The House of Favourite Newspapers

Kavumbagu asaini Vietnam, Azam FC yafunguka

0

kavumbagu11Wilbert Molandi, Dar es Salaam

IMEFAHAMIKA kuwa mshambuliaji wa Azam FC, Mrundi, Didier Kavumbagu amesaini Klabu ya Long Tam Long An inayoshiriki Ligi Kuu ya Vietnam.

Awali, mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea Yanga, alikuwa akiwindwa na Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Timu hiyo ya Vietnam alikuwa akiichezea Mtanzania, Danny Mrwanda kabla ya kurejea nchini na kujiunga na Yanga na baadaye Majimaji ya Songea.

Kwa mujibu wa taarifa lilizozipata Championi Jumamosi, Kavumbagu anajiunga na timu hiyo kama mchezaji huru baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

“Kavumbagu amesaini mkataba wa kuichezea Klabu ya Long Tam Long An inayoshiriki Ligi Kuu ya Vietnam, hiyo ni baada ya kufikia makubaliano na klabu hiyo.

“Awali, kabla ya mshambuliaji huyo kusaini mkataba huo, alikuwa akitakiwa na Mbeya City ambayo ilishindwana naye kutokana na kuhitaji dau kubwa la shilingi milioni 40,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba kuzungumzia usajili wa mshambuliaji huyo, alisema wao hawana taarifa za mshambuliaji huyo kusajiliwa huko, wao wanachofahamu mchezaji huyo mkataba wake ulimalizika msimu huu wa ligi kuu.

“Na kingine wachezaji wote ambao mikataba yao imemalizika na wengine wote hatma yao itaamuliwa mara kocha wetu atakaporejea nchini Julai Mosi, mwaka huu na timu kuingia kambini,” alisema Kawemba.

Leave A Reply