The House of Favourite Newspapers

Kahaba Kutoka China-10

0

Wachina bado walionekana kuwa na hasira kupita kawaida, kila siku hitaji lao liliendelea kuwa lile lile, Bwana Zhan afikishwe mahakamani. Kwa sababu Bwana Zhan alikuwa swahiba mkubwa wa rais Bwana Wou jambo lile likaonekana kuwa gumu sana kufanyika na kama lingefanyika basi Bwana Zhan angeshinda kila kitu na hivyo kuwekwa huru.

Wachina walikuwa wamekwishalijua hilo na kwa sasa walitaka kufanya kitu kimoja tu, kumuua Bwana Zhan na familia yake kama njia ya mkato kwa ajili ya kuirudisha furaha yao ambayo ilikuwa imeingia doa kutokana na kitendo cha Bwana Zhan kuchukua fedha za wananchi, fedha ambazo zilitakiwa kusaidia idara mbalimbali.

Wachina mia moja, wanaume ambao walikuwa na nguvu na hasira wakajikusanya kwa lengo moja tu, kuvamia nyumba ya Bwana Zhan na kisha kumuua na familia yake. Kila mmoja alikuwa na silaha, kila mmoja alikuwa akitaka kufanikisha kile ambacho walikuwa wakitaka kufanikisha kwa wakati huo. Kilichofanyika, usiku wa saa sita wakaanza kuelekea katika mtaa wa Yungshai, mtaa uliokuwa ukikaliwa na matajiri kwa lengo la kuiteketeza familia ya Bwana Zhan.

Kila mmoja alikuwa na silaha mikononi mwao na walikuwa wakitaka kufanya kitu kimoya kimya. Walipofika katika geti la kuingilia ndani ya nyumba ile, kitu cha kwanza wakawaweka chini ya ulinzi walinzi ambao walikuwa mahali hapo na kisha kwenda kuzitoa kamera ambazo zilikuwa zimezunguka nyumba hiyo na kisha kuanza kuelekea ndani.

Mlango ulikuwa ukifunguliwa kwa alama za vidole vya wahusika wa nyumba ile lakini kwa sababu nao walikuwa wamejiandaa vilivyo, vijana ambao walikuwa wazoefu katika kuchezea kompyuta walikuwa pamoja nao. Kwa haraka kijana mmoja akaanza kuufuata mlango, akachukua kompyuta yake ndogo ya mapajani na kisha kuuchukua waya, akaifungua mashine ile na kuanza kuchezea kwenye kompyuta yake. Wala haikuchukua muda mrefu, akakipeleka kidole chake katika mlango ule na kisha mlango kufunguka, kilichofuatia, vijana kumi wakaanza kuingia ndani ya nyumba ile.

Kila mmoja aliyeingia ndani ya nyumba ile alikuwa na lengo moja tu kichwani mwake, kumuua Bwana Zhan pamoja na mkewe. Vijana wawili wakabaki pale sebuleni na wengine kuelekea katika sehemu kulipokuwa na chumba cha Bwana Zhan na kisha kutaka kuufungua mlango. Mlango ukaonekana kuwa mgumu kukufunguka, wakajaribu kukitekenya kitasa lakini wala haukuweza kufungua jambo ambalo likawafanya kuanza kuupiga teke mlango ambao ukaachia na kuwa wazi.

Wakaingia ndani ya nyumba ile, ni Bwana Zhan peke yake ndiye alikuwepo ndani ya chumba kile. Walichokifanya, hawakutaka kuuliza nini wala nini, wakaanza kumshambulia kwa hasira na ndani ya dakika moja tu, Bwana Zhan akatulia sakafuni, damu zilikuwa zimetapakaa sakafuni pale, alikuwa amekwishakata roho.

“Mkewe!” Kijana mmoja alisema.

“Yupo wapi?”

“Sijui. Au kajificha?”

“Sijui yupo wapi

Vijana wale wakaanza kumtafuta Lucy, wakaanza kuingia katika kila chumba. Wafanyakazi wote wa ndani ambao walikutwa ndani ya vyumba vingine wakawekwa chini ya ulinzi huku wakiamriwa kutopiga kelele. Walitafuta katika kila kona ndani ya nyumba ile lakini Lucy hakuonekana kabisa jambo ambalo lilionekana kumshangaza kila mtu.

