The House of Favourite Newspapers

Kamanda Muliro Awataja Matapeli Wanatumia Jina La Spika Tulia – Video

0
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP. Muliro J. Muliro

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na kikosi kazi maalum cha kuzuia na kupambana na matumizi ya makosa ya kimtandao kimeendelea na kazi ya Ufuatiliaji  na kufanikiwa kwa mara nyingine  kuwakamata Claudian Makaranga (28) mkazi wa Kawe, Kinondoni na Hongliang Yang (35) Mchina, mkazi wa Kigamboni, kwa tuhuma za kuingiza vifaa vya mawasiliano ya intanet nchini bila kufuata utaratibu wa kisheria vyenye jina la STARLINK KIT/DEVICE.

Watuhumiwa hao wamekuwa wakijitangaza kuuza vifaa na kutoa huduma ya internet nchini kupitia mtandao ya kijamii wa Instagram kwa akaunti yenye jina la STARLINK.
Baadhi ya vifaa vilivyoingizwa nchini imebaika  vilishauzwa na kutumika katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kitendo ambacho ni kosa na  kinyume na sheria kwani havijaidhinishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Vifaa vilivyokamatwa ni Starline Dish 12, Starlink Router 12.

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imetoa wito kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya vifaa vya mawasiliano, ambavyo havijaidhinishwa na mamlaka husika.
Pia amekamatwa mtuhumiwa Wilfred Werandumi (44),  Mkazi wa Tungi,  Morogoro na Abdulrahim Mwakibinga (30), Mkazi wa Mwandege, Morogoro kwa kutumia majina ya Viongozi mbalimbali wa nchi kutapeli watu ,kwa kujifanya wanaomba michango ya harusi, misiba na matibabu.
Baadhi viongozi ambao majina yao yametumika katika utapeli huu ni Mh. Dr. Stergomena Tax, Mhe. Innocent Bashungwa, Mhe. Mohamed Nchengerwa, Mhe. Eng. Hamadi Masauni, na Katibu Mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo.

Vilevile amekamatwa pia Salum Kingu (25) mkazi wa Mbalizi, Mbeya na Loveness Silonga (24) mkazi wa Mbalizi, Mbeya kwa tuhuma za kutumia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook yenye jina la Kopa Faster Tulia Trust Foundation na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali kwa kudai kuwa wanatoa mikopo kwa masharti nafuu na haraka wakitumia namba ya simu 0749 704445.
Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji mkali wa tabia hizi na watuhumiwa wote watashughulikiwa vikali kwa mujibu wa sheria.

Leave A Reply