The House of Favourite Newspapers

Kahaba Kutoka China-13

0

Katika kipindi cha kwanza Peter aliona kazi aliyopewa ya kumteka Irene na kisha kumpeleka sehemu husika kuwa kazi rahisi sana kwa kuona kwamba angetumia kiasi fulani cha fedha na hatimae msichana huyo kuingia ndani ya himaya yake. Kitu ambacho alikiamini ni kwamba asilimia kubwa ya wanawake walikuwa wakizitamani sana fedha na walikuwa tayari kukaa meza moja na mtu wasiyemfahamu kwa sababu ya fedha, walikuwa tayari kulala na mtu wasiyemfahamu kwa sababu ya fedha tu.

Katika fedha, hicho ndicho kitu ambacho Peter alikuwa akiamini kwamba angeweza kufanikisha kile ambacho alikuwa amekipanga kwa wakati huo. Ila wazo lake likaonekana kubadilika ghafla, wepesi wa kufanya jambo lile ukatoweka na kumjia ugumu wa kutekeleza jambo lile hasa mara baada ya kuambiwa kwamba Irene alikuwa msagaji. Kwa maana hiyo ilimaanisha kwamba Irene hakuwa mwepesi kukamatika kutokana na wanawake wengi wa aina hiyo kutukupenelea kukaa pamoja na wanaume.

Hilo tayari likaonekana kuwa tatizo kwake, hakujua ni kwa staili gani ambayo alitakiwa kuifanya na hatimae kutimiza lile ambalo alikuwa ameambiwa alitimize kwa wakati muafaka. Kwa msagaji, hakuwa akipenda kukaa na wanaume, mara kwa mara alikuwa akipenda kukaa na wanawake wenzake. Hiyo tayari ikamfanya Peter aanze kufikiria kitu kingine zaidi kwamba ili kumteka Irene ilimpasa kumtumia msichana.

Kuhusu kumpata msichana wala halikuwa tatizo kubwa sana, alichokifanya usiku wa siku hiyo ni kuelekea mpaka katika Ambiance, sehemu ambayo wanawake wengi walikuwa wakijiuza na kisha kulisimamisha gari lake kando kabisa ya barabara katika upande unaoelekea Shekilango. Baadhi ya wanawake ambao waliliona gari lile wakaanza kulisogelea kwa karibu kwani kila mmoja aliamini kwamba mtu aliyekuwa ndani ya gari hilo alikuwa mmoja wa wateja ambao walikuwa wakihitaji wanawake wa kulala nao usiku.

Alichokifanya Peter ni kushusha kioo cha mbele cha gari lake na kisha kuanza kuwaangalia wasichana wale mmoja baada ya mwingine, kila msichana alikuwa akijigeuza huku na kule kama njia mojawapo ya kumvutia mteja wao ambaye waliamini kwamba ilikuwa ni lazima kuondoka na mmoja au wawili.

“Namhitaji huyo white” Peter alisema.

“Mimi?”

“Hapana. Huyo aliyevaa sketi fupi. Amenivutia” Peter alisema na hapo hapo bila kuchelewa msichana yule akapiga hatua kumfuata.

“Mambo vipi!” Peter alimsalimia msichana yule.

“Poa. Karibu” Msichana yule alimkaribisha.

“Usijali. Hadi asubuhi shilingi ngapi?” Peter alimuuliza msichana yule.

“Kwako wewe, kijana mzuri na mtanashati, acha iwe elfu arobaini” Msichana yule alijibu.

“Kwangu bei hiyo, kwa wengine je?” Peter aliuliza huku akitaka nafasi ya kumzoea msichana yule.

“Kwa wengine bei ya kawaida tu”

“Kwa nini nami isiwe bei ya kawaida kama wengine?”

“Kwanza wewe una gari, kwa hiyo mambo ya usafiri si tatizo yaani hautotumia gharama ya usafiri. Cha pili ni kwamba tunaweza kufanya hata ndani ya gari, kwa maana hiyo unaweza usilipie gharama ya chumba nyumba ya wageni” Msichana yule alimjibu.

“Wewe ni mwanamahesabu mkubwa sana, halafu unavutia sana, umenona, mweupe, u mzuri na una mvuto mkubwa sana. Kuna chimbo lolote hapa unalijua? Chimbo ambalo hata tukikaa hivi na kupata nyama choma kusiwe na mishemishe za watu kutuona?” Peter alimuuliza msichana yule.

“Kwani unataka tuongee tena?”

“Yeah! Unajua sitaki tufanya mapenzi kama kuku. Ni lazima tukae chini tuongee, tule tushibe na kisha tuingie mzigoni manake bila kula unaweza kunifia kitandani” Peter alimwambia msichana yule na wote kuanza kucheka.

“Mmmh! Inamaana umejiandaa sana?”

“Yeah! Unajua nimekula mitishamba fulani hapa, yaani mpaka misuli imenisimama. Sasa tusipokula chakula cha kutosha. Itakuwa balaa. Ingia garini twende kwenye chimbo unaloliona kufaa” Peter alimwambia msichana yule ambaye akaingia ndani ya gari na kisha kuondoka mahali hapo.

Garini, katika kipindi chote Peter alikuwa akiongea kirafiki sana huku wakati mwingine akiingizia utani wa hapa na pale kiasi ambacho kikamfanya msichana yule kujitambulisha kwa jina la Husna huku akionyesha ushirikiano mkubwa kwa Peter ambaye alikuwa akiongea maneno mengi kama kuijiaza ujinga akili ya msichana yule ili kumuona kwamba ni kijana ambaye hakuwa na lengo jingine zaidi ya kutaka kufanya nae mapenzi usiku huo.

“Hili chimbo unalionaje?” Husna alimuuliza mara baada ya kufika katika baa ya New Mawela, baa iliyokuwa Sinza Vatican.

“Hapa bomba” Peter alijibu na kisha wote kuteremka na kwenda kukaa kwenye viti vilivyozunguka meza na kisha kumuagiza mhudumu kuwaletea nyama choma na bia.

****

Katika kipindi ambacho vinywaji na vyakula vilipokuwa vikiletwa mahali hapo, Peter alikuwa muongeaji mkubwa huku akitaka kuchukua muda wake mwingi kumsoma Husna ambaye wala hakuonekana kuwa mahali hapo zaidi ya kula na kunywa na kisha kuingia chumbani na kuifanya kazi ambayo Peter alikuwa akitaka kufanyika kwa malipo ambayo alikuwa akiyataka.

Vichwa vyao wote wawili vilikuwa vikifikiria vitu tofauti, katika kipindi ambacho Husna alikuwa akifikiria kufanya mapenzi na Peter, yeye, Peter hakuwa akifikiria hilo, alikuwa akikisumbua kichwa chake katika kufikiria ni kwa namna gani angeweza kufanikisha kile ambacho kilimfanya kuwa mahali hapo na msichana yule ambaye alionekana kuwa tayari kwa kufanya jambo lolote ili mladi tu aandaliwe fedha ya kutosha.

Wote walikula na kunywa, Japokuwa Husna alikunywa chupa nyingi za pombe lakini wala hakuweza kulewa hali ambayo ilimuonyesha kuwa mzoefu wa kunywa kiasi kikubwa cha pombe. Mara baada ya kumaliza, moja kwa moja Peter akamuita mhudumu ambaye akafika mahali hapo na kisha kuchukua vyombo vyake, huku Peter akiwa amejipanga vilivyo kuanza kuongea na Husna juu ya jambo lile ambalo lilimfanya kuwa mahali pale pamoja nae.

“Huwa kwa siku unaingiza kiasi gani katika kazi yako hii?” Peter alimuuliza Husna ambaye alikuwa akimaliza kunywa pombe iliyokuwa imebakia kwenye chupa.

“Inategemea. Ila sijui kwa sababu gani umeniuliza swali hilo?”  Husna alimuuliza Peter.

“Kuna kitu ningependa kufahamu zaidi ili nami nijue ni kipi natakiwa kukifanya” Peter alimwambia Husna.

“Ila wewe si mteja kama wateja wengine, sasa mbona unakuwa na maswali kabla ya kazi?” Husna aliuliza.