“Inawezekana kwamba hakulala ndani ya nyumba hii?” Kijana mmoja aliuliza.

“Haiwezekani hata kidogo”

“Sasa yupo wapi?”

“Mmmh! Sijui. Tusingekuwa tumemuua yule mzee angetuambia tu”

“Kwa hiyo tufanye nini?”

“Tuondokeni”

“Tuondoke bila kumuua mke wake?’

“Yeah! Haina jinsi”

“Sawa”

Vijana wale waliongea na kushauriana. Katika kipindi hicho hawakutakiwa kubaki sana ndani ya nyumba ile, kwa sababu walikuwa wamemkosa Lucy, wote kwa pamoja wakashauriana kuondoka ndani ya nyumba ile bila ya kufanikisha zoezi la kumuua Lucy. Wakatoka nje ya nyumba ile, wakawafunga kamba walinzi na kisha wao kuondoka.

Asubuhi, vyombo vya habari vikaanza kutangaza kuhusiana na mauaji ya Bwana Zhan. Hakukuwa na mtu ambaye alihuzunika, kila mmoja alikuwa akifurahi, taarifa ile kwao ikaonekana kuwa njema, hawakuwapenda kabisa mafisadi, watu ambao walikuwa wakiyatumia madaraka kwa ajili ya kujinufaisha wao na familia zao.

Swali moja ndio ambalo lilibaki, mke wake alikuwa wapi? Hakukuwa na mtu aliyekuwa akilijua jibu la swali lile. Waliulizwa walinzi, hawakuwa wakifahamu, wakaulizwa wafanyakazi wa ndani lakini nao jibu lilikuwa lile lile, hawakuwa kifahamu pia. Kila mmoja akaonekana kuchanganyikiwa, kifo cha Bwana Zhan kilionekana kuwafurahisha lakini bila Lucy kuuawa kilionekana kuwakasirisha, yaani kwao walifananisha na kuukata mti na kisha kuubakisha mzizi, mzizi ule uliobaki ungeweza hata kuuleta mti mwingine, mti ambao ungekuwa kama ule uliokatwa na hivyo kuonekana kutofanya kitu chochote kile.

****

Bwana Zhan alikuwa chumbani pamoja na mke wake, muda mwingi alikuwa akiifikiria safari yao ya kuelekea nchini Tanzania. Kila kitu ambacho walikuwa wakikitaka walikuwa wamekwishakipata na wala kusingekuwa na tatizo lolote kuhusiana na safari yao ya kuelekea nchini Tanzania. Kama ni fedha, tayari zilikuwa zimekwishatumwa nchini Tanzania kwa ajili ya kuendelea na maisha yao mara baada ya kufika ndani ya nchi hiyo.

Usiku kwao ukaonekana kuwa mrefu, mioyo yao ilikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba kulikuwa na uwezekano wa Wachina kufanya jambo lolote lile baya kama tu wangeendelea kubaki nchini hapo. Ilipofika usiku wa sita usiku, Bwana Zhan akaonekana kuhisi kitu, hata kabla hajafanya kitu chochote kile akaanza kuifuata kompyuta yake iliyokuwa mezani na kisha kuiwasha.

Akaanza kuziangalia kamera zake ambazo alikuwa amezitegesha katika maeneo mbalimbali ndani ya nyumba ile. Zile kamera ambazo zilikuwa nje, hazikuwa zikionyesha chochote kile kitu kilichomfanya kugundua kwamba zilikuwa zimetolewa. Hapo ndipo ambapo akashikwa zaidi na hofu moyoni mwake. Akaendelea kuziangalia kamera nyingine hasa zile zilizokuwa sebuleni na maeneo mengi, kamera za sebuleni zikawaonyesha watu fulani wakiingia sebuleni pale.

