testiingg
The House of Favourite Newspapers

Kamanda Muliro Atoa Tahadhari Ya Kiusalama Mchezo wa Soka Kati ya Simba na Yanga Leo

0

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatambua kuwa leo Jumapili, Novemba 05, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam kutakuwa na mchezo wa soka mashindano ligi ya NBC baina timu ya Simba na Yanga zote za Jijini Dar es Salaam .

Mchezo huo utaochezwa saa 11 jioni hivyo Jeshi la Polisi linatambua mchezo huo utakuwa na mvuto wa hali ya juu, hivyo kutakuwa na
mkusanyiko mkubwa wa mashabiki wa soka wa timu hizo katika kiwanja hicho kutokana ushindani wa timu hizo. Kwa kulitambua hilo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama limechukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo huo.

Ukaguzi wa hali ya juu utafanywa katika milango ya kuingia na hairuhisiwi mtu yeyote kwenda uwanjani na silaha ya aina yoyote, isipokuwa baadhi ya vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.

Asiyekuwa na tiketi hataruhusiwa kusogelea uwanja huo au maeneo ya milango ya kuingia. Tahadhari zote za kiusalama zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na baadhi ya barabara chache kufungwa ili kupunguza msongamano wa kuelekea na kutoka uwanjani siku hiyo. Jeshi linashauri mashabiki wa soka wafike mapema ili kuepusha usumbufu wa kuingia uwanjani kwani milango ya uwanja huo itafunguliwa kuanzia saa nne (4) asubuhi.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawatahadharisha baadhi ya mashabiki wenye tabia chafu zisizo za maadili kujiepushasha nazo kwani majukwaani watakuwepo makachero ambao watakuwa wakifuatilia kwa karibu vitendo vyote vya hovyo na baada ya mchezo watakaohusika na makosa hayo watakamatwa ili kukomesha tabia ambazo sio za kistarabu kwenye viwanja vya soka. Jeshi la Polisi linawatakia mashabiki wa soka na timu zao kila kheri.
Imetolewa na;
Muliro J. MULIRO – SACP
Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam

Leave A Reply