“Hauoni kama mimi ni mteja mkarimu? Kabla ya kazi nimeweza kulitosheleza tumbo lako kwanza. Shida yangu kwako Husna si kufanya mapenzi na wewe. Kuna kazi ambayo natakiwa kukushirikisha na kama ukifanikisha, nadhani itakuwa safi sana” Peter alimwambia Husna ambaye akaonekana kushtuka.

“Kazi gani?”

“Kazi ya kawaida sana. Usiogope, si kazi ya magendo, ni kazi ya amani kazi ambayo hata serikali imeipitisha kwamba ni halali” Peter alimwambia Husna huku akijitahidi kumuondoa wasiwasi.

“Niambie kwanza ni kazi gani”

“Ndio maana nikakuuliza unaingiza kiasi gani kwa siku ili niweze kukulipa fedha halali. Naweza nikakuingiza katika kazi hiyo halafu nikakulipa fedha kidogo kitu ambacho sitaki kitokee” Peter alimwambia Husna ambaye akakaa kimya kwa muda.

Maneno ambayo alikuwa akiongea Peter katika kipindi hicho yakaonekana kuanza kumuingia Husna. Peter alikuwa akiongea kiungwana sana, kitaratibu na kiustaarabu kupita kawaida. Maneno yale yakaonekana kuwa ushawishi mkubwa sana moyoni mwa Husna, wasiwasi juu ya Peter ukaonekana kumuondoka moyoni mwake, katika kipindi hicho alimchukulia Peter kuwa kama rafiki yake wa kipindi kirefu.

“Huwa ninaingiza hadi elfu hamsini kwa siku” Husna alimwambia Peter.

“Ok! Kuna kazi nitataka kukupa, kazi ambayo itakufanya kuingiza kiasi kikubwa zaidi ya hiki unachoingiza. Utakuwa tayari?” Peter alimwambia na kisha kumuuliza.

“Kazi gani? Mbona hautaki kuniambia ni kazi yenyewe?”

“Kazi ya kawaida sana halafu ni kazi rahisi sana” Peter alimwambia Husna.

“Kama si kazi haramu, mbona hautaki kuniambia?”

“Ok! Usijali. Kazi yenyewe ni kwamba nataka unionganishie msichana fulani hivi” Peter alimwambia Husna maneno ambayo yakaonekana kumshtua.

“Nikuonganishie msichana fulani?”

“Ndio. Mbona umeshtuka sana?”

“Umenishangaza sana. Nitakuonganishiaje sasa na wakati kila sababu ya kumpata msichana yeyote hapa jijini unayo” Husna alimwambia Peter.

“Kila sababu ninayo? Sababu gani?”

“Una fedha, una gari na unaonekana maisha yako mazuri sana. Hauoni kwamba hizo ni fimbo tosha kwa wasichana wa hapa jijini?” Husna alisema na kuuliza.

“Najua. Ila nitahitaji msaada wako. Huyu msichana si wa kumuingia pupa pupa. Si msichana anayeshobokea fedha au mali. Ingekuwa hivyo, kitambo sana ningekwishamchukua” Peter alimwambia Husna ambaye bado alionekana kuwa na mshangao.

Bado Peter alionekana kuwa kijana wa tofauti sana kwa Husna. Peter alionekana kuwa na maisha mazuri, alionekana kuwa miongoni mwa vijana waliokuwa na fedha nyingi ndani ya jiji la Dar es Salaam. Maisha yake kwa jinsi yalivyokuwa yakionekana yalikuwa ni maisha ya mtu ambaye alikuwa na fedha za kutosha, fedha ambazo zingemfanya kuishi maisha yoyote yale ambayo angependa kuishi katika kipindi hicho.

Kitendo cha kumwambia kwamba alikuwa akitaka kumuonganishia msichana fulani kilionekana kumshtua kupita kawaida. Hakuamini kama mwanaume ambaye alikuwa na fedha kiasi kile angeweza kuzungumza maneno yale mbele ya macho yake. Peter alionekana kuwa na kila sababu ya kumchukua msichana yeyote ambaye alikuwa akisifika kwa uzuri ndani ya jiji la Dar es Salaam, alionekana kutokuwa na sababu ya kumwambia kwamba alitakiwa kumuonganishia msichana fulani.

“Kwanza msichana yupi?” Husna alijikuta akiuliza.

“Demu fulani anaitwa Irene Godfrey. Ninampenda sana na ninatamani sana nimuoe kama itawezekana” Peter alimwambia Husna.

“Anaishi wapi?”

“Hosteli”

“Hosteli ipi?”

“Hiyo ya hapo Sinza Makaburini”

“Hii hosteli ya wasagaji?”

“Mmmh! Sijui kama ndio yenyewe au la”

“Si hii ipo karibu na Makaburi ambayo unaingia ndani kidogo?”

“Yeah!”

“Bila shaka demu mwenyewe ni msagaji pia” Husna alimwambia Peter ambaye akabaki kimya kwa muda.

“Sihitaji kujua kama ni msagaji au la. Ninachokitaka ni kumuona anakuwa mchumba wangu na kisha kuweka jiko ndani. Hilo tu” Peter alimwambia Husna.

“Nimekuelewa sana. Kwa hiyo unataka mimi nianze kufanya nini ili nihakikishe kwamba unamchukua huyo demu?” Husna alimuuliza.

“Nataka ukaishi ndani ya hosteli ile” Peter alimwambia Husna.

“Mimi! Nikaishi ndani ya hosteli ile? Hosteli ya wasagaji!”

“Yeah! Haimaanishi ukikaa na mchungaji nawe utakuwa mchungaji. Unaweza ukaishi nae mwisho wa siku ukawa cha pombe. Na haimaanishi kwamba ukiishi karibu na msikiti utakuwa ukienda sana msikitini, unaweza ukaishi karibu na msikiti na nyumbani kwako ukatengeneza baa. Umenipata nimemaanisha nini hapo?” Peter alisema na kisha kumuuliza.

“Nimekupata. Kwa hiyo unataka niende nikaishi ndani ya hosteli ile?”

“Yeah! Hiyo ndio maana yangu”

“Na vipi kuhusu malipo?”

“Wewe unataka kiasi gani kwa siku? Manake ukianza kazi yangu hautakiwi kwenda Ambiance”

“Hilo si tatizo. Laki moja kwa siku. Ipo?”

“Hilo si tatizo. Tena kutakuwa na marupurupu ya kumwaga mpaka kazi ikamilike” Peter alimwambia Husna.

“Sawa. Nitakwenda huko”

“Ila hakikisha kwamba unafanikiwa. Katika kipindi chote hicho mimi nitakuwa kama kaka yako. Umenielewa?”

“Usijali”

Kuanzia usiku huo Peter na Husna wakaanza kuwa karibu zaidi na mishemishe za kuanza kutafuta chumba ndani ya hosteli ile kuanza mara moja, Walichokifanya ni kuelekea katika hosteli ile ambapo wakaulizia mahali alipokuwa akiishi mhusika, walipoambiwa wakaanza kuelekea huko. Kila mmoja ndani ya gari alionekana kuwa na furaha kwa kuona kwamba kila kitu ambacho walikuwa wamepanga kingekwenda kufanikiwa kama walivyotaka iwe.

Kichwani mwa Husna alionekana kuamini kila kitu ambacho Peter alikuwa amemuambia kuhusiana na Irene bila kujua kwamba mtu huyo alikuwa akifikiria jambo jingine kabisa zaidi ya kuwa na mahusiano na msichana huyo. Ndani ya moyo wake, Peter alikuwa akitaka kumuua Irene ambaye alionekana kuwa chanzo cha kila kitu kilichompelekea Rose kutoroka ndani ya nyumba yao na kuelekea kusipojulikana huku akiwa na ujauzito ambao aliamini kwamba ulikuwa wake.

Hawakutumia muda mrefu, wakawa wamefika Mwenge, mahali ambapo alikuwa akiishi mmiliki wa hosteli ile ambapo baada ya kuwaelezea shida yao, akawaambia kwamba kulikuwa na vitanda vingine ambavyo vilikuwa wazi, kwa hiyo Husna alikuwa amepata nafasi bila tatizo lolote lile. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwao, kila kitu ambacho walikuwa wamepanga kikaonekana kuwa katika mstali, kazi kubwa ambayo walikuwa wameiona kabla ikaonekana kuwa kazi nyepesi ambayo ilikuwa ni sawa na kumsukuma mlevi katika mteremko.

