The House of Favourite Newspapers

Kama hamuwezi kuachana bora liserereke

0

divorceNi Jumanne tena imefika huku ‘oyaoya’ za kampeni za uchaguzi mkuu zikiwa zimepamba moto kote nchini. Kila mgombea anaomba kura, lakini tusikilize sera zao badala ya kufuata ushabiki tu.

Mada yangu ya leo ni; KAMA HAMUWEZI KUACHANA, BORA LISEREREKE! Mada hii inabidi kuisoma kwa upana zaidi ili kuilewa vinginevyo kwa juujuu unaweza kusema ninachochea kuvunjika kwa uhusiano.

Nimefuatilia sana na kubaini kuwa, kwa hapa nyumbani Tanzania, wawili waliopendana wakiachana hutengeneza uadui wa kutosalimiana au kuwa chanzo cha hata kupelekana polisi au mahakamani.

MKIPENDANA KWA DHATI

Hii yote husababishwa na nafsi kutokubaliana na maamuzi hayo. Wengi hawajui kwamba, mnapopendana sana, kwa mapenzi ya dhati, kuachana kwenu hakuwezi kuwa na amani hata siku moja.

Ukikuta watu wanasemeana maneno machafu kila wakikutana na walikuwa wapenzi, tambua upendo wao ulikuwa wa dhati. Nafsi inakataa kuachana lakini ikatokea, kwa visa au kwa nguvu ya ushawishi kutoka kwingine.

KUNDI NINALOLIZUNGUMZIA

Ukiacha kundi hilo la kuachana kwa uadui, lakini pia kuna kundi la wapendanao kwa dhati kiasi kwamba inapotokea mgogoro wa kusababisha kuachana, hakuna aliye tayari kwa kutengana. Kundi hili huishi maisha ya shida sana katika uhusiano kwa vile kila mmoja anaona hawezi kuishi bila mwenzake. Hawezi kusema hadharani wala kukiri kwa mwenza wake lakini ndani ya nafsi anajijua.

WASIO KATIKA NDOA

Sasa kwa wale wasio kwenye ndoa, yaani kila mmoja anaishi kwake, inapotokea hali hii ya kushindwa kuachana, huweza kuendelea kuwa katika uhusiano wa polepole wakiliacha penzi lao kuserereka mpaka siku moja kuja kukatika kabisa na kila mmoja kuendelea na maisha yake.

Watu hawa, hata kama walipendana kwa dhati lakini hawawezi kuja kuwekeana uadui baada ya penzi kufa kuliko wale ambao walishindwa kuachana lakini ikabidi waachane ghafla.

WALIO NDANI YA NDOA

Kundi hili linakabiliwa na kuzalisha watoto wa mitaani, kwani wanapotokea kupendana kwa dhati, wakafunga ndoa, wakazaa, wakija kuachana kwa ghafla huku nafsi haitaki, uadui hujengeka na matokeo yake ni watoto kususwa au kutelekezwa.

Nilipenda sana mada yangu izungumzie kwa kina kundi hili. Kwamba, kama mmefunga ndoa mkiwa ndani ya upendo wa dhati, ukatokea mgogoro mkubwa kiasi kwamba, kila mmoja nafsi ikamwambia afadhali kuachana lakini mkashindwa, ni bora mkaacha uhusiano wenu userereke tu, yaani muwe mpompo kwa faida ya watoto.

Lakini pia watu wa kundi hili waliojikuta bora liserereke wengi walifanikiwa kuurudisha upendo upya na maisha yakawa ya furaha kuliko awali kushinda wale walioachana ghafla ambao wengi wao hujikuta katika uhusiano mpya na wanaoumia ni watoto.

Mnaposhindwana sana na kuamua bora uhusiano userereke husaidia kuendelea kujengeana heshima ya woga na ndiyo msingi wa kuweza kurejesha uhusiano kama mwanzo. Kama mnatoka nyumba moja, bado kila mmoja atajihesabia kuwa ni mtu wa mwenzake kuliko mkiachana ghafla na kutawanyika, hesabu itakuwa ni ‘kwani mi ni mtu wake?’

Wanandoa wakiachana, kila mtu akaenda kuishi kwake, haiwezekani mmoja akimwona mwenzake mahali penye shaka akamtumia meseji kumuuliza ‘hapo unafanya nini muda huu?’

Lakini mkiacha liserereke huku mnatokea nyumba moja, ukimwona mwenzako mahali pa hivyo, unaweza kumuuliza naye akakujibu kwa mshtuko kwamba amenaswa sehemu si sahihi.

Kwa hiyo mimi naamini kuna faida kubwa ya walio kwenye mgogoro wa kimapenzi huku wanapendana kwa dhati kuacha uhusiano userereke kuliko wanaokata ghafla na kila mmoja kushika njia yake ambapo huzua uadui.

Leave A Reply