The House of Favourite Newspapers

Kiba King Anatembea Njia za Darassa?

0
Alikiba.

SEDUCE ME, ndiyo habari ya mjini, hili halina ubishi. Kwamba King Kiba, amerejea kwenye ubora wake wa enzi baada ya kazi kubwa ya kuchungulia kila aina ya tobo ili kuweza kujua wapi kuna upenyo, apenye.

Ali Kiba ni msanii mkubwa, hili pia halina ubishi. Ni mmoja wa watu ambao walifanikiwa kuugeuza muziki wa Kizazi Kipya kuwa mali yake binafsi, akiufanya vile alivyotaka, nao ukatii, mithili ya vile Ronaldinho Gaucho alivyoufanya mpira wa miguu.

Haimaanishi kuwa enzi zake hakukuwa na wasanii wengine waliofanya vizuri, la hasha, walikuwepo kama ambavyo wanasoka wa enzi za Ronaldinho walivyo-kuwepo, lakini hawa-kufikia levo zake. Yeye alikuwa katika kiti ambacho wengi walitamani kukikalia, lakini wakakosa vigezo.

Pengine alishafika alipotaka, Kiba akaamua kupumzika muziki na kuufanya kwa hobi tu, ndipo watu wakachomoza na kukalia kiti kilichokuwa wazi. Hata aliporejea, kwa jeuri ya kujiamini, alisema anarejea kukalia kiti chake, kwani kipo wazi, anachotakiwa kufanya ni kukifuta vumbi tu!

Haikuwa rahisi na haiwezi kuwa rahisi. Kwa muda mrefu tangu aliporejea katika muziki wa ushindani, amekuwa akitarajiwa wakati wowote kurejea kiti chake, na kwa mashabiki wake ambao wamewehuka, wamekuwa wakimuweka Kiba kuwa juu ya wasanii wote kwa sasa.

Ninafahamu kazi ya Kiba, yule wa kipindi kile alipokuwa ameshika hatamu, kuanzia utambulisho wake wa Cinderela. Kila mmoja alimfahamu kwa sababu kila kibao alichoachia, kili-Hit.

Darassa.

Nakshi Mrembo, Usiniseme, Dushelele, Single Boy, Macmuga, Mapenzi yana-run Dunia ni baadhi ya nyimbo zake ambazo kila mmoja ulikuwa juu ulipotoka. Lakini baada ya mapumziko yake ya karibu miaka mitatu, Kiba alirejea na vibao vingi.

Aje, Mwana, Chekecha Cheketua ni baadhi ya kazi zake za awamu ya pili. Zilikuwa nzuri na zikapendwa, lakini hazikuweza kurejesha hadhi yake katika msitu uliojaa wasanii wengi wanaoshindana kwa kazi nzuri.

Kuna kitu kimoja ambacho mashabiki wa muziki, kumbuka, nazungumzia mashabiki wa muziki, siyo mashabiki wa Kiba, wanakizungumza. Kwa muda wote tangu aliporejea, King Kiba alikuwa anabebwa na ukubwa wa jina lake na siyo ubora wa kazi zake.

Nyimbo na video zake zilikuwa za kawaida tu, ambazo zingeweza kushindanishwa na wasanii wengi vijana. Lakini kuna hiki kitu, cha ajabu kabisa, Seduce Me. Ni moja kati ya nyimbo kali ambazo Kiba amewahi kufanya.

Kimepokelewa vizuri, vizuri sana. Mashabiki wa Kiba wanaamini sasa mtu wao amesharejea kileleni, kwamba hakuna tena wa kumsumbua. Sijawahi kuwa mtabiri, kwa hiyo siwezi kuungana nao wala kubishana nao, chini ya jua, lolote linawezekana.

Katika nukuu nyingi za Bruce Lee, yule mkali wa sanaa za mapigano, mojawapo alipata kusema “Ni rahisi sana kupambana ili kuwa staa, lakini ni ngumu mno kupigana ili kubakia kuwa staa”.

Miezi michache iliyopita, ilikuwa ni wakati wa Darassa na kibao chake cha Muziki. Alisumbua sana na baadhi wakamtabiria kuwa nyakati zinaelekea upande wake. Yaweza kuwa siyo sawa pengine kumlinganisha Kiba na Darassa, lakini unapozungumzia kuhusu sanaa ya muziki, hakuna kitu ‘permanent’.

Kupokewa vizuri kwa Wimbo wa Seduce Me hakujatokea tu kwa sababu ya uzuri wake. Kuna vitu vingi vimechangia watu kuupa hadhi uliyonayo hivi sasa na Kiba kama msanii anajua. Kuna mambo ya ndani na nje ya uwanja.

Ingawa aliingiza pesa nyingi na kuvuma kwa jina lake, Wimbo wa Muziki umemponza sana Darassa. Jaribio lake la kwanza la kutoa kazi nzuri kuliko Muziki limegonga mwamba na kwa udogo wa jina lake kisanii, huenda asipate tena ‘mileage’.

King Kiba anatakiwa kutoa singo bomba zaidi itakayokamata kuliko Seduce Me, ili kuthibitisha kuwa kweli Mfalme amerejea, vinginevyo endapo atategemea ukubwa wa jina lake kuzibeba nyimbo zake, atafeli. Mimi siyo shabiki wa Kiba, ni shabiki wa muziki.

Seduce Me ni bonge la ngoma, kali kinyama. Lakini bahati mbaya wimbo huu umefanywa na msanii mwenye jina na ‘fanbase’ kubwa.

Lakini mbaya zaidi ni kuwa wimbo huu umetoka wakati kukiwa na upinzani mkali miongoni mwa mashabiki juu ya ubora wa Kiba na wapinzani wake. Ana deni la kuthibitisha kuwa alichokifanya, ni baada ya kazi ya muda mrefu ya kuchungulia ‘matobo’ na kuja kubaini njia sahihi ya kukata ngebe za wapinzani wake!

Makala: Ojuku Abraham

 

Cheki Roma Alivyokwepa Swali Kuhusu Magufuli na Lowassa, Lazima Ucheke

Leave A Reply