The House of Favourite Newspapers

PUMA YATUMIA KLABU YA WANAFUNZI KUTOA ELIMU YA USALAMA BARABARANI

Baadhi ya wanafunzi ambao ni mabalozi wa usalama barabarani wakitoa elimu kwa madereva waliofika kwenye Kituo cha Mafuta cha Puma kilichopo Upanga jijini Dar es Salaama kuweka mafuta.
Wakitoa elimu waliyoipata kutoka Taasisi ya Amend  juu ya usalama barabarani. 
Hali ilivyoonekana.

KLABU ya Usalama barabarani ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Bunge wametoa elimu ya usalama wa barabarani kwa madereva wa magari na bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani haswa vivuko vya watembea kwa miguu ili kuepusha ajali na vifo.

 

Pia wametoa elimu,  zawadi ya madaftari, kalenda na mabegi ya shule yenye jumbe mbalimbali zinahusu masuala ya usalama barabarani kwa madereva mbalimbali kama sehemu ya kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inafika kila mahali.

Wanafunzi hao 18 ambao ni mabalozi wa usalama barabarani kutoka kwenye Klabu hiyo wametoa elimu hiyo na zawadi hizo Novemba 10, 2018 wakiwa kwenye Kituo cha Mafuta cha Puma kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam ambapo madereva waliofika kuweka mafuta walikuwa wakipewa elimu hiyo inayohusu usalama barabarani.

Akizungumza wakati wa utoaji elimu kwa madereva, Rosenice Senyandumi ambaye ni Mwanafunzi wa shule hiyo amesema ajali za barabarani zimekuwa zikikatisha uhai wa binadamu wasio na hatia wakiwemo wanafunzi na mara nyingi huchangiwa na madereva wazembe.

“Ajali za barabarani zinapunguza nguvu kazi ya Taifa na kuathiri watoto kwa kuwa wengi hupoteza wategemezi wao na wakati mwingine watoto wenyewe kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali,” amesema.

Mwanafunzi huyo amesema kutokana na athari na madhara yanayotokana na ajali Kampuni ya mafuta Puma nchini Tanzania kupitia programu yake ya Usalama Barabarani imeamua kutoa elimu ya usalama kwao kupitia Shirika ka Amend ambao jukumu lao kufundisha wanafunzi na wadau wengine kuhusu umuhimu wa usalama na kisha wao kama mabalozi wa elimu hiyo nao wanaitoa kwa wengine.

Amefafanua imebainika  asilimia kubwa ya ajali za barabarani huchangiwa na uzembe wa madereva na visababishi ni pamoja na ulevi wakati wa safari, uchovu, matumizi ya simu wakati wa kuendesha na kutozingatia alama za barabarani, hivyo wameamua kutoa elimu hiyo kama wanafunzi ili kuhakikisha tatizo la ajali za barabarani linakoma.

Kwa upande wake, Kassim Juma ambaye ni dereva aliyepatiwa elimu ya usalama wa barabarani na kupewa zawadi ya begi la shule na kalenda amesema wanafunzi hao wameonesha uzalendo na wanapaswa kuungwa mkono ili kuwafikia madereva wengi zaidi na kuwapatia elimu ya usalama wa barabarani.

“Nawapongeza hata walioanzisha wazo la kuwawezesha wanafunzi hawa kutoa elimu kwa kuwa tunafahamu kwamba misingi bora ya elimu huanzia chini, hivyo watoto hawa watakuwa ni mabalozi bora wa vizazi vijavyo,” amesema.

Awali Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania, Dominic Dhanah amesema kampuni hiyo imedhamiria kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika masuala ya usalama barabarani ili kudhibiti ajali.

Amesema mwaka 2013 baada ya kugundua kwamba watoto wapo hatarini zaidi walianza kutoa elimu ya usalama wa barabarani katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Geita na Ruvuma na mwaka juzi walianzisha klabu ya usalama wa barabarani katika shule ya msingi Bunge.

“Tunahitaji kuwa na jamii ambayo inaheshimu sheria za usalama barabarani, na kwa kupitia wanafunzi hao ambao wamepewa elimu ya usalama barabarani wamekuwa wakieneza elimu hiyo kwa wadau wengine kuhakikisha sote kwa pamoja tunapunguza ajali za barabarani,” amesema.

Wakati huo huo Meneja wa Usalama Kazini wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Boniface Menchi amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa shule ambazo zipo hatarini zaidi zilizopo pembezoni mwa barabara.

Comments are closed.