“Fanya kazi Husna. Wakikuuliza unasoma chuo gani wewe sema chuo chochote kile” Peter alimwambia Husna katika kipindi ambacho alikuwa amekwishakabidhiwa kitanda ndani ya hosteli hiyo.

“Hakuna tatizo”

“Ungependa niwe nakulipa cash au niwe nakuingizia kwenye akaunti yako ya simu?”

“Ingiza kwenye akaunti”

“Hakuna tatizo. Naomba ndani ya mwezi mmoja na nusu kazi iwe imefanyika. Ikitokea nimempata, utafurahi na roho yako” Peter alimwambia Husna.

“Utanipa fedha zaidi au?” Husna aliuliza huku akiachia tabasamu.

“Naweza kukupeleka Dubai ukafanye shopping tu. Ila kwanza kamilisha kazi yangu” Peter alimwambia Husna.

Siku hiyo ndio ikawa siku ya kwanza ambayo Husna akalala ndani ya hosteli hiyo. Kwa kuwa alikuwa mchangamfu sana akaweza kuanza kujipatia marafiki wengi mahali hapo. Kila wakati Husna alikuwa akionyesha dhahiri kwamba kwake, furaha ndio ilikuwa sehemu ya maisha yake. Ingawa alikuwa akiongea na wasichana wengi kadri siku zilivyozidi kwenda mbele lakini katika kichwa chake alikuwa akimfikiria Irene ambaye alionekana kuwa mgumu sana kuzoeana nae kutokana na Irene kuishi kwa wasiwasi sana mahali hapo huku mara kwa mara akiwa anatoka na kuelekea katika miangaiko yake.

Husna hakutaka kujali sana, kitu ambacho alikuwa ameambiwa kukifanikisha ni msichana huyo kuwa rafiki yake na kisha mambo mengine kufuata. Kila siku Irene aliendelea kuwa mtu wa kutoka toka tu, hakutulia sana hosteli jambo ambalo lilimuwia vigumu sana Husna kuweza kuzoeana nae.

“Nitafanikiwa tu” Husna alisema katika kipindi ambacho wiki ya kwanza ilikuwa imekatika tangu aanze kukaa ndani ya hosteli hiyo.

Maisha yaliendelea zaidi na zaidi mpaka mwezi kukatika na hatimae mwezi dume kuingia. Huu ulikuwa ni mwezi ambao wanawake wengi walikuwa wakipigika kwa kutokuwa na fedha hata mara moja, katika kipindi hicho ndicho ambacho wasichana wengine walikuwa wakifikia hatua hadi ya kwenda katika viwanja mbalimbali kujiuza kwa ajili ya kupata kiasi cha fedha ambacho kingeweza kuwawezesha katika maisha yao. Kwa Husna wala hakuonekana kuwa na tatizo lolote lile, kwa sababu alikuwa na fedha nyingi, hapo ndipo akaona kuwa nafasi ya kuweza kumuingiza Irene katika himaya yake kwani nae alionekana kuwa kama wasichana wengine, wasichana waliopigika katika kipindi hicho cha Mwezi Dume.

*****

Hii ilikuwa inaitwa MARIA HOSTEL, ilikuwa ni moja ya hostel ambayo ilikuwa ikipatikana katika mtaa wa Sinza Makaburini. Hosteli hii ilikuwa na vyumba zaidi ya ishirini ambapo kila chumba kimoja walikuwa wakikaa wasichana wanne. Hosteli ya Maria ilionekana kuwa nzuri na yenye mvuto lakini mambo mengi ambayo yalikuwa yakiendelea ndani ya hosteli hiyo hayakuwa mazuri na ya kufurahisha.

Wasichana ambao walikuwa hawajatulia, wasichana ambao walikuwa wakijiuza walikuwa wakipatikana katika hosteli hiyo tena wote wakiwa ni wanachuo wa vyuo mbalimbali ndani ya jiji la Dar es Salaam. Ukiachana na tabia hiyo, kulikuwa na tabia ambayo wala haikuwa na mvuto kabisa, tabia ambayo iliwafanya wasichana wengi kutotaka kwenda kuishi ndani ya hosteli hiyo, usagaji.

Wasichana wengi ambao walikuwa wakiishi ndani ya hosteli hiyo walikuwa wakipenda kusagana tabia ambayo ikaonekana kuwa kero sana. Ndani ya jiji la Dar es Salaam, stori juu ya tabia zilizokuwa zikifanyika ndani ya hosteli hiyo zilikuwa zimesambaa sana, kuna wasichana ambao hawakutaka hata kwenda kuishi ndani ya hosteli hiyo lakini kuna wasichana wengine ambao walikuwa wakikimbilia.

Tabia ile ikaonekana kuwa sugu na iliendelea kukua kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Msichana Irene ndiye ambaye alionekana kuwa nguri katika mchezo mzima wa kusagana, yeye ndiye ambaye alikuwa akiwashughlikia wasichana wengine ambao walikuwa wakitaka kusagwa. Irene akawa na jina kubwa, sifa yake kubwa ya usagaji ilikuwa imeenea ndani ya hosteli ile. Kwa wasichana ambao walikuwa wakipenda sana kusagana walikuwa wakimheshimu sana ila kwa wasichana ambao hawakuwa wakiupenda kabisa mchezo ule walikuwa wakimuogopa sana na wala hawakutaka kumsogelea.

Japokuwa baadhi ya viongozi wa serikali walikuwa wakipiga kelele kuhusiana na hosteli hiyo kufungwa lakini hakukuwa na kitu kilichotendekea zaidi ya hosteli ile kuzidi kutumika zaidi na zaidi. Matendo ambayo yalikuwa yakizidi kufanyika ndani ya hosteli ile yalikuwa matendo machafu ambayo wala hayakuwa ya kuelezeka katika jamii ya Kitanzania, wasichana wengi ambao walikuwa na wapenzi wa na kisha kuhamia ndani ya hosteli ile, baada ya miezi sita hawakuonekana kama walikuwa wakitaka kuendelea na mahusiano na wapenzi wao.

Tabia hiyo ilianza zamani kidogo, ilianza kisiri sana lakini mara baada ya Irene kuhamia ndani ya hosteli hiyo miaka miwili iliypita, hakukuwa na siri tena, mambo yakawa hadharani. Mchezo ule ulikuwa ukifanyika na kadri ulivyoendelea kufanyika na ndivyo ambavyo ulizidi kupata wanachama wengi mpaka kufikia kipindi ambacho asilimia sitini ya wasichana waliokuwa wakiishi mule kuanza kusagana.

Katika kipindi kigumu cha mwezi dume, asilimia kubwa ya wanawake walikuwa wakipigika sana, hawakuwa na fedha jambo ambalo lilikuwa liwafanya wasichana wengi kuondoka na kisha kujiingiza katika kazi ambazo wala hazikuwa kazi rasmi, kujiuza mitaani kwa ajili ya kupata fedha za kuweza kumalizia shida zao.

Wanawake wengi walikuwa wakiondoka katika hosteli hiyo na kwenda kujiuza huku wengine wakiwaita wanaume ndani ya vyumba vyao na kisha kumalizia shida zao ndani ya hosteli hiyo. Katika kipindi cha mwezi dume, hata kwa wasichana ambao walikuwa wakisagana, katika kipindi cha mwezi huo hawakuwa na jinsi, nao walikuwa wakijiingiza mitaani, walikuwa wakifanya hivyo kama njia mojawapo ya kujitafutia fedha za kuwafanya kusogeza siku.

Wanaume waliokuwa wakisoma katika chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndio ambao wengi walikuwa wakifululiza kuja ndani ya hosteli hiyo, walikuwa wakifanya mapenzi ovyo na wasichana hao, na asubuhi, ni mipira ya kiume ndio ambayo ilikuwa imejaa katika mapipa ya uchafu yaliyokuwa katika hosteli hiyo.

Japokuwa wasichana walikiona kipindi hicho kuwa mwezi dume lakini hali ilionekana kuwaa tofauti kabisa kwa msichana Husna ambaye alijitambulisha kama mwanachuo wa chuo cha St’ Peters kilichokuwa Kawe jijini Dar es salaam. Maisha ya Husna yalionekana kuwa ya tofauti sana, wakati wasichana wengi walikuwa wamepigika huku wakihitaji fedha, yeye alikuwa na fedha kama kawa na wala hakukuonekana kama kungekuwa na dalili zozote za kumaliza fedha zile na kubaki mtupu.

