The House of Favourite Newspapers

Kariakoo Women Dabi Kinawaka leo Alhamisi Kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar

0
Wachezaji wa Yanga Princess.

VITA ya Dabi ya Kariakoo kwa timu za Wanawake, Simba Queens na Yanga Princess, inaunguruma leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2022/23, timu zote zitaingia uwanjani zikiwana makocha wapya. Simba Queens ambao ni wenyeji, wanaongozwa na Charlse Lukula, huku Yanga Princess kocha wake ni Sebastian Nkoma.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Nkoma alisema: “Nimepokea kikosi muda mfupi, hiyo haina maana kwamba tutashindwa kuleta ushindani, tunawaheshimu wapinzani wetu, wana benchi zuri la ufundi na wachezaji wazuri, lakini tumejiandaa kupata ushindi.

“Ni dabi, sio mchezo mwepesi, tumejipanga vizuri kwa ajili ya kupata matokeo mazuri, tunaamini kwamba itakuwa ni burudani nzuri, mashabiki wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwa pamoja nasi.”

Nahodha wa Yanga Princess, Amina Bilal, amesema: “Dabi huwa na maandalizi tofauti na mechi nyingine hasa ukizingatia kwamba kila timu ni kubwa na kuna mashabiki wengi wanakuja. Ninaamini kwamba benchi la ufundi limejiandaa kutupa mbinu nzuri ambazo zitatupa matokeo bora.”

Kwa upande wa Charles Lukula ambaye ni Kocha Mkuu wa Simba Queens, amesema: “Mbinu zote kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wetu zimekamilika, ni suala la kusubiri na kuona namna tutakavyosaka matokeo mazuri kwa kuwa makosa ambayo tulifanya kwenye mechi zilizopita tumeyafanyia kazi ili kuzidi kuimarika.”

Opah Clement, Nahodha wa Simba Queens, amebainisha kwamba: “Tumeshiriki mashindano ya kimataifa, pia hapa ni mabingwa watetezi, ambacho tunataka ni kutwaa ubingwa kwa mara nyingine ili kurejea kuiwakilisha nchi kimataifa.”

Mchezo huo ambao unatarajiwa kuanza saa 11:00 jioni, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema hakutakuwa na kiingilio, hivyo ni fursa kwa watu wote kwenda kushuhudia mtanange huo.

STORI: LUNYAMADZO MLYUKA

WATANO WAFYEKWA YANGA, SAIDO APITISHWA RASMI SIMBA, KWA KASI YA YANGA SIMBA WAJIPANGE…

Leave A Reply