The House of Favourite Newspapers

Kama Unataka Kufanikiwa, Lazima Uchague Watu Sahihi

0

NI siku nyingine tunapoendelea na maombolezo ya kifo cha Hayati Dk. John Pombe Magufuli! Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi na ampe nguvu mjane wake, mama Janet Magufuli, watoto wake na familia kwa jumla.

 

Wakati tukiendelea na maombolezo, kuna jambo nataka kuzungumza na wewe msomaji wangu kupitia ukurasa huu, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kila wiki.Ndugu zangu, wapo watu ambao mpaka leo wanaendelea kulalamika kwenye maisha yao, wanawalaumu watu wengine kwamba ndiyo waliowakwamisha kufikia malengo yao maishani mwao.

 

Utakuta mwanaume analalamika, yaani huyu mwanamke tangu nimuoe, mambo yangu yanakwama kila kukicha! Unakuta mwanamke naye analalamika, yaani tangu niolewe na huyu mwanaume, kila siku maisha yangu yanazidi kuwa magumu.

Mwingine unakuta analalamika kwamba marafiki zake ndiyo chanzo cha yeye kufilisika, kuwa mlevi, kuwa na tabia mbaya na kadhalika! Ukitazama ni kweli, Waswahili wanasema ndege wa rangi moja huruka pamoja.

 

Ukiwa na marafiki wenye tabia za ulevi lazima na wewe utakuwa mlevi, ukiwa na marafiki wanaopenda kusengenya na kuwasema wengine vibaya, lazima na wewe utaanza kuwa kama wao, na kama unaishi na mume au mke ambaye kazi yake ni kukukatisha tamaa na kuonesha kwamba huwezi kufanya kitu chochote, asiyekuunga mkono katika unachokifanya, lazima maisha yako yatapoteza mwelekeo tu.Kwa watu ambao wananifahamu kabla sijawa Shigongo huyu unayemjua leo, nilikuwa na maisha ya tofauti kabisa, kipindi hicho nikiwa huko machimboni.

 

Aina ya marafiki niliokuwa nao, pengine kama ningeendelea kuwa nao mpaka leo, ningekuwa mtu tofauti kabisa.

Pengine na mimi ningekuwa nakunywa pombe za kienyeji, nakesha kwenye vilabu vya pombe na tabia nyingine ambazo kamwe zisingeweza kunifikisha hapa nilipo.

 

Nilipogundua kwamba nimezungukwa na watu wasio sahihi, ambao kila wanaponiona basi wanategemea mimi ndiyo wa kuwatatulia shida za, lakini ninapokuwa na matatizo, simuoni hata mmoja, niliamua kufanya mabadiliko.

 

Niliamua kubadilisha aina ya marafiki, nikaachana na marafiki zote wa zamani niliowaona kama kikwazo kwangu na kuanza kupata marafiki wapya.

Hata hivyo, kabla sijaanza kupata marafiki wapya, nilijiwekea nadhiri ya kuwa mtu mpya, nikaachana na mambo yote ya kidunia na ujana na ndani ya muda mfupi tu, nilianza kuona mabadiliko.

 

Mabadiliko hayo ndiyo yaliyonifikisha hapa nilipo leo! Kama nisingeamua kufanya mabadiliko, hata sijui leo ningekuwa mtu wa aina gani!

Kila ninapopata muda wa kuonana na wale marafiki zangu wa kipindi hicho, roho inaniuma sana kwa sababu wameendelea kubaki vilevile, na wengine wamechakaa zaidi na kuzeeka kuliko mimi wakati wengine ni wadogo kwangu.Ndugu zangu, kila mmoja wetu anao marafiki na watu wanaomzunguka. Hao ndiyo wanaoweza kutoa tafsiri sahihi ya yeye ni mtu wa aina gani.

Upo msemo mmoja wa zamani ambao asili yake naambiwa ni nchini Hispania, unaosema ‘Tell me who are your friends, and I’ll tell you who you are’ ukiwa na maana kwamba ‘Nioneshe marafiki zako na nitakwambia wewe ni mtu wa aina gani’.

Usemi huu unapewa nguvu na tafiti nyingi za wataalam wa masuala ya uhusiano ambao wanaeleza wazi kwamba unapokuwa na ukaribu na watu wa aina fulani, taratibu utajikuta na wewe unaanza kufanana nao na mwisho utafanana nao kabisa.Wapo watu wengi ambao wamewahi kuonywa, kwa mfano ‘usipende kuwa karibu na mtu fulani, atakufundisha tabia mbaya’ lakini kwa ubishi wao, wakaendelea na ukaribu huo, mwisho hata wenyewe hawakujua ni lini walianza kubadilika lakini wakajikuta tayari wanafanana na wale waliokuwa karibu nao.

 

Ukitaka kujua kama watu waliokuzunguka ni sahihi au siyo sahihi kwako, fanya zoezi hili jepesi, chukua simu yako kisha anza kutazama majina ya watu waliopo kwenye ‘phonebook’ yako, kisha jiulize mwenyewe ni nani ambaye amekuwa msaada kwako kwenye matatizo yako?

 

Ukikuta watu waliojaa kwenye simu yako ni wale marafiki mnaokutana baa au kwenye starehe, wale mnaoshinda nao vijiweni mkipiga stori za wanawake au wanaume, wale ambao mkikutana kazi ni kujadili maisha ya watu wengine, tambua kwamba umezungukwa na watu wasio sahihi.

 

Yawezekana ukawa na marafiki wengi ambao mmedumu kwa miaka nenda rudi lakini hakuna kitu chochote cha maana ambacho umekuwa ukikipata kutoka kwao, ndugu yangu, kama unataka kufanikiwa, achana nao.