Hapo ndipo wasichaana wengine walipoanza kujigonga, Husna hakuwa na habari nao, kazi yake kubwa katika hosteli hiyo ni kuhakikisha kwamba msichana Irene anakuwa mpenzi wa Peter kama ambavyo alitakiwa kuhakikisha kitu hicho. Alichokifanya Husna ni kuanza kujipendekeza kwa Irene, kila alipokuwa akimuona alikuwa akimpa hi huku wakati mwingine akimtaka watoke sehemu waende kula.

Husna akaanza kuonekana kuwa msaada mkubwa kwa Irene ambaye nae mwezi dume ukaonekana kumkimbiza kupita kawaida, hapo ndipo Irene alipoona kwamba alitakiwa kuhakikisha kwamba hampotezi Husna ambaye mara nyingi sana alikuwa alikua akimnunulia kila kitu alichokuwa akikitaka kwa wakati huo. Fedha zile alizokuwa akipewa Husna  kutoka kwa Peter zikaonekana kuanza kumlevya Irene ambaye aliona kama yupo ndotoni kwani halikuwa jambo la kawaida kumuona msichana akiwa na fedha nyingi kiasi kile hasa katika kipindi kama hicho.

“Mmmh! Wewe unaishi wapi?” Irene alimuuliza Husna katika kipindi ambacho walikuwa katika mgahawa mmoja mkubwa wakila.

“Kwa nini umeuliza hivyo?” Husna aliuliza kabala ya kutoa jibu.

“Basi. Nimejisikiaa kuulia”

“Kwetu kabisa ni Singida, kule Manyoni” Husna alidanganya.

“Mmmh!! Baaba yako anafanya kazi wapi?”

“Yeye ni mfanyabiashara mkubwa sana. Ana kampuni nyingi hapa Tanzania. Ila kwa sasa yupo Marekani kuendelea na biashara nyingine” Husna aliendelea kumdanganya.

“Kumbe! Nilitaka kufahamu tu maanake shosti unaonekana kuwa na kisima cha fedha” Irene alimwambia Husna.

“Kuhusu fedha, hilo si tatizo. Huwa mpaka wakati mwingine natafuta watu wa kutumia nao. Fedha zinachosha sana kutumia hizi natamani niwe nazitupa jalalani au nizimwage pale hosteli watu wachukue, zinanikera sana” Husna alimwambia Irene.

“Daah! Uzimwage na wakati wakina sisi tunazitafuta”

“Usijali. Nitajitahidi kukusaidia kila penye shida. Nitaongea na kaka aniongezee fedha zaidi” Husna alimwambia irene.

“Kaka yako yupi?”

“Si yule aliyeniletea hosteli”

“Hapana. Wala simfahamu”

“Ninae. Unataka kumuona?”

“Labda. Ikiwezekana”

“Sasa hivi?”

“Mmmh! Kwani yupo wapi?”

“Nikiwasiliana nae tu anakuja. Huwa anapenda kuwa karibu na mdogo wake na kamwe hataki kusikia nina tatizo” Husna alimwambia Irene.

Hiyo ikaonekana kuwa nafasi moja kubwa sana, alichokifanya Husna ni kuchukua simu yake na kisha kumpigia Peter ambaye kwake alijitambulisha kwa jina la Abdallah. Peter wala hakuchukua muda mrefu, akafika mahali hapo huku akiwa katika gari lake aina ya Prado, alipofika, moja kwa moja akaelekea katika mghahawa ule na kisha kutulia katika kiti kimoja kati ya viti vilivyozunguka meza ile.

“Karibu Abdallah” Husna alimkaribisha Peter.

“Asante sana” Peter aliitikia na kisha kukaa.

Maongezi yakaanzia mahali hapo, alichokifanya Peter ni kuanza kumwangalia Irene katika mwangalio ule ulioonyesha kwamba alikuwa akimtaka msichana huyo kimapenzi. Muonekano wake wa kinafiki ambao alikuwa akiuonyesha mahali hapo ulionekana sahihi na maneno ambayo alikuwa amemwambia Husna na wakati moyoni mwake alikuwa tofauti kabisa na mwangalio ule.

Chuki kubwa ilikuwa imemkaba kooni mwake kila alipokuwa akimwangalia Irene mahali hapo, hakuamini kama siku hiyo ndio ambayo alikuwa pamoja na Irene ambaye alikuwa kila sababu iliyosababisha mpenzi wake, Rose kutoroka nyumbani kwao. Japokuwa uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu kila wakati lakini moyoni alikuwa akionekana kuwa tofauti kabisa. Hakumpenda kabisa Irene.

Siku hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza kwa wawili hao kufahamiana, Peter hakutaka siku hiyo iwe ya mwisho, alichokifanya ni kuchukua namba ya simu ya Irene na kisha kuanza kuwasiliana simuni. Kitu ambacho alikuwa akikitaka Peter ni kumfanya Irene kuvutika kwake zaidi, alikuwa akiwasiliana nae sana huku akimtumia kiasi cha fedha kama kumlevya. Fedha ambazo alikuwa akitumiwa zikaonekana kuwa kama sumu moyoni mwa Irene, bila kupenda akajikuta akianza kumpenda Peter ambaye moyoni mwake hakuwa na chembe ya mapenzi hata mara moja zaidi ya kufikiria mauaji tu.

Kila walipokuwa wakionana, Irene alikuwa akishindwa kuvumilia, alikuwa akimuonyeshea Peter hisia kali za kimapenzi lakini Peter hakuonekana kujali kitu chochote kile, alichokuwa akikiangalia si mapenzi, alikuwa akifikiria kufanya mauaji zaidi. Kila siku usiku Irene alikuwa akihakikisha akiongea na Peter huku tamaa ya moyo wake ikitaka kumuona Peter akiangukia katika mikono yake siku moja.

“Abdallah!” Irene alimuita Peter katika kipindi ambacho walikutana kwenye mgahawa wakipata chakula cha usiku.

“Naam”

“Unaona nini kila ukiyaangalia macho yangu?” Irene alimuuliza Peter.

“Kwa nini umeuliza hivyo?”

“Nataka kufahamu tu. Unaona nini?” Irene alimuuliza Peter.

“Mapenzi” Peter alijibu.

“Umegundua kwamba ninkupenda sana?”

“Yeah! Nimegundua. Mapenzi huwa hayajifichi Irene” Peter alimwambia Irene huku moyoni akijiona kuwa mshindi.

“Umehisi kitu chochote moyoni mwako juu yangu? Hasa mapenzi?”

“Umekuwa na maswali mengi mno Irene. Halafu maswali yote magumu” Peter alimwambia irene.

“Najua, lakini naomba unijibu Abdallah”

“Yeah! Huwa ninahisi sana juu ya hilo” Peter alimwambia Irene.

“Unanipenda?”

“Ooopss!! Naomba tule kwanza. Nitakujibu tu Irene”

“Unafikiri chakula kitapita kooni mwangu kama hautoamua kuniambia ukweli?” Irene alimwambia Peter.

“Najua. Ila jipe matumaini kwamba nitakuwa wako Irene, tena wako peke yako mpaka kifo kitutenganishe” Peter alimwambia Irene.

“Ninakupenda Abdallah”

“Najua Irene. Ila nitataka kukufanyia kila kitu kama sapraizi”

“Kivipi?”

“Ndio maana nikakwambia kula kwanza”

“Sawa”

Moyo wa Irene ulikuwa na dukuduku kubwa la kutaka kumsikia Peter akimwambia kwamba anampenda. Moyoni alikuwa na mapenzi ya dhati kwa Peter, fedha za Peter zikaonekana kumchanganya kupita kawaida. Fedha zikamfanya kuangukia mapenzini bila kujua kwamba kila kitu kilichokuwa kikifanyika kilikuwa kama mtego kwake, mtego wa kumpeleka katika mauti.

Walipomaliza kula, moja kwa moja wakaelekea garini ambapo wakaanza kuondoka. Kitu kilichokuja kichwani mwa Peter siku hiyo ilikuwa ni lazima akamilishe kile ambacho alitakiwa kukikamilisha, kumuua Irene ambaye tayari alionekana kutosikia chochote juu yake. Alipomfikisha maeneo ya hosteli, akambusu.

