The House of Favourite Newspapers

Kansela Scholz: Putin Hatoshinda Vita Ukraine, Rais Putin Akikiri Vikwazo ni Tatizo

0
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.

 

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amerejelea kauli yake kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin hatoshinda vita nchini Ukraine, wakati Rais Putin naye akikiri kwamba vikwazo vya magharibi vimetatiza mauzo yake.

 

Kansela Scholz ametoa kauli hiyo katika siku ya mwisho ya mkutano wa Jukwaa la kiuchumi mjini Davos, Uswisi, akisema kwamba Putin “tayari ameshindwa kufikia malengo yake yote ya kimkakati”. Aidha Kansela Scholz amesema “ukatili wa vita ya Urusi” umechochea mataifa mawili kujisogeza karibu na Jumuiya ya kujihami NATO, akimaanisha nchi za Finland na Sweden ambazo zinataka kujiunga na muungano huo.

 

Katika hotuba yake, Scholz amewaeleza washiriki wa jukwaa hilo la kiuchumi kwamba Putin alidharau mshikamano wa kundi la mataifa saba yaliyopiga hatua kiviwanda, NATO na Muungano wa Ulaya jinsi walivyoshughulikia uvamizi wake. Ameongeza kuwa “Unyakuzi wa Urusi wa kuikamata Ukraine yote unaonekana kufifia kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa vita na hiyo ni kwasababu ya ulinzi wa jeshi la Ukraine na watu wake”.

 

Wakati matamshi hayo yakitolewa mjini Davos, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Liz Truss naye amenukuliwa siku ya Alhamis kwamba nchi za magharibi zinatakiwa kuhakikisha kwamba Putin anashindwa katika vita hivyo na kuendelea kuisaidia Kyiv bila ya kutetereka.

Truss ameyasema hayo mjini Sarajevo baada ya kukutana na waziri mwenzake wa Bosnia Bisera Turkovic, na kuongeza kuwa “uvamizi wa Urusi usiruhusiwe tena kuvuruga amani ya Ulaya”.

 

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwishoni mwa Februari uliongeza hofu ya kuongezeka kwa mivutano katika eneo lenye hali tete la Balkan, ambalo kijadi limekuwa na mpasuko kati ya Mashariki na Magharibi, na ambapo Urusi inajaribu kuongeza ushawishi wake.

 

Hayo yakijiri, Rais Vladimir Putin amesema kwamba vikwazo vya magharibi dhidi ya Urusi vimetatiza usambazaji wake, lakini akaongeza kwamba hilo halitofanikiwa kuitenga nchi hiyo na teknolojia.

Akizungumza kwa njia ya vidio na viongozi wa zamani wa mataifa ya Sovieti, Putin amesema Urusi itaendelea kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta mbadala wa mauzo ya nje, licha ya kwamba hilo sio mwarobaini wa yote. Ameongeza kuwa katika hatua fulani Urusi imepata hasara lakini hilo limeifanya nchi izidi kuimarika.

 

“Washirika wetu wengi wa Ulaya wametangaza kuondoka Urusi. Unajua! wakati mwingine unaangalia wale wanaoondoka, unasema asante Mungu. Tutachukua maeneo yao. Biashara yetu, uzalishaji wetu tayari umeongezeka na kukua. Tutaketi salama kwenye maeneo yaliyoandaliwa na washirika wetu. Hakuna kitakachobadilika.”

Urusi imezidi kutengwa na nchi za magharibi tangu ilipoivamia Ukraine miezi mitatu iliyopita katika kile inachokitaja kuwa ” operesheni maalum ya kijeshi”. Makampuni mengi yameondoka nchini humo huku vikwazo vikali vikilenga uchumi na biashara za Urusi. Putin amesema kuwa kuondoka kwa baadhi ya makampuni ya kigeni katika soko la Urusi kunaweza kuwa jambo jema.

UNYAMA: MTOTO WA MIAKA (8) ALAWITIWA, , WAZIRI ACHARUKA, ATINGA KUONGEA NA FAMILIA…

Leave A Reply