 

Mtu mmoja amewahi kuniuliza swali nikiwa nafundisha kuhusu somo hili, kwamba sasa kama mume wangu ndiyo amekuwa chanzo cha kunikwamisha nifanye nini? Sipo hapa kuvunja ndoa au uhusiano wa mtu lakini unatakiwa kutafakari mwenyewe.

 

Kama mume wako ndiyo amekuwa mstari wa mbele kukukwamisha, pengine alikuoa ukiwa na ‘certificate’ ya taaluma fulani, kila ukimwambia baba nataka nikasome nipate diploma, anakukatisha tamaa kwamba ‘diploma ya kazi gani, kuna watu kibao mtaani wana diploma na hawana chochote cha maana, unapaswa kuelewa kwamba huyo siyo mume sahihi.

Una diploma, unamwambia nataka nikapate digrii, anaishia kukwambia mbona fulani na fulani wana digrii lakini wapo tu mitaani, hakika huyo hakufai! Nasema tena kwa herufi kubwa, hata kama ni mumeo au mkeo, hakufai huyo.

 

Mtu sahihi ni yule anayejitahidi kukuinua kutoka pale alipokukuta kwenda mbele, ambaye anakushauri vizuri bila kukukatisha tamaa au kukukosoa kwa maneno mabaya, mtu ambaye anajivunia mafanikio yako.

Wapo marafiki wengine ambao unaweza kuwa na wazo fulani ndani ya kichwa chako, lakini ukimshirikisha tu, lazima akukatishe tamaa.

Unaweza kumwambia nimefikiria kufungua duka la samaki, akaishia kukwambia ‘unajua samaki huwa wanaoza? Sasa wakioza si mtaji wote utapotea?

 

Ukimwambia nimefikiria kuanzisha kilimo cha matikiti, anaishia kukwambia unajua kuna nguruwe wanakula sana matikitiki, utapata hasara! Huyo hapaswi kuwa kwenye ‘circle’ ya watu wanaokuzunguka.Sasa swali la msingi ambalo watu wengi wamekuwa wakiniuliza, ni kwamba ‘nitawezaje kuachana na marafiki ambao nimezoeana nao na kupata marafiki wapya?’ Jibu ni rahisi sana, anza wewe kwanza kubadilika.Bila shaka kila mmoja anaijua sumaku! Umewahi kuona sumaku inavuta mbao?

 

La hasha, sumaku inavuta vitu vya chuma pekee. Ili kuwavuta watu sahihi katika maisha yako kama sumaku inavyofanya, ni lazima uanze kwa kubadilika wewe mwenyewe.Ukikaa peke yako, jiulize kuhusu mwenendo wa maisha yako.

 

Jiulize utaendelea kulewa mpaka lini? Utaendelea kufanya starehe na anasa mpaka lini? Ukiona inatosha sasa, wakati wa kubadilika ni sasa na utakapoanza kubadilika tu, utashangaa hata wale marafiki wasiofaa wanajiondoa wenyewe.Kama marafiki zao mlikuwa mkiunganishwa na ulevi kwa mfano, ukiamua kuachana na ulevi, moja kwa moja marafiki hao watajitenga na wewe!

 

Ukiamua kuanza kufanya biashara, hata kwa mtaji mdogo, utajikuta unapata marafiki wapya ambao ni wafanyabiashara wenzako, wakubwa kwa wadogo.

Kama ulikuwa ni mtu wa anasa na starehe, utakapoamua kuachana na maisha hayo, wale marafiki mliokuwa mkiongozana kwenye kumbi za sterehe, taratibu wataanza kujiengua, mmoja baada ya mwingine. Ukiamua kumrudia Mungu wako, utajikuta unapata marafiki wapya, ambao wanafanana na zile tabia mpya ulizoanza kujijengea.

 

Hujachelewa, wakati wa mabadiliko ni sasa na nikupe siri nyingine inayoweza kukusaidia kufanikiwa kwa haraka zaidi? Penda kujenga urafiki na watu ambao wamekuzidi katika kile unachokifanya. Kama wewe ni mfanyabiashara, basi ‘jipendekeze’ kwa wafanyabiashara wakubwa, wakati mwingine omba kukutana nao na kubadilishana nao mawazo, inasaidia sana.

 

Mimi mwenyewe nikikupa simu yangu utazame kwenye ‘phonebook’ yangu, utakutana na majina ya wafanyabiashara wengi walionizidi. Wakati mwingine naweza kumpigia simu mtu aliyenizidi, nikaomba tu kukutana naye, najua hata kama tutakaa na kunywa kahawa tu, kuna mambo nitayapata kutoka kwake.Sisemi kwamba tusiwe na marafiki ambao tumewazidi mafanikio, la hasha!

 

Ninazo namba nyingi pia za watu ambao nimewazidi lakini ninachokifanya kila siku, ni kuwajengea hamu ya kufanikiwa, yaani wakinitazama waseme siku moja natamani kuwa kama Shigongo. Kwa mfumo huo nimekuwa nayabadilisha maisha ya watu wengi, wakati mwingine bila hata kujua.

 

Watu wengi wananitazama kama ‘role model’ wao na kwa kulitambua hilo, najikuta kila siku nikiwa na ari kubwa ya kufanya mambo makubwa ili wale wanaonitazama kama kioo, waendelee kujifunza kutokea kwangu.Utakapoweza kubadlisha aina ya marafiki wanaokuzunguka, utakapoanza kujihusisha na watu waliofanikiwa, hakika na wewe utafanikiwa lakini ukiendelea kuwakumbatia marafiki wasiofaa, kila siku utaendelea kuwa ni mtu wa kuwalaumu wengine wakati nguvu ya mabadiliko unayo ndani yako.Ahsanteni kwa kunisoma, Mungu awabariki wote.

DIARY yaShigongo

Leave A Reply