The House of Favourite Newspapers
gunners X

Kamala Harris Amshambulia Donald Trump Kufuatia Kukamatwa kwa Maduro

0
Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani, Kamala Harris

Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani, Kamala Harris, amemshambulia vikali Rais Donald Trump kufuatia uamuzi wa serikali ya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro na mke wake, akieleza hatua hiyo kuwa “kinyume cha sheria na isiyo na busara.”

Maduro na mke wake waliwasili mjini New York Jumamosi, Januari 3, ili kukabiliana na mashtaka ya shirikisho yanayohusiana na biashara ya dawa za kulevya na ushirikiano na makundi ya uhalifu yaliyotangazwa kuwa ya kigaidi. Rais huyo wa Venezuela amekanusha vikali tuhuma zote dhidi yake.

 

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Harris amesema uamuzi wa Trump haujasaidia usalama, nguvu wala ustawi wa wananchi wa Marekani.

“Hatua za Donald Trump nchini Venezuela haziifanyi Marekani kuwa salama zaidi, imara zaidi wala nafuu zaidi kiuchumi,” ameandika Harris.

“Kwamba Maduro ni dikteta katili na asiyehalali hakubadilishi ukweli kwamba kitendo hiki ni kinyume cha sheria na hakina busara.”

Ameongeza kuwa historia inaonesha hatua kama hizo huishia kusababisha machafuko badala ya suluhu.

“Tumeshaona filamu hii hapo awali — vita vya kubadilisha tawala au kupigania mafuta vinavyouzwa kama ishara ya nguvu, lakini huishia kuleta machafuko, na familia za Wamarekani ndizo hulipa gharama,” amesema.

Harris amesisitiza kuwa hatua hiyo haikulenga kupambana na biashara ya dawa za kulevya wala kulinda demokrasia, bali maslahi ya kiuchumi na kisiasa.

“Hili si suala la dawa za kulevya wala demokrasia. Ni suala la mafuta na tamaa ya Donald Trump kujionesha kama kiongozi mwenye nguvu katika ukanda wa Amerika ya Kusini,” aliongeza.

Alimshutumu Trump kwa kutoa msamaha kwa watu waliopatikana na hatia ya biashara ya dawa za kulevya huku akidai kuhalalisha hatua kali dhidi ya Maduro.

“Iwapo angejali kweli masuala ya dawa za kulevya au demokrasia, asingemsamehe mfanyabiashara wa dawa aliyepatikana na hatia, wala asingelitenga pembeni upinzani halali wa Venezuela huku akifanya mikataba na washirika wa Maduro,” amesema Harris.

Harris pia ameonya kuwa uamuzi wa Trump unaweka maisha ya wanajeshi wa Marekani hatarini, unaigharimu nchi mabilioni ya dola na kuleta msukosuko katika eneo hilo.

Leave A Reply