The House of Favourite Newspapers

KANGI LUGOLA ASHTUKIWA!

Waziri Mambo ya Ndani, Kangi Lugola

DAR ES SALAAM: Waziri wa sasa wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameshtukiwa na baadhi ya wananchi kutokana na moto wake wa kuitendaji aliokuja nao kiasi cha kuwagawa watu huko mtaani.

Hayo yamekuja ikiwa si siku chache tangu ateuliwe ‘kuvaa viatu’ vya aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk. Mwigulu Nchemba aliyeenguliwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, ni ‘viatu’ vya wiraza hiyo kumpwaya.

Ndani ya siku 9 baada ya kuapishwa, Kangi amefanya matukio yaliyowashangaza wengi, moja likiwa ni lile la kuwachukulia hatua maafisa wa polisi wa mkoa wa Mbeya, Kamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani, Mrakibu wa Polisi, Leonard Funguo na amebaki na nyota tatu kutokana na kukithiri kwa ajali na amemshusha cheo Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Kagera, Mrakibu Mwandamizi,George Mrutu kutokana kutokuwepo eneo la tukio la moto mkoani kwake.

Tukio la pili ni lile la kumchukulia hatua Kamishana Mkuu wa Magereza nchini, Dk. Juma Malewa kwa kuchelewa kufika katika kikao kilichojumuisha maafisa mbalimbali wa wizara hiyo baada ya kiongozi huyo kuchelewa kwa dakika tano hivyo kumtimua.

Tatu ni kutinga kwenye hafla ya ujio wa ndege mpya ya Dreamliner Boeing 787-8 iliyowasili nchini na kufanyiwa hafla ya mapokezi katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar juzi akiwa ameshika ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuionesha kwa waalikwa, jambo lililowafanya baadhi wamshangilie na wengine kuguna.

Kufuatia matukio hayo na mengineyo, baadhi ya wananchi walioongea na Uwazi hivi karibuni walionesha kuushutukia moto wa waziri huyo huku wakihoji kama kweli utadumu katika utawala wake wizarani hapo.

Wananchi hao walifunguka hayo baada ya kumuona waziri huyo akitinga katika mapokezi hayo ya ndege akiwa ametinga shati lenye mifuko yenye rangi za bendera ya taifa na kohoji kama kile anachokifanya kitadumu.

“Niseme tu kwamba, kwanza anapendeza sana na lile shati lake lenye mifuko ya rangi za bendera ya taifa lakini najiuliza kwamba, hivi ataweza kuvaa vile katika kila hafla? Nimeona pia ana ile ilani ya CCM, napo najiuliza ataenda nayo kila sehemu? Lakini najiuliza tu kuhusu huu moto wake…acha nisimalizie…” alisema Jonhson Kibwe wa Konondoni jijini Dar.

Naye Faraja Ali alisema, anavyoona yeye wizara aliyopewa Kangi inahitaji kwenda ‘asteaste’ lakini kwa mwendo anaokwenda nao wa kininja, hajui mwisho wake.

“Unakumbuka moto alioingia nao Augostine Mrema enzi zile alipokuwa waziri wa wiraza hiyo, aliingia na moto kama huuhuu wa Kangi, nahisi anaweza kufanya mambo makubwa kwenye wizara huyo lakini kuna mambo naona hatadumu nayo, kama hili la kuvaa mashati yenye rangi za bendera ya taifa, hili la kutinga kwenye mialiko na ilani ya CCM, acha tuone,” alisema dada huyo.

Aidha, baadhi ya watu walioonesha kumfuatilia kiongozi huyo kwa muda mrefu hata kabla ya kupewa wizara hiyo walisema kuwa, wanaona mabadiliko makubwa sana kwenye wizara hiyo kwani Kangi anaweza kusimamia mambo.

“Yule jamaa muone hivihivi, ile wizara nakuambia itanyooka tu, kuna watu wanaonesha kumshutukia kuwa moto alioanza nao ni wa kifuu lakini mimi nakuambia, ule moto ni wa petroli, si tupo hapa, utaona mambo yake,” alisema Rashidi Kali wa Masaki jijini Dar na kuongeza;

“Kama ni hilo la kuvaa shati lenye mifuko ya rangi za bendera ya taifa ni kuamua tu, anaweza kuhakikisha mashati yote yanakuwa nayo, hakuna kinachoshindikana na mimi najua ana maana yake, kama anavyofanya Mwigulu kuvaa skafu ya rangi hizo, huyu naye kaja na staili hii, tumuache afanye kazi aliyotumwa na rais.”

Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Kangi ili kuzungumzia maoni hayo ya wananchi lakini hakupatikana ila baada ya kuteuliwa aliwahi kusema kuwa, kwa kupewa wizara huyo atahakikisha mambo yanakwenda sawia na tayari ametoa maelekezo ikiwemo kuhakikiwa leseni za madereva nchi nzima ili kuepusha ajali.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI

Comments are closed.