The House of Favourite Newspapers

Kalengo atoa kauli ya kutisha

STRAIKA mpya wa Yanga raia wa Zambia, Maybin Kalengo, ametoa vitisho kwa mabeki wa timu pinzani baada ya kusema kuwa yupo Yanga kwa ajili ya kufunga mabao, hivyo hatatishika na beki yeyoye kwenye Ligi Kuu Bara na mashindano yote ambayo kikosi chake kitashiriki.

 

Baada ya kukaa nje kwa takriban wiki moja akiuguza majeraha ya kifundo cha mguu, jana asubuhi straika huyo alianza mazoezi mepesi.

 

Kalengo amejiunga na Yanga hivi karibuni akitokea Zesco FC ya Zambia, lakini tangu amejiunga na kambi ya Yanga amejikuta akikaa nje kwa takriban wiki moja kufuatia kuwa na majeraha kwenye kifundo chake cha mguu.

 

Straika huyo ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao wanatarajiwa kutambulishwa Agosti 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar katika Tamasha la Siku ya Mwananchi ambapo watacheza na AS Vita ya DR Congo.

 

Kalengo alisema kwa kuwa ameanza mazoezi ana imani kubwa ya kuwepo kwenye mchezo wao na AS Vita.

 

“Natamani sana siku hiyo ya tamasha la kilele cha Siku ya Mwananchi nipate nafasi ya kucheza, hivyo namuomba Mungu anijalie uzima ili niweze kuonyesha nilichonacho.

 

“Mbali na hilo, mimi ni mshambuliaji, hivyo suala la kufunga kwangu sio la kuuliza, nitafunga bila ya kumhofia beki wa aina yoyote,” alisema Kalengo.

Comments are closed.