The House of Favourite Newspapers

Kahata: Lazima tuwafunge UD Songo

WAKATI kikosi cha Simba, keshokutwa Jumapili kikitarajiwa kushuka uwanjani kucheza dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa timu hiyo, Mkenya, Francis Kahata amewatangazia hali ya hatari wapinzani wao hao.

 

Simba itapambana na UD Songo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Awali.

 

Timu hizo zilipokutana Msumbiji katika mchezo wa kwanza, matokeo yalikuwa suluhu, hivyo Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote ili iweze kusonga mbele.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa kuhusiana na mchezo huo, Kahata alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo kwa njia yoyote ili waweze kusonga mbele katika mchuano hiyo.

 

Kahata amewataka Wanasimba wote kujua kuwa mchezo huo kwao ni kama fainali, hivyo ni lazima wawe kitu kimoja ili kuhakikisha timu hiyo inaibuka na ushindi. “Sina muda mrefu tangu nijiunga na Simba lakini ndoto yangu ni kutaka kuiona inafika mbali zaidi katika mchuano ya kimataifa na kwa kuanza tunatakiwa kushinda mchezo wetu wa Jumapili dhidi ya UD Songo.

 

“Wachezaji tutakuwa uwanjani tukipambana lakini mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kutuunga mkono kwani uwepo wao uwanjani unatufanya tupambane zaidi,” alisema Kahata.

Comments are closed.