Alichokifanya ni kumuamsha mke wake, akachukua sura ya bandia na kisha kumtaka kuivaa. Lucy hakuelewa sababu iliyompelekea mume wake kufanya jambo lile huku akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa mno, alichotakiwa kukifanya ndicho ambacho alikifanya bila kuonyesha mgomo wowote ule. Alipoona kwamba tayari mke wake alikuwa amekwishaivaa ile sura ya bandia, hapo ndipo akaitoa picha moja aliyoibandika ukutani na kisha macho yake kutua katika kitufe ambacho alikifungua na kukibonyeza. Sakafu ya chini ikajifungua na kisha kumwambia Lucy aingie.

“Ondoka” Bwana Zhan alimwambia Lucy.

“Niende wapi?”

“Popote pale ila ondoka”

“Vipi kuhusu wewe mpenzi?”

“Nabaki. Ngoja nibaki. Usiwe na wasiwasi na mimi” Bwana Zhan alimwambia Lucy huku tayari wakianza kusikika kitasa kikianza kutekenywa na mtu wa nje ambaye alikuwa akitaka kuufungua mlango.

“Chukua hii kadi. Hii kadi ni akaunti yangu ya benki, utakuwa ukichukua fedha kwa ajili ya kukusaidia na pia chukua hii karatasi, humu kuna namba ya Terry, utawasiliana nae baada ya wiki moja ili kujua ni kwa namna gani atakupa kadi ya kukuruhusu kuchukua fedha nchini Tanzania” Bwana Zhan alimwambia Lucy ambaye akaanza kutokwa na machozi.

“Vipi kuhusu wewe?” Lucy aliuliza huku akilia.

“Acha nife. Nimefanya jambo moja kubwa sana kwa watu wa China. Acha nife mke wangu ili wafurahi” bwana Zhan alimwambia Lucy na kisha kumkumbatia.

Lilikuwa ni kumbatio lenye huzuni kupita kawaida, wote kwa pamoja walikuwa wakitokwa na machozi, kila mmoja alijua fika kwamba huo ndio ungekuwa mwisho wa wao wawili kuonana maishani mwao. Walitumia muda wa sekunde kadhaa na kisha kuachiana, Bwana Zhan akambusu Lucy shavuni na kisha kumwambia aondoke mahali pale.

“Usikose kumwambia mtoto wangu kila kilichotokea” Bwana Zhan alimwambia Lucy.

“Nitamwambia…nitamuelezea kila kitu” Lucy alimwambia mume wake na kisha kuanza kuteremka chini.

“Dokta alisema ni wa kike au wa kiume?” Bwana Zhan alimuuliza Lucy.

“Wa kiume”

“Sawa. Mpe jina la Lee endapo ukijifungua salama”

“Nitafanya hivyo” Lucy alisema na kisha Bwana Zhan kuufunga mlango ule wa kuelekea chini.

Lucy alikuwa akikimbia huku akilia, ndani ya bomba lile hakukuwa na usafi wowote ule, uchafu mwingi ulikuwa mahali kule, maji machafu na yanayonuka yalikuwa yakiendelea kumwagika ndani ya bomba lile kubwa ambalo hata ukisimama, bado lilikuwa kubwa.

Lucy alikuwa akitembea zaidi na zaidi kuelekea lilipokuwa likielekea bomba lile. Macho yake yalikuwa mekundu sana huku mashavu yake yakiendelea kuchirizikwa na machozi yaliyokuwa yakimtoka mfululizo. Safari ndani ya bomba lile kubwa haikuwa ndogo, alikuwa akiendelea na safari mpaka baada ya masaa matano ndipo alipotokea katika bahari kubwa, bahari ya Njano ambayo ipo upande wa Mashariki nchini China, bahari ambayo kama ungesonga nayo zaidi, ungeweza kuingia katika bahari nyingine iitwayo Bahari ya Mashariki ya China.

Mara baadaya kutokea katika bahari hiyo, Lucy akatoka na kuanza kutembea pembezoni mwa bahari ile huku usoni akiwa amevaa sura ya bandia ambayo alikuwa amepewa na mume wake. Katika kipindi hicho, Lucy alionekana kuwa tofauti kabisa, sura ambayo alikuwa ameivaa kusingekuwa na mtu ambaye angeweza kumgundua kabisa.