“Jiandae kwa sapraizi Irene. Nitakuwa muwazi kwako siku ya leo” Peter alimwambia Irene.

“Muda gani?” Irene aliuliza huku akionekana kufurahia.

“Usijali. Nitakupigia simu na kuelekea sehemu nzuri ambayo imekaa romantic” Peter alimwambia Irene.

“Kweli?”

“Siwezi kukudanganya. Jiandae, nitakupitia baaadae, kila kitu kitakuwa sapraizi kwako” peter alimwambia Irene ambaye alionekana kuwa na furaha kupita kawaida.

Siku hiyo, Irene alionekana kuwa na furaha kupita kawaida, hakuamini kama mwanaume ambaye alikuwa akitaka kuwa nae katika kipindi hicho alikuwa amekwishaanza kukubaliana nae, akaelekea ndani ya jengo la hosteli huku akiwa na furaha kubwa, hakuamini kama angeweza kukamilisha kuuteka moyo wa Peter kirahisi namna hiyo. Alipofika ndani ya chumba alichokuwa akikaa, akapumzika huku akionekana kuwa mwingi wa furaha.

Furaha yake katika kipindi hicho ilikuwa imezidi kiwango, hakujua ni kwa jinsi gani alitakiwa kuelezea. Hakuonekana kujua, hakujua kwamba moyo wa Peter katika kipindi hicho ulikuwa ukifikiria kitu kimoja tu, kumuua kama kisasi kwa kile alichokuwa amekisababisha kwa Rose, ila kabla ya kuuawa, kulikuwa na maswali ambayo alitakiwa kujibu. Katika usiku huo, mambo yote hayo ndio ambayo yangekwenda kutokea huku Irene akijua kwamba alikuwa akienda kufanyiwa sapraizi itakayomfanya kumuona Peter kuwa katika mapenzi ya dhati kwake kumbe ukweli ni kwamba alitakiwa kuuawa.

****

Peter alionekana kuwa na furaha, hakuamini kama kweli kitu ambacho alikuwa akikihitaji kwa siku nyingi taysri siku hiyo kilionekana kwenda kukamilika. Moyo wake ukajawa na furaha kupita kawaida, hakuamini kam masaa machache yajayo angeweza kukamilisha kile ambacho alitakiwa kukikamilisha katika kipindi hicho. Ndani ya gari, bado furaha yake ilikuwa ikiendelea waziwazi, kazi ile katika kipindi cha nyuma aliiona kuwa ngumu sana lakini mara baada ya kuwa nusu ya kuifanikisha, akaonekana kuuona urahisi mkubwa wa kazi ile kuliko alivyofikiria kabla.

Katika kipindi hicho alikuwa ndani ya gari akielekea nyumbani kwao. Alitaka kumtaarifu baba yake, Bwana Edward kla kitu ambacho kilikuwa kimetokea na kwamba alikuwa akienda kukamilisha kila kitu ndani ya masaa machache ila hakutaka kazi yote aifanye peke yake bali alitakiwa kusaidiwa kama ambavyo walivykuwa wamepanga kabla.

Alipofika nyumbani, moja kwa moja akaanza kumuita baba yake na kisha kuelekea nae nje kwa ajili ya kufanya maongezi ya dharura ambayo hayakutakiwa kusikika na mtu yeyote zaidi yao. Kwa jinsi uso wa Peter ulivyokuwa ukionekana, Bwana Edward akajua wazi kwamba kila kitu ambacho walikuwa wakikitaka kilikuwa kimekwenda kama jinsi walivyotaka kiwe. Walipoona kwamba wamesimama sehemu ambayo ilikuwa salama, wakaanza kuongea.

“Imekuwaje?” Bwana Edward aliuliza huku akionekana kuwa na shauku ya kutaka kufahamu.

“Kila kitu safi”

“Kwa hiyo fedha zimekwenda kihalali?”

“Yeah! Kila kitu kipo poa. Kazi imebakia yenu sasa” Peter alimwambia baba yake, Bwana Edward.

“Hebu niambie umefikia hatua gani mpaka sasa hivi?”

“Nimeongea nae na baadae nataka kwenda kuonana nae sehemu fulani,hapajui ila ninachokitaka nyie muwe pale Magomeni Kanisani ili kama nitatokea na gari kutoka huku Sinza basi nikifika pale muingie garini” Peter alimwambia.

“Wewe umepanga kwenda wapi pamoja nae?”

“Nilimwambia kwamba ningemtoa mtoko baade ila bado sijajua wapi na wala sitaki kujua. Ninachotaka ni nyie kuingia garini marabaada ya kufika Magomeni Kanisani” Peter alimwambia baba yake.

“Hakuna tatizo” Bwana Edward alimwambia.

Kwa haraka sana bila kuchelewesha kitu chochote kile mawasiliano baina ya Bwana Edward na Bwana Shedrack yakaanza kufanyika. Sauti ya Bwana Shedrack ilisikika kuwa na furaha kupita kawaida mara baada ya kuambiwa kwamba kila kitu kilikuwa kimekamilika na ni kazi ya mauaji tu ndio ambayo ilitakiwa kufanyika katika kipindi hicho.

Bwana Shedrack hakutaka kujali kama Irene alikuwa mtoto wa dada yake, kitu ambacho alikuwa akikiangalia katika kipindi hicho ni kumuua msichana huyo kwa sababu alikuwa amemharibia binti yake pamoja na kumfanya kutoroka bila kufahamu ni mahali gani alipokuwa katika kipindi hicho. Mara baada ya kuongea mengi, simu ikakatwa na kila mmoja kuusubiria muda huo.

Siku hiyo mshale wa dakika ukaonekana kwenda taratibu sana tofauti na siku nyingine, kila mmoja alikuwa na kiu ya kukamilisha kazi ambayo ilikuwepo mbele yao, kumuua Irene na kisha kuendelea na mambo yao. Hakukuwa na mtu ambaye alimuonea huruma Irene, kwao, msichana huyo alionekana kuwa mbaya ambaye alikuwa na kila sababu za kuuawa kwa mikono yao wenyewe.

Muda ambao walikuwa wakiusubiria ukafika, katika kipindi ambacho Peter alikuwa akielekea hosteli kwa ajili ya kumchukua Irene, Bwana Shedrack akafika mahali hapo na kisha kuanza kuelekea barabarani ambapo wakakodi bajaji iliyoanza kuwapeleka mpaka Magomeni Kanisani na kisha kuteremka huku wakilisubiri gari la Peter kwa kujua kwamba hata Irene angekuwepo ndani ya gari hilo.

Peter bado alikuwa safarini kuelekea katika hosteli ya Maria iliyokuwa Sinza Makaburini, ndani ya gari lake, mawazo yake yalikuwa juu ya mpenzi wake, Rose ambaye mpaka katika kipindi hicho hakuwa akijua mahali alipokuwa. Mawazo yake hayakuishia kumfikira Rose, yakaanza kuufikiria na ujauzito ambao alikuwa nao Rose, kwake, ujauzito ule ukaonekana kuwa muhimu sana kwani alikuwa na kiu kubwa ya kumuona mtoto wake ambaye angezaliwa.

Alitumia dakika kumi mpaka kufika Sinza ambapo akampigia simu Irene ambaye akatoka nje ya jengo la hosteli ile na kisha kuingia garini. Kama kawaida yake, alikuwa amevaa sketi fupi ambayo iliishia juu ya magoti yake huku kwa ndani akionekana dhahiri kuvaa zile nguo za ndani ambazo zilikuwa zimeingia katikati ya makalio yake, bikini. Alipolifikia gari lile, huku akionekana kuwa na furaha, akaingia ndani.

“Nimechelewa sana mpenzi?” Peter alimuuliza Irene.

“Hapana. Umekuja muda muafaka, haujachelewa wala kuwahi” Irene alimwambia Peter.

“Umependeza sana. Umependeza kupita kawaida” Peter alimwambia Irene ambaye akaachia tabasamu pana.

“Nashukuru sana mpenzi. Napenda kuvaa hivi kila nitokapo usiku” Irene alimwambia Peter.

