The House of Favourite Newspapers

Kaze Noma! Apitisha Panga Kali Yanga

0

KUMEKUCHA! Ndivyo utakavyoweza kusema hivi sasa ni baada ya baadhi ya wachezaji wa Yanga kuanza kuwaaga wenzao wanaotarajiwa kuachwa na wengine kutolewa kwa mkopo katika dirisha dogo la usajili msimu huu.

 

Hiyo ni katika kuelekea usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu na tayari Yanga wamekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Mrundi Saidi Ntibazonkiza.

Timu hiyo iliyokuwepo katika mipango ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, pia ipo kwenye mipango ya kuwatoa kwa mkopo baadhi ya wachezaji katika dirisha hilo dogo.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Kocha wa Yanga, Cedric Kaze ndiye aliyependekeza kuwatoa mastaa hao kwa mkopo kwa lengo la kupata nafasi ya kucheza ili warejeshe viwango vyao.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kocha huyo amefurahishwa na viwango vyao, lakini anawatoa kwa mkopo kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi chake.

 

Alisema kuwa baadhi ya wachezaji wameondoka tayari kwenye kambi ya timu hiyo muda mrefu kati ya hao ni Abdulaziz Makame aliyekuwepo kwao visiwani Zanzibar akisubiria wapi atakapopelekwa kwa mkopo.

 

Aliwataja wachezaji wengine watakaotolewa kwa mkopo ni Juma Mahadhi, Adeyum Saleh, Waziri Junior, Paul Godfrey ‘Boxer’, Said Makapu na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.“

Kocha wa Yanga, Cedric Kaze

Kocha tayari amekabidhi ripoti yake ya usajili ambayo imeanza kufanyiwa kazi kwa muda mrefu na viongozi ambao wamefanikisha usajili wa Saido atakayeanza kuichezea Yanga kuanzia Desemba 15, mwaka huu mara baada ya dirisha dogo kufunguliwa.“

 

Katika ripoti hiyo pia kocha ametoa mapendekezo ya wachezaji wa kuwatoa kwa mkopo ambao wamepewa taarifa na uongozi na tayari wameanza kuaga kwa wachezaji wenzao.“

 

Makame yeye muda mrefu ni kama amejitoa katika timu baada ya kusikia tetesi za kutolewa kwa mkopo na kocha kuwatoa kwa mkopo siyo kwamba hawana uwezo kikubwa wamekosa kuleta ushindani kwa wachezaji wenzao,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Kaze hivi karibuni alisema kuwa: “Hivi sasa siwezi kuzungumzia usajili na badala yake akili zangu nimezielekeza kwenye ligi na kikubwa ninataka kushinda michezo yote tuliyoibakisha kwa lengo la kuendelea kukaa kileleni kwenye msimamo.”

Stori na Wilbert Molandi na ibrahim Mussa, Dar

Leave A Reply