Alitembea pembezoni mwa bahari ile mpaka alipotokea katika sehemu iliyokuwa na hoteli kubwa, hakutaka kukaa ndani ya hoteli hiyo bali alikuwa akiitumia njia hiyo ya hoteli kutokea nyuma mpaka pale alipoingia barabarani. Kichwani kwake kwa wakati huo alikuwa akitaka kuelekea Dongying, sehemu ambayo ilikuwa ni kijiji kikubwa, kijiji ambacho kilikuwa kilometa mia tatu kutoka katika jiji la Beijing.

Alichokifanya Lucy ni kuchukua basi kubwa la abiria ambalo lilikuwa likielekea Dongying ambapo huko angeanza maisha mapya kwa kuona kwamba hata kama alikuwa na sura ya bandia, hasingeweza kuishi ndani ya jiji la Beijing. Safari ile ilichukua masaa mawili, akafika katika kijiji hicho ambapo akateremka na kuanza kuelekea katika sehemu ambazo zilikuwa na nyumba nyingi.

Alichokifanya Lucy ni kuulizia sehemu kulipokuwa na nyumba ya mwenyekiti wa kijiji hicho, Bwana Sheng Lou kwa ajili ya kutaka kuzungumza nae mambo machache. Vijana ambao alikuwa amewauliza ndio ambao wakampeleka mpaka katika nyumba ya mwenyekiti wa kijiji hicho na kisha kuanza kuongea nae.

“Mumeo amefariki?” Bwana Lou aliuliza..

“Ndio” Alifariki katika lile tetemeko la ardhi lililotokea Shangdon katika ule mgodi wa dhahabu” Lucy alidanganya.

“Sawa. Kwa hiyo nikusaidie nini?”

“Nimekuja kutafuta kazi. Maisha yangu ni ya kimasikini sana, nimekuja kuomba kazi ili nipate fedha za kumlea mtoto wangu atakayezaliwa”

“unaweza kulima?” Mzee Lou alimuuliza.

“Nitaweza tu”

“Hakuna tatizo. Huwa tunawasaidia watu mbalimbali kijijini hapa, tunapenda watu” Mzee Lou alimwambia.

Kuanzia siku hiyo Lucy akaanza kukaa ndani ya kijiji hicho, kila siku alikuwa akielekea shambani kulima pamoja na wanawake wengine. Kwake, maisha hayakuonekana kuwa rahisi hata kidogo, hakuzoea kulima hata mara moja lakini katika kipindi hicho hakuwa na jinsi, alitakiwa kulima huku akivuta muda wa kujifungua na kisha kuanza safari ya kuelekea nchini tanzania.

Baada ya wiki mbili, akaanza kuwasiliana na Terry ambaye akamtumia kadi yake ya benki ambayo alitakiwa kuitumia nchini Tanzania. Katika kipindi hicho DHL ndio ilionekana kukamilisha kila kitu Mizigo yote ambayo alikuwa akiitaka kuipata kutoka nchini Marekani alikuwa akiipata bila wasiwasi wowote ule.

Kazi zilikuwa zikiendelea kama kawaida kijijini hapo, wanawake wengi walikuwa wakifanya kazi kwa kujitoa. Hakukuwa na mtu ambaye alijua kwamba msichana ambaye alijitambulisha kwa jina la Lanfen alikuwa Lucy, mke wa marehemu Zhan ambaye alikuwa ameuawa katika kifo cha kinyama, mtu ambaye alikuwa akichukiwa sana na wachina.

Siku zikaendelea kukatika mpaka katika siku ile ambayo Lucy akashikwa na uchungu. Hakupelekwa hospitalini zaidi ya kujifungua kupitia kwa wakunga wanawake ambao walikuwa wakizifanya kazi zile vizuri tena bila wasiwasi wowote ule. Mtoto wa kiume akazaliwa na kupewa jina la Lee, jina ambalo baba yake alitaka mtoto huyo apewe.

Lee akaonekana kuwa kila kitu kwa mama yake, lee akaonekana kuwa mtu wa thamani sana kwa mama yake, Lucy. Kila wakati alikuwa pamoja nae, alikuwa akimjali kupita kawaida. Muda mwingi alipokuwa akimwangalia lee alikuwa akitokwa na machozi, maisha ambayo lee alikuwa akiyaishi ndani ya kijiji kile yalionekana kuwa maisha ambayo hakutakiwa kuyaishi kabisa kutokana na fedha ambazo alikuwa nazo.