Peter hakutaka kupoteza muda mahali hapo, alichokifanya ni kuwasha gari na kisha kisha kuondoka. Hapo, mawazo yake yakazidi kuongezekana zaidi, akazidi kufikiria kuhusu mauaji ambayo yalitakiwa kufanyika. Kama walivyokuwa binadamu wengine, kwa mbali akaanza kumuonea huruma Irene kwa kuona kwamba alikuwa njiani kuuawa, yaani hakuwa na zaidi ya masaa mawili kuvuta pumzi ya dunia hii.

Japokuwa roho ya huruma ilikuwa imeanza kumuingia lakini akajikuta akiilazimisha kuitoa kwani katika kipindi hicho hali hiyo haikutakiwa kabisa ndani ya mwili wake, alitakiwa kuwa na roho ya kikatili, roho ambayo ingeendelea kumwambia kwamba msichana yule ndiye alikuwa chanzo cha msichana wake kutoroka na hivyo kumuwia wakati mgumu kumuona mtoto wake.

Safari iliendelea zaidi na zaidi, Irene hakutaka kuuliza chochote juu ya mahali walipokuwa wakielekea katika kipindi hicho kwani kitu ambacho alikuwa akikijua ni kwamba mpenzi wake huyo, Peter ambaye alikuwa akimjua kwa jina la Abdallah alikuwa amemuandalia sapraizi moja kubwa ambayo ingemfanya kutokuamini macho yake.

“Ila mbona hautaki kuniambia ni sapraizi gani uliyoniandalia?” Irene aliuliza huku akijichekesha.

“Nikikwambia, haitokuwa tena sapraizi” Peter alimwambia Irene.

“Ila nitaifurahia?”

“Hapana”

“Hahaha! Kwa hiyo nitalia?”

“Hapana”

“Sasa nitakuwaje?”

“Utazimia kwa mshtuko”

“Hahaha! Ni kubwa kiasi gani?”

“Utaiona tu mpenzi. Hautakiwi kuwa na wasiwasi” Peter alisema na hapo hapo bila kuchelewa akamusogeza uso wake karibu na Irene na kisha kuanza kubadilishana nae mate.

Kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea ni kama kumtia upofu Irene ili ajione kwamba alikuwa akipendwa na kuthaminiwa kumbe si hivyo. Kitendo kile ambacho alikuwa amefanyiwa cha kubadilishana mate na Peter kikaonekana kumchanganya kupita kawaida na hivyo kuendelea kumuwekea upofu kwa kuona kwamba Peter alikuwa mpenzi sahihi ambaye aliletwa ndani ya dunia hii kwa ajili yake tu.

Gari lilipofika maeneo ya Magomeni Kanisani, Peter akalitembeza gari pembeni na kisha kulisimamisha. Kwa mbali Irene akaonekana kushtuka lakini kutoka na uaminifu mkubwa ambao alijiwekea kwa Peter ukaonekana kuuondoa wasiwasi ambao alikuwa nao. Peter akaanza kuangalia huku na kule mahali pale, mara Bwana Shedrack na Bwana Edward wakaonekana wakija kwa kasi, walipolifikia gari lile, wakaingia ndani.

Irene akaonekana kushtuka kupita kawaida, hata kabla hajauliza ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, akajikuta akipigwa roba na kisha kuvutwa katika siti za nyuma na kisha kuwekwa katikati. Peter hakutaka kuchelewa, alichokifanya mara baada ya kuona kwamba kila kitu kilikuwa kimekwenda kama kilivyotakwa, akaliondoa gari mahali hapo.

Irene hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea mpaka watu wale kuingia ndani ya gari lile na kisha kumuweka chini ya ulinzi. Hapo ndipo mawazo yake yalipomwambia kwamba Peter hakuwa mtu mzuri hata kidogo kutokana na kile ambacho kilikuwa kimetokea.

“Abdallah….!!” Irene alijikuta akiita huku akionekana kuwa na wasiwasi.

“Nyamaza…!!” Bwana Edward alimwambia huku akimpiga kibao kimoja cha nguvu.

“Irene akaanza kulia, kibao kile kikaonekana kumuumiza kupita kawaida, tayari maisha yake yakaonekana kuwa kwenye hatari, hakuamini kile ambacho kilikuwa kimeendelea baina yake na Peter kilikuwa kama mchezo fulani wa kuigiza tu.

“Rose yupo wapi?” Lilikuwa ni swali lililosikika kutoka kwa mtu aliyekuwa amekaa upande wake wa kulia.

“Mjomba..!!” Irene aliita huku akionekana kutokuamini.

“Rose yupo wapi?” Bwana Shedrack alilirudia swali lake.

“Sijui” Irene alijibu.

“Ok! Tutajua kama unajua au haujui” Bwana Shedrack alimwambia Rose.

Safari ilikuwa ikielekea na katika kipindi hicho walikuwa wakielekea Kawe, sehemu ambayo walikuwa wamepanga kufanya mauaji ya Irene. Muda wote Irene alikuwa akitetemeka kwa hofu, uwepo wa mjomba wake ulikuwa umemtia wasiwasi kupita kawaida kwa kuona kwamba siku hiyo .ndio ilikuwa siku yake ya mwisho kwani yule mtu ambaye alikuwa akimkimbia kila siku, leo hii alikuwa katika mikono yake.

“Naomba unisamehe mjombaaaaa..!!” Irene alisema huku akionyesha dhahiri kuomba msamaha.

“Wewe ni kiburi, sasa leo tutakikomesha hicho kiburi chako” Bwana Shedrack alimwambia Irene ambaye bado alikuwa akiomba msamaha huku akilia.

“Naomba unisamehe”

“Ningekusamehe endapo ungesema Rose yupo wapi. Ila umejifanya kiburi, mimi ni kiburi zaidi yako” Bwana Shedrack alimwambia Irene.

“Naomba unisamehe nitawaambia Rose yupo wapi” Irene alisema huku akiendelea kulia na kuzidi kuomba msamaha.

“Tuambie kabla hatujafika sehemu husika, tukifika huko hatutotaka kuambiwa chochote kile, usalama wako ni kutuambia kabla hatujafika huko” Bwana Edward alimwambia Rose.

“Rose yupo Kinondoni” Irene alijibu huku akiendelea kulia.

“Kinondoni wapi?”

“Kinondoni B”

“Anafanya nini huko?”

“Aliniomba aende akakae katika chumba changu” Irene alijibu.

“Kwa hiyo kwa nini ulikuwa ukimsaga binti yangu?” Bwana Shedrack alimuuliza Irene.

“Naomba unisamehe”

“Hilo sio jibu. Ninataka jibu Irene. Kwa nini?”

“Naomba unisamehe mjomba”

Bwana Shedrack hakutaka kuongea kitu chochote kile, akabaki kimya huku akionekana kuifuatilia safari ile. Gari lilizidi kusonga mbele, foleni kubwa ambayo ilikuwepo barabarani ikaonekana kuwachelewesha kupita kawaida. Katika kipindi chote cha safari Irene alikuwa akiendelea kuomba msamaha, tayari alikwishaona kwamba mwisho wa safari hiyo kulikuwa na kitu kingine ambacho kingeweza kutokea.

Akazidi kuomba msamaha zaidi na zaidi lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kumuelewa. Walipofika Kawe Round About, wakachukua barabara ya vumbi ambayo ilikuwa ikielekea ufukweni na kisha kulisogeza gari kwa mbele kidogo, wakalipaki na kisha kutulia huku Bwana Shedracka kiitoa bunduki yake.

“Nafasi ya mwisho kwako, kwa nini ulikuwa ukimsaga Rose?” Bwana Shedrack alimuuliza Irene.

“Naomba unisamehe” Irene alimwambia.

Kitendo cha kuomba msamaha ndicho ambacho kikaonekana kumkasirisha zaidi, walichokifanya ni kumteremsha Irene kutoka garini. Irene akaanza kupiga kelele za kuomba msaada lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyefika mahali kule. Walipoona kwamba alikuwa mbishi kupiga hatua, Peter akaanza kumbebea  begani na kisha kuzidi kuelekea nae ufukweni.

Muda ulikuwa ni saa saba kasoro, usiku ulikuwa umekwenda sana, Irene alikuwa akizidi kupiga kelele lakini hakukuwa na mtu yeyte ambaye alionekana kuja mahali hapo na kumuokoa kutoka katika mikono ya watu hao. Ufukweni hakukuonekana kuwa na watu kabisa, vibanda vya wavuvi vilikuwa vikionekana lakini hali ilikuwa ni ya ukimya kabisa. Walichokifanya ni kumlaza Irene pembeni kabisa ya maji ya bahari ya Indi na kisha kumtaka kusali sala yake ya mwisho.

