The House of Favourite Newspapers

Karibu Ramadhani, Ni Nguzo ya Nne ya Uislamu!

0

 

 

Baada ya shahada, swala tano, kutoa zaka, ni kufunga Ramadhani na kuhiji Makka. Kwa wasioswali, hawatoi zaka, hawaendi kuhiji, wasipofunga Ramadhan uislamu wao unabaki tete sana.

 

Kufunga ni rahisi. Ni kujizuia kula na kunywa chochote. Jua likichomoza (alfajiri) mpaka lichwe (magharibi).

Mfungaji anatakiwa awe mtu mzima (ameshabalehe) sio kichaa na awe ni mwenye afya nzuri.

Mgonjwa au aliye safarini ruhusa kutokufunga na kulipa hiyo funga kwa kufunga baadae.

 

Mzee au mtu asiyemudu kufunga kabisa kwa ugonjwa kama vidonda vya tumbo pia ruksa kutokufunga. Anaweza kutoa fidia ambayo ni kumlisha mtu mmoja kwa kila siku aliyoacha kufunga.

 

Mwanamke mwenye damu ya hedhi (mwezi) au ya uzazi (nifasi) hafungi. Atafunga baadae.

Vilevile mfungaji anatakiwa awe msafi. Asiwe na janaba. Kwa kifupi aoge kabla jua halijachomoza kama alifanya mambo yake usiku.

Yanayovunja funga (swaumu) ni haya;

1. Kula au kunywa kwa makusudi. Kusahau inaruhusiwa.

2. Kujitapisha

3. Tendo la ndoa (mchana) hii ni pamoja na kujichua.

4. Kuchoma sindano au dawa kama za puani na sikio au kuingiza kitu tumboni.

 

Kuna kokolo nyingi mitaani za kukatisha tamaa watu wasifunge kabisa. Nyingine kutoka hata kwa mashehe. Iko hivi; Kufunga ni lazima kwa muislamu. Asiefunga atawajibika. Hivyo ukifunga hata kwa matata matata, dhambi ya aliyeacha kufunga wewe huna.

 

Kusema uongo, ugomvi, kupiga makelele kutukana, kusikiliza muziki, kutoa ushahidi wa uongo, kupikiwa na kimada na balaa zako nyingine unazozijua hazivunji funga yako. Ila zinapunguza au kuondoa malipo ya kufunga kwako na kusamehewa dhambi zako.

 

Tendo la ndoa kwa walioana ruksa. Vinginevyo ni dhambi kama ilivyo miezi mingine. Ukifanya hilo tendo wakati wa umefunga, funga yako inavunjika na utakuwa na adhabu ya kuwalisha watu 60 au kulazimika kufunga siku 60 mfululizo.

 

Kula futari na daku, kunywa maji mengi kwa afya. Moja ya sababu ya kufunga ni kupata afya.
Ukila mivyakula mingi na misukari unapoteza lengo la kufunga.

Nawatakieni mfungo mwema.

Leave A Reply