Mwaka wa kwanza ukapita, mwaka wa pili ukaingia na hatimae mwaka wa tatu kuingia. Lucy hakutaka tena kuishi ndani ya kijiji hicho, alichokifanya ni kuaga kwamba alikuwa akielekea mjini kwa ajili ya kutafuta maisha zaidi. Hakuzuiliwa na mzee Lou zaidi ya kutakiwa kuwa makini, akaondoka zake.

Alipofika Beijing akaanza kufanya mishemishe za kutaka kuja nchini tanzania. Kwanza kabisa akaanzisha kampuni yake ya ujenzi ambayo akaambiwa achague nchi ya kufanyia kazi, akachagua nchi ya tanzania. Kama ilivyokuwa kwa wachina wengine, serikali ikamuunga mkono kwa kila kitu, ikamgawia kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kumsadia kwani serikali ilikuwa ikitaka watu wake watawanyike dunia nzima kwa ajili ya kufanya mambo mengi.

Pamoja na hayo, serikali ikamwandalia wafanyakazi kadhaa kwa ajili ya kumuunga mkono kwa kile ambacho alikuwa akitakiwa kukifanya. Mpaka miezi miwili inakatika, na kwa kutumia kiasi kilichobaki katika akaunti ya mume wake, akaanza safari ya kuelekea nchini Tanzania huku wachina wakiendelea kumtafuta kwani nae alitakiwa kuuawa pia.

Alipofika nchini tanzania, akatafuta nyumba na kisha kuanza kuishi pamoja na mtoto wake. Kwa sababu alikwishaitaarifu serikali ya Tanzania juu ya ujio wake, akapewa tenda ya kutengeneza ghorofa kubwa Posta Mpya, ghorofa la McFee ambalo lipo karibu na jengo la kampuni ya TTCL.

Lucy hakutaka kuchelewa, kwa sababu kampuni yake ilikuwa na makarani wakubwa na wenye uwezo mkubwa akaipokea tenda hiyo kwa mikono miwili na hatimae baada ya miezi miwili kazi kuanza mahali hapo. Makarani hao ndio ambao walikuwa wakisimamia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo huku makubaliano ya malipo ya fedha yakiwa yamekwishaanza kufanyika.
Mpaka kufika katika kipindi hicho, hakutoa kiasi chochote cha fedha kutoka mfukoni mwake, serikali ya China ndio ambayo ilikuwa ikilipia kila kitu ambacho kilikuwa kikifanyika likiwa pamoja na suala la kuwalipa wafanyakazi waliokuwa wakibeba matofali na hata kunyanyua vyuma.
Wakinamama mbalimbali wakaanza kukusanyika katika eneo la ghorofa hilo ambalo lilikuwa likiendelea na ujenzi kama kawaida, wakinamama hao walikuwa na kazi moja tu mahali hapo, kuuza vyakula kwa wafanyakazi ambao walikuwa wakiendelea kufanya kazi ya ujenzi katika ghorofa lile ambalo lilikuwa likiendelea kwa kasi sana.
Kati ya wakinamama wote ambao walikuwa wakifanya biashara mahali hapo, kuna msichana mmoja ndiye ambaye alikuwa akisifika sana kutokana na chakula chake kuwa kitamu. Wafanyakazi wengi walikuwa wakila kwake, alionekana kujua kupika sana huku mara nyingi akitumia hata viungo vya kichina jambo ambalo liliwafanya hata wachina akiwepo Lucy kula chakula chake.
Chakula chake kilikuwa maarufu sana mahali hapo hata zaidi ya yeye mwenyewe. Kila siku alikuwa akiingiza fedha huku kimuonekano akionekana kuwa mwanamke mjamzito ambaye wala hakuwa na muda mwingi kabla ya kujifungua. Baada ya wiki kadhaa, mwanamke yule hakuonekana tena mahali pale jambo ambalo kila mtu akajua kwamba katika kipindi hicho alikuwa akikaribia kujifungua.

Je, nini kitaendelea?

Tukutane kesho hapahapa.

Leave A Reply