The House of Favourite Newspapers

Kazi imekwisha!

0

lowassa kura

Edward Lowassa aliyekiwakilisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akipiga kura pamoja na mkewe.

Waandishi Wetu
Kazi imekwisha! Huo ndiyo msemo unaoweza kuelezea vizuri hali ya kisiasa nchini baada ya jana, Oktoba 25, 2015 Watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuwachagua rais, wabunge na madiwani kwenye uchaguzi mkuu.

Timu nzima ya Gazeti la Ijumaa Wikienda ilikuwa ikifuatilia mchakato mzima na hapa inakuletea mtiririko wa yaliyojiri maeneo mbalimbali ya nchi:

MAGUFULI, LOWASA WAPIGA SALA
Wagombea urais wenye nguvu zaidi, Dk. John Pombe Magufuli aliyepeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa aliyekiwakilisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa nyakati tofauti walionekana wakisali kabla ya zoezi la upigaji kura, Magufuli akiwa kijijini kwao, Chato, Geita na Lowassa akiwa Monduli mkoani Arusha.

MIMBA FEKI ZAIBUKA
Katika zoezi la upigaji kura, vituko havikosekani. Wanawake wengi walikuwa wakitumia ujanja wa kutengeneza mimba feki kwa kujiwekea matambara tumboni, ili wapate urahisi wa kupiga kura hasa ikizingatiwa kwamba wajawazito, wagonjwa, wanaonyonyesha, walemavu na wazee walikuwa wakipata upendeleo maalum wa kupiga kura bila kukaa kwenye foleni kama wananchi wengine.

MPIGAKURA AKUTA MAUZAUZA KITUONI
Mpigakura mmoja (jina halikufahamika mara moja) wa Tegeta Kibaoni, Dar alijikuta akikosa haki yake ya msingi ya kupiga kura baada ya jina lake kuonekana limetumiwa kupiga kura na mtu mwingine huku wakala akimtuhumu kuwa tayari ameshapiga kura na anataka kurudia awamu ya pili baada ya kubadilisha nguo, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Hata hivyo, mhusika aliendelea kushikilia msimamo huku akionesha kidole chake kidogo cha mkono wa kushoto ambacho hakikuwa na wino, kuthibitisha kwamba ni kweli hakupiga kura.

WATOTO WAGEUKA ‘DILI’ MITAANI Vimbwanga vingine vilivyoibuka jana ni baadhi ya wapigakura (wanawake) kubuni mbinu mpya ya kwenda na watoto wa kuazima katika vituo vya kupigia kura ili wapate urahisi wa kutopanga foleni, jambo lililosababisha watoto wadogo kugeuka dili mitaani kwa kila mtu kujifanya ananyonyesha au ana mtoto mdogo.

“Yaani kwa mfano mimi mwanangu Elisha mwenye miezi nane, jana hakushinda nyumbani, majirani walikuwa wanakuja kumchukua na kwenda naye kwenye vituo vya kupigia kura,” alisema mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Mama Elisha, mkazi wa Vingunguti, Dar.

magufuli

Mgombea urais, Dk. John Pombe Magufuli akipiga kura.

BAADHI YA WANANCHI WASHINDWA KUPIGA KURA
Tukio jingine la kusikitisha lilitokea katika vituo vya kupigia kura vya EDP Royal na Stop Over A na B, Kimara jijini Dar kushindwa kupiga kura katika muda uliopangwa kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kupigia kura, zikiwemo karatasi.

VIFAA VYACHOMWA MOTO
Hali ilizidi kuwa tete kwa baadhi ya wananchi wasio na hekima wa Jimbo la Kwera mkoani Rukwa kuvichoma moto vifaa vya uchaguzi kwa tuhuma kuwa kulikuwa na kura zilizokwishapigwa tayari.

MABOMU YARINDIMA TANDALE, DAR
Wakati gazeti likiwa kwenye hatua za mwisho za maandalizi kabla ya kwenda mitamboni, mwandishi wetu aliripoti taarifa za kutokea kwa fujo katika eneo la Shule ya Msingi Tandale, Dar baada ya vijana wasiofahamika ni kutoka chama gani, kuanzisha fujo na kuwalazimu jeshi la polisi kutumia mabomu ya machozi.

VITUO VYABADILISHWA ‘KINYEMELA’
Katika kituo cha kupigia kura cha St. Peters, Kimara, Dar, wananchi wa hapo walilalamikia kuhamishwa ghafla kwa kituo chao na kupelekwa Mavurunza.
“Ajabu ni kwamba majina yetu yamebandikwa hapa na vifaa vya kupigia kura vililetwa na askari walivilinda usiku kucha lakini tulipofika asubuhi tumeambiwa kituo kimehamishwa. Wazee na wagonjwa walijipanga kupiga kura hapa, sasa huko walipohamishia kwa nini wasiseme jana?” aliuliza Saidi Ali mkazi wa eneo hilo.

lowassa1Gazeti hili lilifika katika kituo cha Mavurunza na kukutana na kiongozi wa kituo hicho ambaye hakutaka kuandikwa jina gazetini, akakiri kuhamishwa kwa kituo hicho.
Nao wananchi wa Kituo cha Shule ya Msingi Malamba Mawili jijini Dar walilalamikia kucheleweshwa kwa vifaa vya kupigia kura.
“Tumekuja saa kumi na moja alfajiri lakini tumeambiwa hakuna masanduku ya kura na vituo vingine havina wino, huu ni usumbufu mkubwa,” alisema mpiga kura aliyejitambulisha kwa jina la Pili Mohamed.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Malamba Mawili, Kilo Waziri alipoulizwa juu ya matatizo hayo alikiri kuyafahamu.

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo, pia walilalamikiwa kuhamishiwa katika Kituo cha Msigani, Mbezi, Dar bila kutaarifiwa kabla.

MATOKEO KUTANGAZWA LEO
Mpaka tunakwenda mitamboni, habari zilizotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene zimeeleza kuwa matokeo yatatangzwa leo kwa awamu nne; saa tatu asubuhi, saa sita mchana, saa tisa alasiri na saa 12 jioni.

Leave A Reply