The House of Favourite Newspapers

Kampuni ya Fast-Jet Kujiondoa Katika Soko la Tanzania Hi

Shirika la Ndege la Fastjet linatarajia kuondoka katika soko la Tanzania, baada ya kujiendesha kwa hasara kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo ushindani kutoka Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), changamoto za kisheria, na uwezo wake wa kukusanya fedha.

 

Kampuni ya Fastjet Plc iliyoorodheshwa katika soko la hisa la London, nchini Uingereza inatarajia kuuza hisa zake asilimia 49 katika Shirika la Ndege la Fastjet Tanzania kutokana na changamoto kubwa za kibiashara.

 

Kuondoka kwa Fastjet Plc ndani ya Fastjet Tanzania kutaliacha shirika hilo (Fastjet Tanzania) na uwezo mdogo wa kushindana na ATCL, ambayo imeanza kwa kasi kufufua upya shirika hilo.

 

Fastjet imeeleza kuwa, changamoto za mazingira ya kufanyia biashara na ushindani wa ATCL ndio changamoto kubwa ambazo mmiliki mpya atakabiliana nazo katika kuhakikisha shirika hilo linatengeneza faida. Baada ya serikali kununua ndege nne mpya, imeongeza ushindani mkubwa kwa Fastjet kwani imekuwa ikifanya safari katika maeneo Fastjet ilikuwa ikifanya, na hivyo kupunguza wateja.

 

Fastjet imeeleza kuwa imekuwa ikipata changamoto kubwa katika safari za Dar es Salaam-Mwanza na Dar es Salam-Kilimanjaro baada ya ATCL kuanza kutumia ndege yake mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 262.

 

Changamoto za kisheria ambazo shirika hilo limeeleza kukumbana nazo ni pamoja na kuchukua muda mrefu kwa ndege zake mpya tatu aina ya ATR72-600 kuruhusiwa kuanza kufanya kazi. Hatua hiyo inafanya wazidi kuingia gharama za kutunza ndege hizo wakati hazifanyi kazi.

 

“Hakuna dalili changamoto hizi zitamalizika lini. Kulikuwa na changamoto za uingizwaji wa ndege mpya za ATR72-600, pamoja na kibali cha safari za ndani kwa ajili ya ATR72-600 na ERJ190 ambacho kwa miezi kadhaa sasa bado hakijapatikana, na hii imeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kampuni.”

 

Aidha, Fastjet imesema kuwa itakodisha ndege hizo, kuliko kufanyia biashara katika anga la Tanzania.
Kuanzia Januari hadi Juni 2018, Fastjet ilisafirisha abiria 201,000 ambapo safari kati ya Dar es Salaam na Mwanza, ndizo zilikuwa na abiria wengine zaidi.

 

Lakini idadi hiyo ya abiria ilipungua kwa asilimia 9, kutokana na kubadilishwa ndege ya safari kutoka Airbus A319 yenye uwezo wa kubeba abiria 144 na kutumia Embraer190s yenye uwezo wa kubeba abiria 104.

WIZARA YA NISHATI Yaja Kivingine, Yataja Mradi Mkubwa

Comments are closed.