokana na mpangilio wake kutokuwa wa kuvutia.

“Imekuwaje tena?” Irene alimuuliza Rose.

“Nilikimbia nyumbani. Nilihofia kwamba kama baba amegundua nimekupigia simu, hasira zake zingeishia kwangu” Rose alimwambia Irene.

“Pole sana. Kwa hiyo hautorudi tena?”

“Siwezi kurudi”

“Dah! Haina jinsi. Ngoja nikufanyie mishemishe ya mjini hapa ukakae katika chumba kimoja nilipanga hapo Kinondoni ila sijakitumia sana na kuhamia hosteli. Kama miezi sita imebaki mpaka kodi kumalizika. Unaonaje? Au utashindwa kukaa peke yako?” Irene alimwambia Rose.

“Hakuna tatizo” Rose alijibu.

Irene hakutaka kuchelewa sana, akaoga na kisha wote kwa pamoja kuanza safari ya kuelekea Kinondoni na kisha kuelekea katika chumba hicho. Walipofika, wakaingia ndani na kisha kuanza kukifanyia usafi kutokana na fumbi kuwa jingi ndani ya chumba hicho.

Chumba kilionekana kuwa kikubwa, kilikuwa na kila kitu, makochi makubwa, kitanda pamoja na jiko la gesi bila kusahau televisheni ambayo ilikuwa katika stendi yake. Kwa kiasi fulani, chumba kile kilionekana kumvutia Rose ambaye akaridhika kwa moyo mmoja kukaa ndani ya chumba kile.

Hapo ndipo ambapo Rose akaanza maisha, mara kwa mara Irene alikuwa akifika hali hapo kwa ajili ya kumuona na pia kumfanyia usagaji. Katika kipindi hiki Rose akaonekana kubadilika sana, hakutaka kufanyiwa mchezo wa usagaji, alikuwa amekwishaamua kwamba alikuwa ameuacha mchezo huo kwa sababu tu alikuwa mjauzito katika kipindi hicho.

Irene alibaki kumshangaa, hakuamini kama kulikuwa na msichana ambaye alikuwa akiufanya mchezo ule na kisha kubadilika na kuamua kuuacha kabisa. Hilo likaonekana kuwa tatizo kwa Irene, mara kwa mara alikuwa amimshawishi Rose lakini wala hakuonekana kukubaliana nae, alikuwa ameamua kubadilika kwa asilimia mia moja.

Irene hakuonekana kufahamu kile ambacho kilikuwa kikiendelea kwa Rose, hakufahamu kama binti huyo katika kipindi hicho alikuwa mjauzito. Kwake, alimuona kuwa msichana wa kawaida sana ambaye wala hakuwa na kiumbe chochote tumboni mwake.

“Kwa nini lakini mpenzi?” Irene alimuuliza Rose kwa sauti ya unyonge.

“Hapana. Nimeamua tu” Rose alijibu.

“Hakuna mtu anayeamua kitu bila sababu. Kutakuwa na sababu tu”

“Nina mimba. Hiyo ndio sababu yenyewe” Rose alitoa jibu liliomfanya Irene kushtuka.

“Una mimba? Ya nani? Imekuwaje tena?” Irene aliuliza huku akionekana kushtuka.

“Nimepata mimba Irene”

“Kivipi.Kiungo wa bandia umekupa mimba?”

“Hapana. Nimepewa mimba na Joshua” Rose alijibu.

Hapo ndipo ambapo Rose akaamua kumhadithia Irene kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake katika kipindi ambacho alikuwa nyumbani. Ile ikaonekana kuwa stori mbaya kwa Irene ambaye alikuwa makini akimsikiliza tu. Hakukuwa na kitu kilichobadilisha ukweli katika kipindi hicho, Rose alikuwa mjauzito na kwa mbali tumbo lilikwishaanza kuonekana.

“Kwa hiyo ndio basi tena?” Irene aliuliza kwa sauti ya upole.

“Haina jinsi. Itabidi iwe hivyo” Rose alijibu.

“Sasa itakuwaje kwa Peter ambaye anaamini mimba ni yake?”

“Bado sijajua. Sitaki kufikiria hilo kwa sasa. Acha nifanye mambo yangu kwanza” Rose alimwambia Irene.

****

Terry alikuwa kimya huku akiifanya kazi yake ambayo aliambiwa aifanye katika kipindi hicho. Aliambiwa azitoe fedha zote na kubakisha kiasi cha dola milioni mbili ambazo hizo zingebaki na kisha Bwana Zhan kufanyia mambo yake. Kama alivyosema, zoezi wala halikuwa kubwa, ni ndani ya dakika nne tu tayari zoezi zima lilkuwa limekamilika.

Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwa Bwana Zhan ambaye akaamua kula chakula cha mchana na Terry na kisha kumfanyia mipango ya usafiri wa ndege kwa ajili ya kurudi nchini Marekani huku akitaka kila kitu kiwe siri yao na asiambiwe mtu yeyote, kwa maana hiyo siri ingekuwa kwa Bwana Zhan, Terry pamoja na mke wa Bwana Zhan, Lucy.

Bado kulikuwa na mambo mengi ya kufanya kwa wakati huo, bado aliona kwamba kulikuwa na kitu kimoja ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati huo, kutoroka na kuelekea nchini Tanzania bila kugundulika. Hiyo haikuonekana kuwa rahisi kufanyika, alitakiwa afanye kitu kitu kimoja ambacho kingemfanya kutokujulikana na mtu yeyote kama alikuwa yeye.

Wazo moja likamjia kichwani, wazo lile likaonekana kustahili sana kuchukuliwa hatua, kwa moyo mmoja, akaamua kutengeneza sura za bandia ambayo angeitumia kusafiria mpaka nchini Tanzania pamoja na mke wake. Kwa haraka bila kupoteza muda akaanza kuwasiliana na wachongaji wa sura za bandia na ndani ya masaa mawili walikuwa ndani ya nyumba hiyo na kisha kuanza kuwapa maelekezo juu ya nini kilitakiwa kufanyika mahali hapo.

Kiasi kikubwa cha fedha kilihitajika kwa ajili ya kukamilisha kila kitu ambacho alikuwa akitaka kifanyike na ndani ya siku mbili, tayari sura mbili za bandia zilikuwa zimekwishakamilika. Mpaka hapo kila kitu kilikuwa tayari na walipanga kwamba siku itakayofuatia ndio ilikuwa siku ya kuondoka nchini hapo na kuelekea nchini Tanzania. Usiku wakalala kitandani kwao huku sura za bandia zikiwa pembeni ili ikifika asubuhi wazivae na kisha kuanza kuitoroka nchi ya China.

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane kesho hapahapa.

Leave A Reply