“Nisamehe mjomba” Irene alimwambia Bwana Shedrack huku akilia kama mtoto.

“Nikusamehe. Umemsaga mtoto wangu, ukaona haitoshi, ukamtorosha pia halafu leo unasema nikusamehe, nitaanza vipi kukusamehe wewe malaya mkubwa?” Bwana Shedrack alimuuliza huku akionekana kuwa na hasira kali.

Mdomo wa bunduki ulikuwa umemlenga usoni mwake, Irene alikuwa akilia lakini kilio chake hakikumfanya mtu yeyote kuwa na huruma nae. Bila kuchelewa na bila kuuliza kitu chochote kile, Bwana Shedrack akabonyeza kitufe cha bunduki ile, risasi ikatoka na kumpiga Irene katika paji la uso, Bwana Shedrack hakuonekana kuridhika, bado alijiona kuwa na hasira sana na Rose, akampiga risasi nyingine mbili za kifuani na baada ya kuhakikisha kwamba alikuwa amekufa, wakaanza kuondoka mahali hapo.

“Bora nimekuua malaya mkubwa wewe” Bwana Shedrack alisema huku akionekana kuridhika.

Wala hawakufika mbali, wakaanza kusikia minong’ono ya watu mahali fulani kulipokuwa na vichaka, mara mikuki ikaanza kurushwa, walipogundua kwamba walikuwa wakirushiwa mikuki bila kuwaona warushaji, wakaanza kukimbia kurudi garini. Mikuki ile iliendelea kurushwa zaidi na zaidi na kabla ya kufika mbali sana, mkuki mmoja ukamuingia Bwana Edward ubavuni mwake, akapiga uyowe mkubwa, akashindwa kukimbia, kama mzigo, akaanguka chini huku akilia kwa maumivu makali.

*****

Bwana Edward alikuwa akiendelea kulia kwa maumivu makali pale chini, mmoja wa mikuki ambayo ilikuwa imerushwa ulikuwa umemchoma ubavuni mwake na kuingia kwa zaidi ya sentimeta saba. Peter na Bwana Shedrack wakasimama, wasingeweza kuendelea na safari yao na wakati mwenzao alikuwa chni akiwa amepigwa na mkuki. Japokuwa mikuki ilikuwa ikirushwa na watu waliosadikiwa kuwa ni wavuvi, wakamchukua na kisha Peter kumbeba na kisha kuondoka mahali hapo.

Damu zilikuwa zikimtoka Bwana Edward ubavuni, shati jeupe ambalo alikuwa amelivaa lilikuwa limeloanishwa na damu katika sehemu kubwa sana. Walipolifikia gari lao, hawakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, walichokifanya ni Peter kushikilia usukani huku Bwana Shedrack akiwa na Bwana Edward huku akijaribu kumpoza poaza ndani ya gari lile.

Peter alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi, katika kipindi hicho tayari akili yake ilikwishamwambia kwamba alitakiwa kuelekea katika hospitali ya Mikocheni B ambayo wala haikuwa mbali kutoka katika sehemu hiyo. Japokuwa napo kulikuwa na kambi ya jeshi ambayo ilikuwa na hospitali lakini wakaona kuelekea mahali hapo lisingekuwa wazo zuri, hivyo walitakiwa kuelekea katika hospitali ya Mikocheni B.

Wala hawakuchukua muda mrefu wakafika katika hospitali hiyo, muda wote Bwana Edward alikuwa akilia kwa maumivu huku damu zikiendelea kumtoka ubavuni mwake, mkuki ule wenye ncha kali ulionekana kumchoma vilivyo jambo ambalo lilimwachia kidonda kikubwa sana ambacho kadri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo kilikuwa kikizidi kutoa damu zaidi na zaidi.

Bwana Shedrack akambeba na kisha kumtoa garini huku Peter pamoja na manesi wawili waliokuwa ne wakiivuta machela na kisha kumpandisha. Japokuwa alikuwa mwanajeshi, mtu ambaye alipitia aina nyingi za mafunzo lakini hakuweza kuyazuia macho yake yasitoe machozi katika kipindi hicho, alionekana kuwa kwenye maumivu makali sana kitu ambacho kilimfanya kulia muda wote.

Akafikishwa katika chumba husika na kisha daktari kuitwa na kuelekea katika chumba kile huku Bwana Shedrack na Peter wakiambiwa wasubiri nje katika mabenchi yaliyokuwa nje ya chumba kile. Kila mmoja alionekana kuwa kwenye hali isiyokuwa ya kawaida, kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika kipindi hicho hawakukitegemea hata kidogo, hawakutegemea kama kungekuwa na watu ambao wangewaona na kisha kufanya kile ambacho walikuwa wamekifanya.

Dakika zikazidi kwenda mbele kama kawaida lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alitoka ndani ya chumba kile jambo ambalo lilionyesha kwamba kulikuwa na kazi nzito ambayo ilikuwa ikiendelea ndani ya chumba kile. Saa la kwanza likakatika, saa la pili likakatika lakini bado mlango ule haukufunguliwa na mtu yeyote kutoka. Saa kumi na mbili kasoro asubuhi ndio ulikuwa muda ambao mlango wa chumba kile ukafunguliwa na kisha manesi kuanza kutoka na baada ya dakika kadhaa, dokta kutoka ndani ya chumba kile na kuwataka kumfuata ofisini kwake jambo ambalo wala hawakubisha, wakaanza kumfuata.

“Nini kimeendelea?” Bwana Shedrack aliuliza mara baada ya kukaa katika kiti ndani ya ofisi ile.

“Kitu gani kilitokea?” Dokta Pius aliuliza huku akimkazia macho.

“Kulitokea mapigano ya visu hapo Msasani Club na kwa bahati mbaya alikuwa amechomwa kisu na mtu ambaye alikuwa akipambana nae” Bwana Shedrack alimwambia.

“Kwa hiyo unataka kuniambia kwamba lile ni jeraha la kisu?” Dokta aliuliza.

“Yeah”

“Hapana. Lile si jeraha la kisu. Inawezekana ukawa mkuki. Hebu niambieni vizuri. Ukweli wenu ndio utakaomfanya mgonjwa wenu kupona zaidi” Dokta Pius aliwaambia.

“Huo ndio ukweli dokta”

“Basi hakuna tatizo. Kama ulikuwa ni ugomvi na kabla hatujaendelea na kitu chochote kile, ningependa kupokea PF3 kutoka polisi” Dokta Pius aliwaambia.

“PF3?”

“Ndio. Hiyo ndio inavyokuwa kila siku. Kukitokea mapigano na watu kujeruiwa huwa tunatakiwa kupokea PF3 kutoka kwao kabla ya kuanza matibabu. Sikuomba PF3 mwanzo kwa sababu mgonjwa alikuwa katika hali mbaya, alipoteza kiasi kikubwa cha damu. Naombeni PF3 kabla hatujaendelea” Dokta Pius aliwaambia huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema.

Kwanza kila mmoja akabaki kimya kwa muda, maneno ambayo aliyaongea Dokta Pius yalikuwa ni ukweli mtupu kwamba ni PF3 kutoka polisi ndio ambayo ilikuwa ikihitajika mahali hapo, kila mmoja akaonekana kunywea. Mara baada ya kubaki kimya kwa sekunde kadhaa, Bwana Shedrack akaona kwamba alikuwa na kitu ambacho alitakiwa kukifanya, yeye alikuwa mwanajeshi mwenye cheo kikubwa kwa hiyo aliamini kwamba kwa kupitia cheo chake, dokta angeweza kumuelewa. Alichokifanya ni kutoa kitambulisho chake cha kazi na kumpa dokta Pius ambaye alikichukua na kuanza kukiangalia.

“Nimekuelewa” Dokta Pius alimwambia huku akimrudishia kitambulisho kile.

“Kuna kitu gani kimeendelea?” Peter aliuliza.

“Lile jeraha ni la mkuki, mkuki uliingia sana katika ubavu wake, ukachana sehemu ambazo kuna nyamanyama kadhaa za kuzishikilia mbavu, mbaya zaidi mkuki huo ulikuwa umepakwa sumu, kwa hiyo sumu imeingia katika mwili wake” Dokta Pius aliwaambia maneno ambayo yakaonekana kuwashtua kupita kawaida.

“Sumu?”

“Ndio. Inaonyesha mkuki huo ulikuwa umepakwa sumu, tena sumu kali sana iitwayo Selphonipherioum ambayo kazi yake kubwa ni kuulia wanyama wakali kama simba na wengineo” Dokta Pius aliwaambia.

“Kwa hiyo ikawaje?”

“Tumehangaika kadri ya uwezo wetu na sasa hivi ndio tunaitoa sumu iliyokuwa mwilini mwake”

“Itamalizika leo?”

“Hapana. Ni kazi kubwa sana. Utoaji wa sumu unaweza kuchukua mwezi mzima”

“Mwezi mzima! Mungu wangu!”

“Yeah! Kazi ya utoaji sumu si kazi ndogo. Kama tukisema tufanye haraka haraka, inaweza kuleta tatizo kubwa zaidi kwa sumu ile kuingia katika utumbo mkubwa wa chakula na kisha kutapakaa katika tumbo zima kitu ambacho kitahitimisha maisha yake yote” Dokta aliwaambia.

Maneno ambayo aliyaongea dokta Pius yalikuwa ni ukweli kabisa. Sumu ile ilikuwa imeingia katika damu yake na hivyo ingechukua muda wa mwezi mmoja mpaka sumu ile kutolewa yote na matibabu mengine kufuata. Kuanzia siku hiyo, Peter pamoja na mama yake, Bi Stella wakawa ni watu wa kuelekea katika hospitali hiyo ambapo bado uchujaji wa sumu kutoka katika damu yake ulikuwa ukiendelea zaidi na zaidi.

Kila siku kwao zikaoekana kuwa na majonzi, Peter hakutaka kufanya jambo lolote katika kipindi hicho, akaamua kumsahau kwanza Rose kwa wakati huo na kutulia kuangalia hali ya baba yake ambayo wala haikuonyesha unafuu wowote ule. Siku zikakatika na hatimae mwezi kukatika na zoezi zima la uchujaji wa sumu kukamilika na matibabu mengine kuendelea.

“Sumu yote imekwisha” Dokta aliwaambia maneno ambayo yalionekana kuwa faraja kwao.

“Asante Yesu!”

“Ila bado kuna tatizo moja”

“Tatizo gani tena?”

“Sehemu ambayo mkuki uliingia ni sehemu mbaya sana, mkuki uliweza kuchanachana sana nyama zake, sijui kama kutakuwa na kitu cha kufanya zaidi, sehemu ile bado itaendelea kuwa na jeraha, damu bado itakuwa ikivilia kwa ndani” Dokta aliongea maneno ambayo yalikuwa kama sumu mioyoni mwao.

“Kwa hiyo hatoponana kurudi kama zamani?”

“Atapona ila bado jeraha litakuwepo. Cha msingi hatakiwi kufanya kazi ngumu na kutembea kwa muda mrefu” Dokta Pius aliwaambia.

“Ooopsss!” Peter alijikuta akishusha pumzi nzito.

Ilimchukua muda wa miezi mingine miwili na ndipo Bwana Edward kutoka hospitalini, bado alikuwa akihisia maumivu kwa ndani japokuwa kwa kumwangalia alionekana kuwa mzima wa afya. Kila siku akawa mtu wa kukaa ndani huku akipewa nafasi zaidi ya kupumzika kutoka kazini. Maumivu ya nyama zilizochanwa yalikuwa makubwa ubavuni mwake lakini hakuwa mtu wa kulia, alikuwa mtu wa kuvumilia maumivu yale tu.

“Unapakumbuka mahali alipopasema yule malaya?” Bwana Edward alimuuliza Peter.

“Napakumbuka. Alisema Kinondoni B”

“Yeah! Nenda kamtafute”

“Ila nitafanikiwa kweli? Kuna nyumba nyingi sana kule” Peter alimwambia baba yake, Bwana Edward.

“Kajaribu” Bwana Edward alimwambia Peter.

Hakukuwa na jinsi, katika kipindi hicho ndicho ambacho Peter akaanza kuelekea Kinondoni B kwa ajili ya kumtafuta Rose. Hilo halikuwa jambo dogo, lilikuwa jambo kubwa na zito, mara kwa mara Peter alikuwa akielekea huko lakini wala hakufanikiwa kumpata Rose. Mpaka miezi sita inakatika, bado hakuwa amefanikiwa katika suala hilo mpaka kufikia kipindi ambacho akaamua kukata tamaa kwa kuona kwamba kwa sababu msichana huyo alikuwa na mimba yake, angeweza kumtafuta.

Peter akasahau kila kitu, mwaka wa kwanza ukakatika, wa pili, wa tatu mpaka mwaka wa tano unaingia, bado Peter alionekana kutokujali, alikuwa akiisubiri siku ambayo Rose angeweza kuja na kumwambia mengi kuhusiana na mtoto wake.

Katika kipindi hiki, matatizo mengine yakaonekana kuanza kutokea, katika kipindi cha miaka miwili ya nyuma Bwana Edward alijiona kuwa kama zamani jambo ambalo lilimfanya kuanza kupuuzia yale dokta aliyokuwa ameshauri. Akaanza kutembea kwa umbali mrefu huku akifanya kazi ngumu kama kawaida yake.

Tatizo likaonekana kuanza tena, katika kipindi hiki kila kitu kikaonekana kuwa kama zamani. Muda mwingi Bwana Edward alikuwa akilalamikia maumivu, alikuwa amezitonesha nyama zake mbavuni jambo ambalo lilikuwa likimletea maumivu makali kupita kawaida. Kila siku alikuwa akilia peke yake, mpaka walipoamua kumpeleka hospitalini, walikuwa wamechelewa kwani damu zilikuwa zimekwishaanza kuvilia tumboni mwake.

“Mbona mmemchelewesha namna hii?” Dokta Pius ambaye alimtibia miaka mitano iliyopita aliwauliza.

“Kwani imekuwaje?”

“Damu zimeanza kuingia tumboni mwake. Nadhani alipuuzia ushauri wangu na tatizo kurudi tena, limerudi kwa kasi zaidi” Dokta Pius aliwaambia.

Kila mmoja alionekana kushtuka, maneno ambayo aliyaongea dokta Pius yakaonekana kuwatisha kupita kawaida, kwa kifupi maneno yale yalimaanisha kwamba Bwana Edward asingeweza kupona na kuwa kama zamani, ni lazima angekufa. Dokta Pius hakutaka kumkatisha tamaa mgonjwa wake, kila siku alikuwa akimtibia na kumtia moyo japokuwa moyoni alijua kwamba mgonjwa wake muda wowote alikuwa akienda kufa kitandani kutokana na damu kuanza kuingia tumboni.

“Peter….” Bwana Edward alimuita Peter ambaye alikuwa pembeni yake.

“Naam”

“Mjukuu wangu ana miaka mitano sasa. Ninataka kumuona mjukuu wangu kabla sijafariki” Bwana Edward alimwambia Peter kwa sauti ya chini.

“Baba…nimemtafuta sana Rose kwa miaka yote hii sijampata” Peter alimwambia.

“Haijalishi Peter. Ninataka kumuona mjukuu wangu kabla sijafa. Tumia fedha, tumia bunduki, ua au mjeruhi mtu, ninachokitaka ni kumuona mjukuu wangu tu” Bwana Shedrack alimwambia Peter.

“Nitampatia wapi?”

“Kaanze kule kule ulipoambiwa. Fanya juu chini mpaka namuona mjukuu wangu hapa hospitalini” Bwana Shedrack alimwambia Peter.

“Kama Rose akikataa?”

“Usimpe taarifa. Hata kama kumteka, wewe mteke tu. Ninachikitaka ni kumuona mjukuu wangu tu. Mtafute kila kona, nataka kumuona hata kabla sijafa” Bwana Edward alimwambia Peter.

“Nitafanya hivyo baba. Nitakuja na mjukuu wako mahali hapa” Peter alimwambia baba yake na kisha kuondoka mahali hapo.

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane Jumamosi.

Leave A Reply